Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kusema kuwa leo nitaelezea masharti na aina ya viambatanisho unavyopaswa kuweka katika kuwasilisha fomu ya maombi ya leseni. Naomba kuwashukuru wasomaji wangu kwa kunipigia simu nyingi kadiri inavyowezekana na kwa kuonyesha kuwa mnatamani kupata kitabu hiki haraka kadiri inavyowezekana.
Sitanii, kitabu hiki nitakichapisha na kukiingiza mitaani hivi karibuni, ila nawaomba uvumilivu. Wapo mliotaka niwatumie nakala tete (soft copy) ya kitabu hiki, hakika naomba nisifanye hivyo. Suala la nakala tete litakuwa limenipotezea haki miliki (patent rights). Nafanya utafiti katika kuandika masuala haya na nimewekeza hadi darasani kwa ngazi ya Uzamili kusomea biashara, hivyo kutoa nakala tete ni njia rahisi ya kutorejesha gharama nilizowekeza.
Baada ya usuli huo, sasa nirejee kwenye hoja yenyewe. Ikiwa biashara yako imesajiliwa kama kampuni, unapaswa kuweka nakala ya cheti cha usajili na kama ni jina la biashara, unapaswa kuambatanisha tamko kama nyongeza ya nakala ya cheti cha usajili.
Kama ni kampuni pia unapaswa kuweka nakala ya Katiba ya Kampuni (Memorandum of Understanding and Articles of Association) ikionyesha kuwa kampuni husika imeruhusiwa kufanya biashara inayoombewa leseni.
Sitanii, kiambatanisho kingine ni uthibitisho wa uraia. Unapaswa kuthibitisha iwapo wewe ni raia wa Tanzania kwa kuweka nakala ya hati ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa au kitambulisho cha taifa. Na kama hivyo vyote hauna, basi unapaswa kwenda mahakamani kuapa na kupata hati ya kiapo kuthibitisha uraia wako (affidavit).
Ikiwa mwombaji ni raia wa kigeni, anapaswa kuwasilisha nakala ya kuishi nchini Daraja la A inayomruhusu kuwekeza katika biashara hiyo. Endapo wenye hisa kwenye kampuni wote wapo nje ya nchi, itabidi iwasilishwe hati ya kiwakili (power of attorney) kuthibitisha kuwa aliyewasilisha maombi ni mwakilishi halali wa kampuni hiyo.
Mwombaji pia anapaswa kuwasilisha ushahidi kuwa anako mahala pa kufanyia biashara. Hapa anaweza kuwasilisha nakala ya hati, mkataba wa pango au nakala ya risiti ya kununua jengo husika analotarajia kufanyia biashara. Kwa mtu binafsi anajaza fomu na kuambatanisha hayo yote isipokuwa Katiba au andiko.
Awali katika kitabu hiki, niliandika utaratibu wa kupata namba ya mlipa kodi (TIN). Katika hatua hii ya kuomba leseni, mfanyabiashara anapaswa kuwasilisha nakala ya hati ya namba ya mlipa kodi ikionyesha kuwa mhusika amesajiliwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama mlipa kodi.
Sitanii, mapema katika andiko hili nilisema baadhi ya biashara zinahitaji kuwa na leseni zaidi ya moja. Kwa mantiki hiyo wakati unawasilisha maombi ya leseni, unatakiwa kuwa na nakala ya leseni ya biashara hiyo maalumu.
Kwa mfano, kama unahitaji kufanya biashara ya kuingiza na kuondoa mizigo bandarini (clearing and forwarding), unapaswa kuwa na Leseni ya Wakala wa Forodha. Kwa biashara ya utalii, unapaswa kuwa tayari unayo leseni ya uwakala wa utalii (TALA).
Kwa biashara zote za kitaaluma, mfano kuendesha biashara ya hospitali, zahanati, udaktari, sheria, ujenzi, uhandisi, urubani wa ndege, unahodha wa meli na nyingine za aina hii, unapaswa kuwa na hati ya utaalamu (professional certificate). Kwa vyombo vya usafiri kama ndege, meli na treni unapaswa kuwa na hati ya ubora kutoka kwenye mamlaka zinazohusika.
Sitanii, nimeulizwa mara nyingi juu ya viwango vya ada. Jibu la swali hili ni inategemea biashara unayoifanya na mahala unapoifanyia. Ila kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2014, kama ilivyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 28, Vol. 95 la Julai 11, 2014 viwango vya leseni vinaanzia Sh 5,000 hadi Sh 300,000 kulingana na biashara ipo jijini au kijijini. Pia kwa wageni viwango vinapanda hadi dola 20,000 kulingana na aina ya biashara.
Kimsingi, kwa watu wanaofanya biashara viwango hivi si vikubwa na si viwango vya kumfanya mtu akwepe kulipia leseni, kwani vinalipika ikiwa kweli mhusika anafanya biashara. Wiki ijayo nitahitimisha masharti ya kusajili jina la biashara na baada ya hapo niingie katika utaratibu wa kusajili kampuni.
Eneo la kodi zinazolipwa, naomba kama nilivyoomba awali iwe mada itakayokuja baada ya hizi mbili za usajili wa jina la biashara na kampuni. Tukutane wiki ijayo katika safu hii.