Jipu ni uvimbe mkubwa unaotunga usaha. Chanco cha jipu kuota sehemu yoyote ya mwili wa mtu ni bacteria, viumbehai vidogo sana visivyoonekana kwa macho ila kwa hadubini, ambavyo huingia sehemu fulani ya mwili na kuozesha sehemu hiyo baada ya kuwashinda selidamu nyeupe katika mapambano makali.
Hapana mtu yeyote anayependa kupata jipu kwa sababu ni ugonjwa kama magonjwa mengine ambayo hudhoofisha afya ya mtu. Jipu linauma, linavuta na linapwita na kuleta usumbufu mkubwa hata kusababisha homa kali. Afueni haipo upatapo jipu hadi liive na uliminye na kulikamua litoke usaha.
Kutoa usaha tu hakutoshi wala hakuna maana ya kueleweka iwapo hujatoa moyo wake kwa sababu litaota tena baada siku chache zijazo na kukuletea maumivu makali na utashindwa kutimiza shughuli zako. Tiba kamili ni kuliminya hadi moyo wote utoke. Moyo wake ni usaha na damu zilizochanganyika pamoja.
Usiombe kuumwa jipu na wala usiombe kupata jipu sehemu ya kichwani, kwapani au maeneo ya siri ya mwili wako. Utalia na kusaga meno jinsi maumivu yalivyo makali. Utamtafuta aliyekupa jipu na wala hutamwona. Hilo ndilo jipu la mwilini mwa mtu.
Siku hizi, Rais John Pombe Magufuli ametumia neno jipu na kulifanya kuwa istilahi inayowakilisha dhana ya kisiasa katika mambo ya uchumi, uongozi, utawala, wajibu na maadili yasipotendwa kufuata taratibu zake zilizowekwa na mamlaka husika. Hilo ni jipu kwa mtendaji au msimamizi.
Jipu, istilahi mpya ya kisiasa. Sielewi mtani wangu na Rais wangu aliwaza vipi na alikerwa kiasi gani hata kubuni kasoro hizo ni majipu na kuja na istilahi hii ‘dhana ya utumbuaji majipu’, dhana iliyoeleweka na kukubalika haraka na Watanzania na watu wa mataifa mengine duniani. Heko na kongole Rais John Pombe Magufuli.
Kuwa na fedha au mali nyingi kutokana na njia za ujanja-ujanja, ukwapuzi, kula rushwa, ufisadi au udhulumati nafsi ya mtu au watu ni tendo haramu. Na hilo ndiyo jipu linalostahili kutumbuliwa. Lakini kuwa na fedha au mali nyingi kutokana na njia halali si jipu na hustahili kutumbuliwa.
Mtu anayetuhumiwa ana mali au amejilimbikizia mali kwa njia haramu ni hati ya kuitwa jipu na anastahili kuwekwa kitimoto aeleze alivyoipata mali hiyo. Ikiwa njia ni halali siyo tabu. Kinyume chake ndiyo shida ilipo na ndipo unapokuwa jipu na lazima atumbuliwe.
Aidha, jipu kisiasa inaweza ikawa na maana pia ya mtu au watu wavivu, wazembe, wababaishaji, wapuuzaji na wengine kama hao wapo kulea kasoro katika taratibu, kanuni, na sheria za kazi alizopangiwa na kuweka kero kwa wananchi. Mtu kama huyo ni jipu, anapaswa kutumbuliwa bila ya kuonewa soo. Majipu yako mengi na yanatumbuliwa katika maeneo mbalimbali kuanzia kwanye Serikali na taasisi zake na mashirika ya umma kwa sababu wahusika wanashiriki kuhujumu uchumi wa nchi. Majipu kama hayo wala yasisubiriwe hadi yaive kwani yanakera na yanaaibisha Taifa.
Kwa muda mrefu wananchi kote nchini wameuguza majipu kwa karaha na vilio visivyokuwa na wabembelezaji na wala wasijue la kufanya. Majipu yametoa harufu mbaya na kuudhi pua zivutazo. Macho ya majipurukusha kujenga mazoea ya kuona majipu ni kama burudani na nyoyo kukereka na kutukutika.
Ingawaje dawa na watumbuaji walikuwako, hawakufaulu kuyatumbua na kuyatibu. Walitibu kwa huba na moyo wa jipu kubakizwa. Leo, watumbuaji wamepatikana tena mabingwa. Tayari baadhi ya wananchi waliokerwa na harufu mbaya na mioyo kusononeka wameanza kutoa lawama na kueleza utumbuaji hauna huruma.
Ndipo mtumbuaji mkuu aliposema mbona walipokuwa wakiota kama uyoga hawakuwa na huruma? Waliota hadi maeneo ya siri. Vipi leo watumbuliwe kwa huruma? Hiyo imekula kwenu na kwao. Mwendo mdundo hadi kieleweke. Jipu ni jipu – liwe la hadharani au la sirini litumbuliwe tu.
Tuache kuona majipu ni mafisadi au wala rushwa tu. Hapana. Nafsi yako kuweka kinyongo na baadaye kumsulubu mtu au kumpendelea mtu na kumpa madaraka ilhali hana sifa na uwezo, wewe na yeye ni majipu. Nafsi yako kudhulumu nafsi nyingine – iwe katika biashara au ujira, wewe ni jipu.
Wananchi hatuna budi kuendelea kuwaunga mkono watumbuaji ili nchi irudi kwenye reli yake na kujenga heshima ya watu wake. Rais Magufuli si wa kwanza kutumbua majipu duniani.
Wapo viongozi katika nchi kadhaa walifanya hivyo kwa maslahi ya wananchi. Mathalani, Wachina walitumbuliwa majipu enzi za uongozi wake Mao Tse Tung. Cuba walifanya enzi za Fidel Castro. Warusi walitumbuliwa enzi za Joseph Stalin na Wajerumani enzi za Adolf Hitler. Leo nchi hizo mguu sawa na macho mbele mita mia moja.
Kila lenye mwanzo huwa na mwisho. Nina imani kubwa huu ndiyo mwisho wa majipu iwapo wazalendo tutakuwa wamoja ndani ya chombo kimoja. Rais wetu, John Pombe Magufuli, usiyumbe wala kutetereka, wananchi wako nyuma yako na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe na Serikali yako. Mungu ibariki Tanzania.