Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC) ikiongozwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila leo Machi 24, 2024 imepokea na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Ilala (DCC) ya kuligawa jimbo la Ukonga lililopo Wilaya ya Ilala kuwa majimbo mawili ambayo ni jimbo la Ukonga na Jimbo Kivule ambapo mchakato unaofuata ni kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye mamlaka husika ikiwemo OR-TAMISEMI ili kupata ridhaa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa RCC mara baada ya kupokea mapendekezo hayo, RC Chalamila amesema mapendekezo hayo yamelenga kuboresha huduma kwa kuzingatia jimbo hilo ni kubwa na lina idadi kubwa ya watu hivyo kamati imepokea mapendekezo hayo na yatawasilishwa ngazi zingine kwa maamuzi zaidi

Aidha RC Chalamila amesema baada ya kugawanywa jimbo jipya la Kivule litakua na kata sita ambazo ni Kipunguni, Mzinga, Msongola, Kitunda, Kivule na Majohe, jimbo hilo lina kilometa za mraba 128, idadi ya watu 431,736 na Jimbo la ukonga likibaki na Kata saba ambazo ni Ukonga, Chanika, Gongo la Mboto, Zingiziwa, Buyuni na Pugu Station likiwa na idadi ya watu 490,121.

Awali akiwasilisha taarifa ya mapendelezo ya ugawaji wa jimbo la Ukonga kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bwana Saloni Asheri Nyika ambae ni Katibu Tawala Msaidizi Usimamizi,Ufuatiliaji na Ukaguzi Mkoa huo amesema baada ya mapendekezo hayo ofisi ya katibu Tawala Mkoa ilituma wataalamu ambao walikwenda kujiridhisha na kubaini ni kweli jimbo hilo linahitaji kugawanywa na vigezo vyote vilizingatiwa ikiwemo Idadi ya watu pamoja na shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Dar es Salaam Juma Simba Gadafi amesema kwenye kutazama maslahi ya wananchi ni muhimu kuacha ubinafsi kwani kugawanya majimbo ni kuboresha huduma kwa wananchi.