Wiki iliyopita niliahidi kujibu maswali haya: “Je, unafahamu utaratibu wa kisheria wa kusajili Jina la Biashara, gharama ya usajili, muda wa kukamilisha usajili, nyaraka zinazotakiwa, umri wa mtu anayetaka kusajili Jina la Biashara na matakwa mengine ya kisheria? Usikose nakala yako ya Gazeti hili makini la uchunguzi la JAMHURI Jumanne ijayo.”

Sitanii, baada ya makala hii, nimepata maombi mengi. Nimepata simu na ujumbe mwingi wa simu ya mkononi, kiasi nikashawishika mada ya aina ya usajili niendelee nayo wiki ijayo, kwanza nijibu maswali haya maana muda ukipita sana yatapoteza maana.

“Kaka Balile, nafuatilia kwa karibu sana makala hii. Naomba usiiache ukaingia katika kuandika siasa. Huu ndiyo ukombozi. Sisi Watanzania hatujui jinsi ya kufanya biashara. Kupitia makala yako tumeanza kuuona mwanga. Mimi nina shida. Nilikuwa nafuga kuku, ila bei ya vyakula imepanda, bei ya kuuza kuku imeshuka. Dawa za kutibu kuku zimepanda bei. Sasa nawaza kwenda kulima mihogo. Naomba unishauri nifanyeje?”

Huyu ni msomaji kutoka Dodoma. Ujumbe huu ni moja kati ya ujumbe ulionifanya nisitishe kwanza mtitiriko wa makala yangu nisaidie na wengine 20 walioleta ujumbe wa aina hii. Nimemjibu huyu mfugaji wa kuku ila kwa kuwa nimeona tatizo hili linajirudia kwa watu wengi kukata tamaa na kufunga biashara, nikaona bora nisaidie kuepusha balaa.

Sitanii, kwanza kama unafanya biashara yoyote usiiache. Ni matumaini yangu kuwa biashara unayoifanya tayari unaifahamu vema kuliko biashara unayotaka kuijaribu. Cha msingi hapa ni kukaa chini ukaainisha matatizo unayopata katika biashara unayoifanya sasa na ukawaza jinsi ya kupata ufumbuzi.

Kwa mfano, huyu mfugaji wa kuku nimezungumza naye. Ameniambia kuwa soko la kuku lipo la kutosha. Kuku anauzwa kati ya Sh 9,000 na 11,000 kulingana na uzito wa kuku. Katika mazungumzo naye, nimebaini kitu kimoja. Mfugaji huyu, anafuga kuku kama mengineyo. Haifanyi kuwa biashara yake ya msingi inayomweka mjini.

Nimemuuliza kama anayo ratiba ya kuwalisha kuku, banda analisafisha mara ngapi kwa wiki, chanjo kwa kuku anatoa mara ngapi, maji anawawekea kiasi gani bandani, kuku wanakula kiasi gani, anafunga kuku zaidi ya 100 au chini ya kiwango hicho, kilichonisikitisha kila swali ilikuwa anaanza na jibu “inategemea.”

Dodoma ni jiji sasa. Ufugaji wa kuku ukifanywa kwa tija, mfugaji akawa na ratiba na mpango si tu wa kununua chakula, bali hata kuzaisha chakula cha kuku mwenyewe, ataongeza thamani na kupunguza gharama ya uzalishaji au ufugaji wa kuku, hali itakayompatia faida kubwa.

Nafasi inazidi kuwa finyu. Nimepigiwa simu na muuza mbao, duka, chips na wengine wengi. Suala jingine nililobaini watu hawa hawafungi hesabu. Hawakai chini kufahamu aliingiza shilingi ngapi, gharama ya uendeshaji ni shilingi ngapi na faida ni kiasi gani.

Mmoja ameniambia: “Mimi ninauza na kuweka kwenye kopo fedha, kusema kweli wakati mwingi huwa nachukua matumizi ya nyumbani kwenye kopo hilo nanunua vitu vidogo vidogo kama chumvi, kiberiti, sukari na mara chache hutoa hela za mboga kwenye kopo, lakini mimi si mfujaji ila ajabu kibanda changu cha chipsi hakikui nikaweza kulipa ada za watoto. Nadhani kuna jirani yangu ameniwekea chuma ulete kila ninachopata kinakwenda kwake.”

Ushauri wangu kwa kila mwenye biashara ya aina yoyote, ni lazima kufunga hesabu. Ni lazima ufahamu ulichouza, mtaji uliotumia na faida iliyopatikana ni kiasi gani kabla ya matumizi. Ukijenga utamaduni wa kutunza hesabu mara moja utafahamu tatizo la biashara yako liko wapi.

Sitanii, jiepushe na mtindo wa kubadili biashara kama nguo. Unapobadili biashara unapoteza uzoefu katika biashara husika. Kama kwa mfano unauza madaftari, ukihamia kwenye kuuza saruji, basi ufahamu kuwa wateja watabadilika, na mpango wa biashara utapaswa kuwa mwingine. Rejea makala yangu ya kwanza, ya pili na ya tatu juu ya wazo la biashara na mahala pa kufanyia biashara.

Mwisho, nawaomba wasomaji wangu mniruhusu nisiwe nawajibu maswali yenu kwa sasa kwani ni mengi. Nikiingia katika kujibu maswali hayo kama nilivyofanya leo, hakika sitaweza kukamilisha mada hii inayopaswa kuwa na makala zisizopungua 12, zikiwa msingi wa jinsi ya kufanya biashara Tanzania. Tukutane wiki ijayo.