Jumla ya watu watano wametajwa kuwania Jimbo la Kiteto lililopo mkoani Manyara, kumrithi Mbunge Benedict ole Nangoro (CCM), anayemaliza muda wake mwaka huu.
Waliotajwa kutaka kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Emmanuel Papian, Amina Saidi Mrisho (CCM), anayefanya kazi Tume ya Takwimu Taifa, Jonathan Kilani, mwanachama kutoka Chadema, na Goodluck Mmari (CCM) na Mashaka Said Fundi (SAU).
Hata hivyo, wakati wananchi hao wakijitokeza kuwania jimbo hilo, taarifa za uhakika kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Ole Nangoro (pichani) zinaeleza kuwa anakusudia kutetea nafasi yake hiyo mara muda ukifika.
“Tunahitaji wengi wajitokeze ili tuweze kuwachuja na kumpata kiongozi bora atakayekomboa Jimbo la Kiteto ambalo kwa sasa lina changamoto nyingi zikiwamo za migogoro ya ardhi,” anasema mmoja wa wananchi wilayani humo.
Kwa miaka saba mfululizo, wananchi wa Kiteto wamekuwa kwenye kipindi kigumu cha maisha kutokana na kutumia muda mwingi kwenye migogoro ya ardhi kuliko kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Migogoro hiyo imeleta madhara makubwa ndani na nje ya nchi baada ya kujitokeza vitendo vya kikatili na vya aina yake vya watu kuuana kwa kutumia silaha za jadi na hata bunduki wakigombea ardhi.
Akizungumza hayo, Ibrahimu Msindo, mwananchi wa kawaida, anasema miaka saba iliyopita imekuwa shubiri na historia kwa wana-Kiteto ambako kila mtu ana cha kuhadithia baada ya wengi wao kufanyiwa ukatili.
“Kuna waliouawa shambani, wengine machungajini na wengine kufungwa jela kwa madai ya kuvamia maeneo na wengine, kuteketezewa mali zao kutokana na ghasia zilizoibuka wilayani humo,” anasema Msindo.
“Tunataka kiongozi atakayejibu matatizo haya kati ya hao, kwani mwenye mamlaka ya kumweka kiongozi madarakani ama kutomweka ni mwananchi mwenyewe na siyo vinginevyo,” anasema.
Kipindi hiki ni mwafaka na adhimu kwa wana-Kiteto kufanya uamuzi mgumu wa nani anaweza kuwa mkombozi wa kulinda maisha yao ambayo yako mashakani kila kukicha.
Wakati ukatili huo ukiendelea, viongozi wa wilaya wamekuwa wakiendelea kukabiliana na vitendo hivyo na kwamba pamoja na jitihada hizo bado ziliendelea kugonga mwamba, hali iliyolazimu uongozi wa ngazi za juu kuja kuingilia kati.
Kwa mwezi mmoja na nusu sasa hali ya Kiteto imeanza kurejea na hii imedaiwa ni kutokana na wakulima wengi mashamba yao kuteketezwa na mifugo na kukata tamaa kurejea nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa za wilaya, migogoro Kiteto huanza kipindi cha kilimo kinapoanza mwanzo wa mvua mwezi wa kumi na mbili na wakati wa mavuno kuanzia mwezi wa sita.
Hata hivyo, katika hatua hiyo wananchi wamewataka waliojitokeza kuwania jimbo hilo kujipima juu ya yaliyojitokeza kwa wananchi kuuana, wengine kufilisika na hata kupata vilema vya maisha kama wanatosha katika nafasi hiyo.
Tangu kuzinduliwa Jimbo la Kiteto mwaka 1974, Wilaya ya Kiteto imeongozwa na wabunge watano akiwamo Abdalah Kimosa, Erasto Losioki, Jumanne Surumbu ambaye aliongoza kwa miezi mitatu, Benedict Kiroiya Loosurutya na Benedict ole Nangoro aliyepo madarakani sasa.