Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kuainisha mapato yatokanayo na ajira ambayo kisheria unapaswa kuyalipia kodi kama mwajiriwa. Ni wajibu wa mwajiri kukata kodi hiyo ya zuio kwa pato la mwajiriwa pale anapompatia malipo hayo kila mwezi.
Sitanii, jambo moja nilisisitize hapa, biashara nyingi zinapata tabu sana kutokana na kutofanya marejesho ya kodi kila miezi sita na kila baada ya mwaka. Ipo fomu maalumu ya TRA inaitwa ITX215.01.E-P.A.Y.E. Fomu hii inapaswa kujazwa kila miezi sita na kila mwaka kuonyesha wafanyakazi walipata nini? Uliwakata nini kwenye malipo waliyopokea kutoka kwenye kampuni yako? Hii fomu inajazwa kila baada ya miezi sita na kuwasilishwa TRA kila tarehe ya mwisho wa mwezi Juni na Desemba.
Najiuliza, je, ni waajiri wote hapa nchini wanalifahamu suala hili na wanatekeleza kwa mujibu wa sheria? Hapa katika maboresho ya jinsi ya kufanya biashara, kwenye hiyo ‘Blue Print’ limekuja wazo kuwa kama marejesho ya VAT yanavyofanyika online, lakini pia PAYE na SDL zinavyolipwa online, basi ingekuwa vema hata hii statement ikawa online kupunguza gharama za kufanya biashara.
Sitanii, kodi ina mawanda mapana. Kuna masuala mengine mengi ambayo unapoajiri watu unapaswa kuyazingatia kwa mujibu wa sheria, ikiwamo viwango wanavyolipishwa wajiriwa. Kama ni wageni wanakatwa asilimia 15 ya mapato yao yote na kama ni malipo ya wakurugenzi wasio watendaji, nayo yanapaswa kukatwa asilimia 15 ya kiasi anachopokea mkurugenzi husika.
Zipo nyaraka ambazo mwajiri anapaswa kuzitunza kisheria. Kila mwajiri baada ya kufunga mwaka wa fedha na kuwasilisha ripoti iliyokaguliwa TRA, anapaswa kutunza nyaraka kwa muda wa miaka mitano, isipokuwa kama Kamishna wa TRA ameelekeza vinginevyo.
Nyaraka anazopaswa kutunza mwajiri ni pamoja na orodha ya malipo ya ujira na mishahara kwa watumishi, vitabu, nyaraka au kumbukumbu zozote zilizotumika kufanya malipo yanayohusiana na kodi, malipo kwa mwajiriwa au kodi ya zuio aliyoikata mwajiri.
Kushindwa kuhifadhi nyaraka hizi ni kosa kisheria na ukitiwa hatiani unaweza kupigwa faini au kuambulia kifungo ikithibitika kuwa ulikwepa kodi au ulisaidia ukwepaji kodi.
Kodi hizi za mapato, hasa PAYE zimerahisishwa. Kwa waajiri anapaswa kuingia kwenye mtandao wa TRA (www.tra.go.tz) na kuingiza kiwango cha malipo anayotoa kwa mfanyakazi kwa mwezi baada ya kukata mafao ya uzeeni, kisha mfumo utamjulisha kiasi anachopaswa kulipa.
Zipo taratibu nyingine za malipo, kwa mfano malipo ya mkupuo, mafao ya kuacha au kuachishwa kazi na mengine ambayo unapaswa kuwasiliana na mwanasheria wa masuala ya kodi kuhakikisha unaelekezwa kodi sahihi kwa kampuni au taasisi yako. Bila kufanya hivyo, unaandaa mazingira magumu ya biashara yako.
Sitanii, leo wakati nahitimisha makala hii nigusie Kodi ya Kuendeleza Ujuzi (SDL). Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi na Sheria ya Mafunzo ya Ufundi, kila mwajiri anayeajiri watu kuanzia wanne kwenda juu, anapaswa kulipa kodi ya SDL.
Kodi hii inakuwa ni asilimia 4.5 ya malipo yote anayofanya kwa wafanyakazi kila mwezi. Hii inajumuisha mshahara, marupurupu, ujira, kamisheni na malipo mengine yote yanayotozwa kodi.
Kila mwezi mwajiri anapaswa kupeleka orodha ya wafanyakazi TRA na kila miezi sita anapaswa kupeleka hati maalumu ya kuonyesha kiasi cha SDL ilicholipa kampuni yake kwa kuwakata wafanyakazi.
Kimsingi kampuni nyingi zinapata tatizo la kodi kutokana na kutokuwa na ujuzi. TRA kwa sasa imeanzisha Kitengo cha Ushauri wa Kodi. Ni vema kampuni au watu binafsi wanaoajiri na kulipa mishahara wakajenga utamaduni wa kutembelea ofisi za TRA kupata maelezo ya kina juu ya aina ya kodi zinazolipwa na kiasi chake.
Mfanyabiashara asipofanya hivyo, wapo wengi wanaojikuta wametumbukia katika mtego wa kutolipa kodi si kwa kukataa, bali kwa kutofahamu kuwa zinastahili kulipwa, na kwa kufanya hivyo, wanajiingiza katika mazingira ya kupigwa faini zinazokwaza biashara. Kuna usemi wasiopaswa kuusahau wafanyabiashara kuwa “kutojua sheria siyo kinga.” Tukutane wiki ijayo.