Wiki iliyopita nilieleza kuwa leo nitaeleza wakati wa kuwasilisha maombi ya leseni chini ya kifungu cha 14 unapaswa kuipitisha hatua zipi. Katika sehemu hii ya 10, naomba kufafanua hili. Fomu yako ya kuomba leseni ni lazima ianzie ngazi ya chini kabisa.

Sitanii, ngazi hizi ndizo za kufanya uamuzi wa awali wenye madhara makubwa mbele ya safari. Unaanzia ngazi ya kijiji au mtaa kulingana na kwamba biashara yako iko mjini au kijijini. Katika ngazi hii watatoa maoni ya kwanza iwapo upewe au usipewe leseni. Watatoa maelezo, tarehe ya kufanya uamuzi na kutia saini za wahusika katika kikao hiki. Pia wataweka na muhuri.

Kwa kutegemea aina ya biashara, kama ni hoteli, kuuza vileo au vyakula, unaweza kutakiwa kupitisha maombi yako kwa Afisa Afya (kwa maombi mapya).

Bila kujali aina ya biashara, hatua ya tatu inapaswa kupitiwa na yeyote anayeomba leseni. Maombi yanapaswa kupitishwa kwa Afisa Biashara wa Wilaya. Fomu yako ya kuomba leseni ikitoka kwa Afisa Biashara, inakwenda kwa Afisa Mipango ama wa Mji Mdogo/Mji/Halmashauri/Manispaa/Jiji kwa uamuzi sawa na ule wa hatua ya kwanza.

Baada ya hatua hii, fomu ya maombi inapelekwa kwenye halmashauri ya Mji/Wilaya/Manispaa/Jiji au Wizara kwa uamuzi wa mwisho kulingana na aina ya leseni, iwapo leseni unayoomba inaangukia kundi A au B.

Baada ya hatua hizo kukamilika, ofisi sasa inakuelekeza ukalipe ada ya leseni kulingana na kundi la biashara yako inakoangukia. Utapewa gharama na ‘control number’ utakayoitumia kufanya malipo kisha utapewa stakabadhi, ambayo namba yake inaandikwa kwenye fomu hiyo. Ofisi itaandika namba ya leseni kwenye fomu hii, tarehe ya kutolewa na itagongwa muhuri. Hapo utaambiwa siku ya kufika kuchukua leseni yako.

Sitanii, niliahidi pia kueleza aina za biashara na leseni zipi biashara husika zinaangukia. Iwapo biashara yako inaangukia katika kundi A, basi maombi haya baada ya kutoka kwenye hatua ya Afisa Mipango utayapeleka Wizara ya Viwanda na Biashara. Ada zote za leseni za Kundi A zinalipwa kwa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Biashara zinazoangukia katika kundi A ni:- 1. Umiliki/Ujenzi wa majengo/Wakala wa mali. 2. Wakala wa meli. 3. Uendeshaji wa shughuli za meli. 4. Usafirishaji wa kibiashara. 5. Wakala wa kupokea na usafirishaji wa mizigo. 6. Bima. 7. Biashara za utalii (ikiwamo hoteli za kitalii, usafirishaji watalii, picha za kitalii na mengine mengi yanayohusiana na utalii).

Biashara nyingine katika kundi hili ni:- 8. Biashara ya fedha. 9. Usafirishaji wa abiria na mizigo kwa ndege. 10. Huduma ya posta. 11. Usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya reli. 12. Huduma za mawasiliano. 13. Uthamini wa mizigo. 14. Uhesabu na upangaji wa mizigo melini. 15. Bandari. 16. Utengenezaji na usambazaji umeme. 17. Maduka ya kubadilisha fedha. 18. Kupakia na kupakua mizigo melini. 19. Wakala wa kusafirisha vifurushi na kusafirisha barua. 20.  Vituo vya radio na televisheni.

Sitanii, nyingine ni:- 21. Huduma za Bandari na Meli. 22. Usafirishaji wa mafuta mazito. 23. Klabu za usiku. 24. Uuzaji na usambazaji silaha na risasi. 25. Uuzaji na usambazaji baruti. 26. Hifadhi ya jamii. 27. Uuzaji bidhaa nje. 28. Uchimbaji na usambazaji maji. 29. Uuzaji wa vifaa vya utangazaji. 30. Utengenezaji na uuzaji wa bidhaa. 31. Ununuzi na uuzaji wa magari. 32. Wakala wa ushuru. 33. Uagizaji wa bidhaa nje ya nchi. 34. Sonara na biashara ya uuzaji wa madini. 35. Biashara yoyote ambayo haikutajwa yenye sura ya kitaifa au kimataifa inayoongozwa na sera.

Sitanii, lipo pia kundi B, ambalo wanaangukia wafanyabiashara wengi hapa nchini, ambao wengi ni wachuuzi. Biashara hizi zinazoishia kwenye halmashauri za miji, wilaya, manispaa na majiji ni:- 1. Wakala wa bima. 2. Migahawa, hoteli za kawaida, nyumba za kulala wageni. 3. Mnada. 4. Kutembeza bidhaa. 5. Bidhaa mchanganyiko (supermarket). 6. Kampuni za biashara za mikoa. 7. Vyama vya ushirika. 8. Uuzaji wa bidhaa za jumla na ujenzi wa kandarasi.

Nyingine ni:- 9. Utaalamu au ushauri wa kitaalamu. 10. Uchapishaji wa vitabu na magazeti. 11. Vipuri. 12. Udalali. 13. Usafirishaji wa abiria mijini. 14. Viwanda vidogo. 15. Simu za kwenye vibanda na biashara yoyote ambayo haikutajwa, na ambayo haina sura ya kitaifa au kimataifa na haiongozwi kisera.

Nafasi gazetini imekuwa finyu. Wiki ijayo nitakuletea masharti na viambatanisho vinavyotakiwa katika fomu hii unapoijaza kabla ya kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kuzingatia katika hatua nilizozieleza wiki iliyopita.

Nikuondoe hofu msomaji wangu, katika kitabu nitakachokichapisha cha ‘Jinsi ya Kufanya Biashara Tanzania’, mada hizi zitakuwa katika mtiririko wa pamoja, hivyo hakutakuwapo haja ya kujikuta unalazimika kuruka au mada kukatwa nusunusu, bali utaipata yote kwa usahihi na kuisoma kwa mtiririko unaofanana. Tukutane wiki ijayo.