Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kuwasisitiza wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni kuhakikisha wanafunga hesabu zilizokaguliwa na kuziwasilisha TRA. Ni imani yangu kuwa wengi kama si nyote mlitekeleza na kama hukufanya hivyo, wasiliana haraka na ofisi ya TRA iliyopo karibu yako, kwani bila kufanya hivyo unahatarisha uhai wa kampuni yako kwa faini za kisheria.
Sitanii, nichukue fursa hii kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) na washirika wake walioandaa tuzo za umahiri katika uandishi. Jumamosi iliyopita Kampuni yetu ya Jamhuri Media Limited imepata tuzo mbili na katika eneo hili la kodi nimekuwa mshindi wa pili. Ni wajibu wangu kushukuru katika kila jambo na kuzidi kuomba kwa Mwenyezi Mungu, kwani ni kwa kufanya hivyo tukishukuru katika kidogo tunachopata Mungu atatujalia makubwa.
Nimpongeze Manyerere Jackton, ambaye alipata tuzo mbili, ikiwamo ya Utawala Bora na Gesi na Madini. Pia Manyerere amefika fainali. Kura zimepungua kidogo, lakini pia nimpongeze Salome Kitomari wa Nipashe aliyeibuka msindi wa Jumla kwa mwaka 2018. Ushindi huu tulioupata unazidi kutupa nguvu za kufanya kazi za uchunguzi.
Tunawashukuru MCT, wadau na Watanzania kwa ujumla, kwamba tumefarijika mno na tuzo hizi ambazo zinatutia moyo kuendelea kufanya kazi hii ya utume, lakini pia zinatuimarisha kama Kampuni ya Jamhuri Media Limited, wachapishaji wa Gazeti la Uchunguzi, JAMHURI.
Sitanii, wakati nikiwa na furaha hiyo nitaonekana wa ajabu mno nisipogusia tukio la aina yake la kuvuliwa ubunge Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Kwa muda sasa nimejizuia kuandika siasa nikiamini kuwa eneo kama hili ninalolikazania la kodi, linaweza kukomboa Watanzania kutoka katika lindi la umaskini kuliko siasa, ila katika hili japo kwa aya chache niligusie.
Nafahamu kuna kanuni, sheria, miongozo, tamaduni na taratibu za Bunge. Nafahamu kuwa Lissu amekuwa nje ya Bunge tangu Septemba 7, 2017 alipopigwa risasa zaidi ya 16 wakati anatoka bungeni. Nikiri, na naamini nchi hii sheria hazijazuia kuwaza, na naomba kuwaza kwa sauti kuwa Spika Job Nduga anapotea njia katika hili.
Wanadamu tumeumbwa kuwa nyuso za aibu. Hata Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete amepata kutwambia kuwa “Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.” Na wala hapa sitayakariri maneno ya Mwalimu Nyerere katika hili juu ya mtu kushauriwa. Sina uhakika kama ameshauriwa au amejishauri kutumia kanuni! Hali ya Lissu ilihitaji utu badala ya sheria.
Sitanii, katika hili Spika Ndugai akisimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu kutoka kwenye sakafu ya moyo wake ni kweli hajui Lissu alipo? Sina kumbukumbu nzuri, lakini pia nadhani katika Bunge hili, Ndugai angekuwa kati ya wabunge wachache wenye ujasiri wa kukejeli ugonjwa kwa kurejea matibabu ya wabunge. Hivi ni kweli kabisa Ndugai hujui alipo Lissu? Inasumbua. Mungu mkubwa.
Nimelazimika kuandika aya hizi iingie katika historia na kumbukumbu za taifa letu. Kwamba uamuzi wa aina hii, kidogo kidogo unamega misingi ya utawala bora. Utawala wa Sheria ni sehemu ya utawala bora. Hata hivyo, ndiyo maana hadi leo haijavumbuliwa teknolojia ya kuendesha mahakama kwa kompyuta kusikiliza mashauri, bado wanatumika mahakimu na majaji.
Jaji au hakimu ni binadamu. Kuna nyakati anaona sheria inaelekeza nini, ila ushahidi wa mazingira na utu, vinamsukuma atoe hukumu inayoacha amani na heshima yake katika jamii. Siwezi kumshauri Ndugai akatubu kanisani, maana sina uhakika kama anaona kuwa amemkosea Mungu na mimi sina mamlaka ya kumhukumu. Naomba kuhitimisha fikra zangu kwa kusema, amani tunayoifurahia leo, imejengwa kwa muda mrefu, tujiepushe na matukio machache yanayoweza kuibomoa miaka si mingi ijayo.
Niwie radhi msomaji wangu, wiki ijayo nitaendelea na mada ya kodi kwa ufasaha, ila wiki hii niliona nina wajibu wa kutoacha wazi zizi bila kuwakumbusha wachungaji, na hatimaye kuangukia kwenye kundi la kuwalaumu miaka michache ijayo. Wakati huo nitaulizwa nilikuwa wapi wakati haya yanatokea, na nilifanya nini? Nitaficha uso wangu. Mungu ibariki Tanzania. Mungu irejeshee nchi yetu moyo wa subira.
Wiki ijayo nitazungumzia kodi ya makampuni (corporation tax). Usilikose JAMHURI.