Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kuhoji iwapo unazifahamu nyaraka tatu muhimu unazopaswa kuwa nazo baada ya kusajili kampuni. Nyaraka hizi nimepata kuzigusia katika makala zilizotangulia na hata nilipozungumzia Jina la Biashara nilizigusia.

Kabla sijaingia kwa kina kuzungumzia nyaraka hizi, naomba kuwashukuru wasomaji wangu wengi mnaonipigia simu kutoka Muheza, Bukoba, Mbeya, Kigoma, Mwanza, Zanzibar, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma na mikoa mingine mkinitaka kuendelea na mada hii.

Nimeguswa na msomaji kutoka Zanzibar, aliyesema ikiwezekana kuleta ufanisi katika biashara nianzishe mada ya jinsi ya kuondosha mzigo bandarini kwani bandari ndiyo inayowafilisi Wazanzibari. Anasema yapo makontena 1,700 yaliyopelekwa Mombasa kutokana na msongamano kwenye Bandari ya Zanzibar, hivyo hata kama mtu atakuwa na kampuni nzuri na nyaraka zote za kufanya biashara, kwa Zanzibar ni vigumu.

“Labda hapo kwenu Dar es Salaam tunakoambiwa mzigo unatolewa kwa saa 24. Ina maana naweza kulala kidogo, ikifika saa 8 usiku nakwenda bandarini kutoa mzigo wangu, kwa Zanzibar si hivyo. Tende zimekwama bandarini, kreni za kubeba kontena iko moja, naamini mnaweza kutusaidia ikiwa uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam utaamua kutuazima japo mashine mbili kuokoa jahazi Zanzibar,” amesema kwa uchungu huyu msomaji wangu.

Sitanii, nimesema tangu mwanzo na hapa nasisitiza, kuwa mwisho wa siku makala hizi nitaziweka pamoja na kuandika kitabu cha “Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania” ndani ya mwaka huu. Kitabu hiki natarajia kitatoa majibu ya maswali mengi ninayoulizwa na mtu mmoja mmoja na yatawasaidia wajasiriamali kuanzisha biashara endelevu.

Juzi nilikuwa katika Kipindi cha Malumbano ya Hoja pale ITV. Mada ililenga kuangalia ushiriki wa vijana katika uchumi wa viwanda. Karibu vijana wote waliochangia mada ile maelezo yao ilikuwa ni “Serikali itusaidie.” Kwa kweli sikuwaficha. Nimewaambia bayana vijana kuwa nchi hii haiwezi kuendelea kwa kila mtu kuililia serikali imsaidie.

Nimewaeleza kuwa uwekezaji hauhitaji mtaji wakati unaanza kama wengi walivyojenga dhana potofu, bali unahitaji uaminifu, kufahamu taratibu na sheria za biashara unayotaka kuifanya. Ni kutokana na watu wengi kutofahamu misingi ya kusajili, kuanzisha na kuendesha biashara nimelazimika kuandika makala hii mfululizo ambapo mwisho wa siku nitachapisha kitabu.

Sitanii, nikirejea katika swali la msingi nililoliacha linaelea hewani wiki iliyopita, zipo nyaraka za msingi tatu ambazo kila kampuni inapaswa kuwa nazo baada ya kupata usajili. Nyaraka ya kwanza ni cheti cha Namba ya Utambuzi wa Mlipakodi (TIN). Namba hii inakufungulia mlango kama kampuni kutambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uko wapi, unafanya nini, unapata nini na unalipa nini.

Ni namba ya TIN itakayotumika kulipia kodi zako zote na wakati unawasilisha hesabu zilizokaguliwa unapaswa kuwa unarejea kodi ulizolipa serikalini kupitia namba hii. Kama ni maisha ya uraiani, namba hii ya TIN kwenye biashara ni sawa na Kitambulisho cha Taifa. Kupata TIN nilikwishaeleza taratibu zake, ila nigusie tu nyaraka unazopaswa kuwa nazo na kuziwasilisha TRA.

Kama kampuni unapaswa kuwasilisha nyaraka sita:- (1) nakala iliyothibitishwa ya Katiba ya Kampuni. (2) nakala iliyiothibitishwa ya cheti cha usajili. (3) nakala zilizothibitishwa za hati za TIN za wakurugenzi wa kampuni hiyo mpya. (4) Nakala iliyothibitishwa  ya Malipo ya Kodi ya Awali (provisional tax). (5) Nakala iliyothibitishwa ya mkataba wa pango wenye kuonyesha umelipia ushuru wa stempu na kodi ya zuio. (6) Nakala zilizothibitishwa za hati za kusafiria au Kitambulisho cha Taifa na picha za ‘passport size.’ Ukiwasilisha nyaraka hizo TRA kampuni inapata usajili wa TIN ndani ya siku zisizozidi 3. TIN inatolewa bure.

Sitanii, baada ya kupata TIN, na ukumbuke ukiishalipa hiyo kodi ya ‘provisional’ unayokuwa umekadiriwa kulingana na maelezo yako, unapaswa kupata Hati ya Mlipakodi (Tax Clearance). Hapo unakwenda kutafuta nyaraka ya pili, ambayo ni muhimu kwa kila kampuni; leseni ya biashara.

Kulingana na aina ya biashara (rejea makala zilizotangulia), unakwenda kuomba leseni yako ama wizarani au kwenye halmashauri ya mji, wilaya, manispaa au jiji na unapaswa kuwasilisha nyaraka 6 zifuatazo:-

(1) Nakala iliyothibitishwa ya Katiba ya Kampuni. (2) Nakala iliyothibitishwa ya cheti cha usajili. (3) Nakala iliyothibitishwa ya TIN ya kampuni hiyo mpya. (4) Nakala iliyothibitishwa ya hati ya mlipakodi kutoka TRA. (5) Nakala iliyothibitishwa ya mkataba wa pango wenye kuonyesha umelipia ushuru wa stempu na kodi ya zuio kwa ajili ya ofisi. (6) Nakala iliyothibitishwa ya hati ya kusafiria au Kitambulisho cha Taifa cha Mkurugenzi/Wakurugenzi. Ukiwa na nyaraka zote hizo unapata leseni katika muda usiozidi siku 3 za kazi. Hapa unalipia gharama za leseni.

Baada ya kupata nyaraka ya pili ambayo ni leseni, sasa uanapaswa kutafuta nyaraka ya tatu ambayo ni Hati ya Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Hapa unapaswa kuwasilisha TRA nyaraka nane:- (1) Nakala iliyothibitishwa ya Katiba ya Kampuni. (2) Nakala iliyothibitishwa ya cheti cha usajili. (3) Nakala iliyothibitishwa ya TIN ya kampuni hiyo mpya. (4) Nakala iliyothibitishwa ya hati ya mlipakodi kutoka TRA.

Nyaraka nyingine ni:- (5) Nakala iliyothibitishwa  ya mkataba wa pango wenye kuonyesha umelipia ushuru wa stempu na kodi ya zuio kwa ajili ya ofisi. (6) Nakala iliyothibitishwa ya hati ya kusafiria au Kitambulisho cha Taifa cha Mkurugenzi/Wakurugenzi. (7) Nakala iiyothibitishwa ya leseni ya biashara. (8) Ununuzi wa mashine ya EFD kwa ajili ya kulipa VAT. Ukiwa na nyaraka zote hizo unapata usajili wa VAT katika muda usiozidi siku 3 za kazi. Hapa hulipii gharama yoyote.

Ukiishapata usajili wa TIN, leseni na VAT basi unapaswa kuangalia biashara unayofanya iwapo inahitaji leseni nyingine. Kwa mfano kama unaanzisha gazeti, unapaswa kupata leseni ya uendeshaji kutoka kwa Msajili wa Magazeti na kupata namba ya chapisho (ISSN) kutoka Maktaba Kuu ya Taifa. Hii inategemea biashara unayofanya, hivyo ni kujiridhisha kupitia kwa mwanasheria kabla ya kuamini kuwa umemaliza usajili.

Sitanii, wiki ijayo nitaendelea na mada hii kwa kuanza kuangalia aina ya kodi unazopaswa kulipa katika uendeshaji wa biashara. Usikose nakala yako ya Gazeti la JAMHURI kufahamu mfumo mzima wa Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania.