Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kuuliza maswali haya: “Je, mfanyabiashara unaufahamu mwaka wa kodi wa taasisi au kampuni yako? Unafahamu makisio na taarifa ya mapato ya biashara au shughuli zako yanafanywaje? Usikose sehemu ya 22 kupitia Gazeti la JAMHURI kila Jumanne kupata majibu haya.”
Sitanii, niwashukuru tena wasomaji wangu kwa mrejesho mkubwa mnaonipa. Nikiri tena sikufahamu kuwa sekta ya biashara ni nyeti kwa kiwango hiki na watu wanapata tabu mno kutafuta majibu ya jinsi ya kuendesha biashara zao. Nianze kwa kujibu swali la mwaka wa fedha ni upi.
Imekuwa kawaida kwa serikali kusoma bajeti yake inayoanza Julai 1, na kuishia Juni 30, ya mwaka unaofuata. Hili limewafanya watu wengi wakiwamo wafanyabiashara kuamini kuwa mwaka wa fedha wa serikali unakwisha Juni 30. Kimsingi hii imevuruga mipango ya wafanyabiashara wengi, na wengine huendesha biashara bila kuvifahamu vema vipindi vya mwaka wa kifedha kwa biashara.
Kwa maana ya mapato, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inahesabu mwaka wake kwa kutumia kalenda ya kawaida ya mwaka. Hii ina maana mwaka wa biashara au mapato ya mfanyabiashara unapaswa kuanza Januari 1, hadi Desemba 31. Kwa TRA huu ndio mwaka wa mapato.
Ni kwa msingi huu, kampuni inapoanzisha biashara, inaruhusiwa kuunganisha hesabu za kwanza hadi miezi 18 ya mwanzo wa biashara yake, kwa nia ya kuziba pengo la miezi ya katikati ili kuwezesha mwaka wako wa fedha uishie Desemba 31.
Hata hivyo, zipo kampuni zilizoanza siku nyingi, zenye utamaduni wa kipekee, hivyo zinapenda mwaka wake wa fedha uishie mwezi mwingie tofauti na mwaka wa serikali au TRA. Mwaka wa serikali unakwisha Juni 30, na mwaka wa mapato wa TRA unakwisha Desemba 31.
Sitanii, ikitokea hivyo, basi kampuni au taasisi kutokana na sababu zenye kuifanya mwisho wa mwaka wake wa fedha usiangukie Desemba 31, inapaswa kumwandikia barua Kamishna wa TRA kupata kibali cha kubadili kalenda ya mwaka wake wa fedha na kuangukia katika mwezi mwingine tofauti na Desemba 31. Mwaka wa fedha ni muhimu kwa ajili ya ulipaji kodi.
Baada ya kuwa umefahamu mwaka wa fedha wa biashara yako, kuna suala la marejesho ya kodi (tax returns). Kampuni inapaswa kuandaa hesabu zilizokaguliwa na kujaza fomu maalumu ambayo inawasilishwa TRA si zaidi ya Juni 30, ya kila mwaka ikionyesha mapato ya kampuni kwa mwaka uliokwisha Desemba 31, ya mwaka uliopita. Hesabu hizo zinapaswa kuonyesha kiwango cha kodi inayolipwa kwa kila mwaka na faida uliyopata katika biashara.
Ikumbukwe chini ya sheria ya fedha, kampuni inapaswa kuwasilisha hesabu hata kama haina mapato yoyote kwa mwaka husika. Hii ina maana kuwa kama kampuni haikufanya biashara, inapaswa kuandaa hesabu na kuwasilisha hesabu kuonyesha kuwa haikufanya biashara.
Kila kampuni na watu wanaotakiwa kuandaa hesabu zilizokaguliwa (kwa maana kuwa mzunguko wa fedha katika biashara yako ni kuanzia Sh milioni 20 kwa mwaka), wanapaswa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa TRA zenye kuonyesha kodi iliyokisiwa na inatakiwa kulipwa katika mwaka wa fedha.
Kuna fomu maalumu za kujaza. Mfano fomu Na. ITA 202.01.E ni ya kodi ya makisio kwa kampuni au mtu binafsi. Makisio haya yanapaswa kulipwa kama nilivyopata kuandika katika makala zilizotanguliwa, kuwa yanalipwa mara nne kwa mwaka.
Sehemu ya kwanza inalipwa ifikapo au kabla ya Machi 31, sehemu ya pili ifikapo au kabla ya Juni 30, sehemu ya tatu ifikapo au kabla ya Septemba 30 na sehemu ya nne ni ifikapo au kabla ya Desemba 31. Ukichelewa kulipa kodi hizi, unatozwa riba inayokuwa imetangazwa na serikali na faini ya asilimia 5 ya kodi inayopaswa kulipwa kila mwaka.
Ni wajibu wa kila kampuni au mfanyabiashara kuhakikisha kuwa anawasilisha TRA hesabu zilizokaguliwa ndani ya miezi sita baada ya Desemba 31. Hesabu hizi zinapaswa kuthibitishwa na mhasibu mwenye sifa za CPA na anayetambuliwa na NBAA.
Je, unafahamu kiwango na sifa za kukisiwa kodi ya mapato katika biashara? Je, unafahamu kodi nyingine zinazolipwa na mfanyabiashara au kampuni baada ya hizi nilizoziandika? Kama jibu ni ndiyo au hapana, basi usikose nakala ya JAMHURI Jumanne upate majibu sahihi.