Katika matoleo yaliyopita, gazeti la JAMHURI limeandika kwa kina taarifa ya uchunguzi juu ya mbinu zinazotumiwa na SABmiller kutolipa kodi sahihi. Katika toleo la leo tunakuletea sehemu ya mwisho ambayo ni ushauri kwa Serikali jinsi inavyoweza kupunguza mianya ya kutolipa kodi sahihi. Endelea…
Nchi tajiri 20 (G20) na Jumuiya ya Ulaya (EU) zinapaswa kutoa mamlaka ya kisiasa kwa Bodi ya Viwango vya Uhasibu vya Kimataifa, ili iweze kuandaa kanuni zitakazokuwa na mamlaka duniani kote kuyataka mashirika ya kimataifa ikijumuisha nchi kwa nchi, kutoa taarifa za msingi katika hesabu zao zilizokaguliwa.
Nchi zinazoendelea hazipaswi kuachia haki yake ya kupata mrahaba, kukubali kutozwa kodi za usimamizi (management fees) na malipo mengine kabla ya kutoza kodi ya mapato. Inaumiza kwamba kodi inayopotezwa na nchi za Ghana na Zambia kutokana na mipango ya kuficha mapato halali tulizogundua zimeongezeka kutokana na mpango wa kulipishana kodi mara mbili chini ya mkataba wa nchi za Uswisi na Uholanzi.
Mkataba huo unapunguza wigo wa kodi ya zuio unaoweza kutozwa malipo wanayolipwa ikilinganishwa na viwango vya kodi za nchi. Huu haupaswi kuwa utaratibu unaopaswa kufanywa na nchi zilizoendelea dhidi ya nchi maskini kwa nia ya kuyasaidia mashirika ya kimataifa. Nchi zilizoendelea nazo zinapaswa kuchunguza ambapo kunahitajika mabadiliko jinsi kampuni za kimataifa zinavyoepuka kodi katika nchi zinazoendelea.
Kwa mfano, nchini Uingereza mabadiliko ya sheria dhidi ya kuepuka kodi yaliyopendekezwa yajulikanayo kama kampuni zinazomilikiwa kimataifa, yataziumiza nchi zinazoendelea kwa kuondoa adhabu zinazotolewa kwa kampuni za Uingereza – kampuni za Uingereza zinazokwepa kodi kwenda nchi nyingine isipokuwa zikikwepa kwenda Uingereza.
Nchini Uholanzi wanapaswa kuweka sheria inayozuia uepukaji kodi kuepusha unyonyaji ulioandaliwa chini ya mtandao wa mikataba ya kutolipa kodi mara mbili inayotumiwa kama njia ya kukwepeshewa mapato. Kwa mfano, kodi ya zuio katika riba na mirahaba inayolipwa katika nchi ambazo ni pepo ya kodi haitozwi kodi.
Nchi za G20 na EU zinapaswa kufanya kazi pamoja na kuweka mikataba itakayoweka masharti mapya yatakayozuia nchi zote duniani kuendelea kuwa na sheria zinazowezesha ukwepaji kodi hasa hasa kutoka nchi zinazoendelea. Hii inapaswa kuhusisha wadau wa maendeleo duniani kuruhusu ubadilishanaji wa taarifa za kodi za kampuni za kimataifa kimkataba.
Nchi zinazoendelea haziwezi kutatua tatizo hili peke yao, mikataba watakayoiandaa ya kuzuia malipo nje ya nchi bila kulipiwa kodi haiwezi kuwa na nguvu bila kushirikisha nchi zilizoendelea. Vivyo hivyo, Umoja wa Mataifa (UN) unapaswa kuhakikisha unakabiliana na mchezo huu wa hatari wa ukwepaji kodi unaodumaza nchi maskini.
Zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa nchi maskini ni uanzishwaji wa mfumo utakaozizuia kampuni kubwa za kimataifa kugawana faida zinayopata kwa kampuni dada kama inavyofanya TBL kupitia Crown Beverage ya nchini Kenya.
Baadhi ya nchi kama Brazil zimeanzisha mfumo wa kutoza kodi kwa kutumia bei ya jumla inayouzwa ndani ya nchi yao bila kujali kuwa vinywaji au bidhaa husika zinauzwa nje ya nchi kwa nia ya kubana ukwepaji.
Kadri mapato ya nchi yanavyozidi kupungua, ndivyo umuhimu wa kupata mapato mengi kutokana na kodi unavyozidi kuwa mkubwa. Ni kwa misingi hiyo Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha inabana mianya ya ukwepaji kodi si kwa TBL tu bali kwa kampuni zote nchini kwa nia ya kupata mapato halali na ya kutosha.