Nikiri nimeendelea kupata simu na maswali mengi kuhusu ‘Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania.’ Nimepata simu kutoka Rukwa, Katavi na maeneo ya mbali. Changamoto kubwa ninayoipata ni wahusika kukutana na makala hii katikati bila kusoma za mwanzo.

Sitanii, ananipigia mtu anaulizia mambo niliyoyazungumzia katika sehemu ya kwanza, ya pili au ya saba. Inaniwia vigumu pia kuanza kumwelezea mtu mmoja mmoja hatua unazopaswa kupitia hadi unasajili kampuni au unaanzisha biashara. Kwa mantiki hiyo, naomba uvumilivu.

Niliahidi kuwa ifikapo mwezi Julai nitakuwa na jibu la mwezi upi hasa nitachapisha kitabu hiki. Naomba nirudie kuwa Mungu akipenda nitachapisha kitabu cha ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania’ si muda mrefu. Nitakitangaza kitabu hiki kwa ufasaha na mwisho wa siku kitawafikia wote wenye nia ya kufanya biashara nchini.

Nikiwa hapa jijini Geneva, nimeshuhudia mifumo mikubwa na ya aina yake kibiashara. Wakati sisi hapo nyumbani tunahangaika na madereva teksi ‘wanaoibia’ wageni kwa kuwatoza fedha zisizolingana na umbali kutoka uwanja wa ndege kwenda Mnazi Mmoja au Mbezi, hapa mambo ni tofauti.

Ukifika airport unakuta mashine kama ATM, unabonyeza inakupatia tiketi inayokuruhusu kupanda usafiri wowote wa umma; yaani treni na mabasi kwa muda usiozidi dakika 80. Hakika kwa muda huo ni lazima uwe umefika unakokwenda ndani ya Geneva, maana sehemu nyingi unasafiri kwa dakika 5 hadi 10 kwa mabasi ya kasi na treni za umeme.

Sitanii, niruhusu niachane na hadithi za hapa Geneva nikurejeshe hapo nyumbani. Wiki iliyopita nimehitimisha makala yangu kwa kuhoji: “Je, unafahamu ikiwa biashara yako ina mzunguko wa zaidi ya Sh milioni 20 utaratibu wa kulipa kodi ukoje? Usikose toleo lijalo la JAMHURI, utaratibu utaelezwa kwa usafaha. Tukutane Jumanne ijayo.”

Leo ni Jumanne. Naeleza wenye biashara zenye mzunguko wa zaidi ya Sh milioni 20 wanalipaje kodi. Kundi hili linapaswa kuandaa hesabu zilizokaguliwa. Kundi hili linatozwa kodi kulingana na faida wanayopata. Viwango vya kodi ni kama ifuatavyo:-

Tanzania Bara  

Badala ya mzunguko wa fedha, kundi hili sasa linaangaliwa mapato kwa mwaka. Hii ina maana mapato haya yanapatikana baada ya kufikia mzunguko wa fedha wa kuanzia Sh milioni 20 na kwenda juu kwa mwaka. Kwa mtu anayepata Sh 2,040,000, halipi chochote.

Ikiwa mapato yako yanazidi Sh 2,040,000, lakini hayazidi Sh 4,320,000 basi unatozwa asilimia 9 ya kiwango kinachozidi Sh 2,040,000. Ikiwa mapato kwa mwaka yanazidi Sh 4,320,000, lakini hayazidi Sh 6,480,000, basi unatozwa Sh 205,200 na asilimia 20 ya mapato yanayozidi Sh 4,320,000.

Ikiwa mapato yanazidi Sh 6,480,000, lakini hayazidi Sh 8,640,000, basi anatozwa Sh 637,200 na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi Sh 6,480,000. Ikiwa mapato yanazidi Sh 8,640,00, basi mfanyabiashara anatozwa Sh 1,177,200 na asilimia 30 ya mapato yanayozidi Sh 8,640,000.

Zanzibar

Mapato yakifikia Sh 1,800,000 kwa mwaka mfanyabiashara halipi kitu chochote. Mapato yakiwa Sh 1,800,000, lakini hayazidi Sh 4,320,000, basi atalipa asilimia 13 ya kiasi kinachozidi Sh 1,800,000. Mapato yakiwa zaidi ya Sh 4,320,000 na si zaidi ya Sh 6,480,000, basi mfanyabiashara anatozwa Sh 327,600 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 4,320,000.

Ikiwa mapato yanazidi Sh 6,480,000, lakini hayazidi Sh 8,640,000, basi kodi yake ni Sh 759,600 na asilimia 25 ya kiwango kinachozidi Sh 6,480,000. Ikiwa mapato yanazidi Sh 8,640,000, basi mfanyabiashara aliyeko Zanzibar atalipia Sh 1,299,600 na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh 8,640,000.

Sitanii, kwa pande zote za muungano, kila mfanyabiashara anapaswa kujaza fomu Na. ITX200.01.E ya kukadiriwa mapato ndani ya miezi mitatu ya mwanzo wa kila mwaka na kuiwasilisha kwa Kamishna wa TRA kwa ajili ya kukadiriwa kodi anayopaswa kulipa.

Kodi unayokadiriwa unapaswa kuilipa katika vipindi vinne kwa mwaka na inapaswa kulipwa kabla au ifikapo Machi 31, Juni 30, Septemba 30 na Desemba 31 ya kila mwaka.

Kwa wale wanaoandaa hesabu, wanapaswa kujaza fomu Na. ITX201.01.E na kuwasilisha hesabu zao TRA ndani ya miezi 6 kabla ya Juni 30, kila mwaka unapoanza.

Je, unafahamu kumbukumbu unazopaswa kuzitunza na aina ya kodi nyingine zinazolipwa katika biashara? Usikose nakala yako ya JAMHURI wiki ijayo.