Uongozi wa Jiji la Dar es Salaam umeiomba Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwapa kibali cha kuongeza mabasi ya usafiri wa haraka (mwendokasi) katika Jiji la Dar es Salaam.
Lengo la kuomba kibali hicho ni kutaka kushirikiana na mkandarasi aliyepewa dhamana ya kuendesha mradi huo ili kuboresha huduma ya usafiri ya mradi huo kwa wakazi wanaoutegemea kufika mjini.
Usafiri huo ambao kwa sasa unaendeshwa na Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART) kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali anayeusimamia (DART), unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa magari, hali inayosababisha wananchi kujazana kwenye mabasi machache yaliyopo huku wengine wakikaa vituoni kwa muda mrefu wakisubiri mabasi.
Kwa sasa mradi una mabasi 140 tu yanayofanya kazi huku idadi ya wasafiri wanaotegemea kutumia huduma ya usafiri huo kwa siku wakifikia 220,000.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam unataka kushirikiana na mkandarasi anayeusimamia kwa kuagiza magari ya nyongeza ili kumaliza changamoto ya abiria kujazana kwenye magari hayo nyakati za asubuhi na jioni.
Akizungumzia nia hiyo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, amesema hawafurahishwi na taabu wanazopata wananchi wanaotumia usafiri huo, hivyo ameiomba TAMISEMI kukubali ombi la jiji kuongeza mabasi 100 katika mradi huo.
“Sisi tumeomba serikali kuu ituruhusu tuweze kuongeza magari ili kusaidiana na mwekezaji aliyepo kwenye huu mradi, wala hatutaki kujimilikisha mradi huo,” amesema Mwita.
Amesema ombi lao la kutaka kushirikiana na mwekezaji aliyepewa mradi huo limeambatana na masharti matatu ambayo serikali kuu ikiyaridhia yatawawezesha kuendesha mradi huo kwa ufanisi.
Amesema sharti la kwanza katika ombi hilo, wameomba serikali ikubali magari yatakayonunuliwa na jiji yawe yanapatiwa ruzuku ya mafuta kutoka serikalini.
Sharti la pili amesema kuwa wameiomba serikali kuyaondolea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) mabasi hayo ya nyongeza wakati wa kuyaingiza kutoka nje ya nchi.
Na sharti la mwisho katika ombi lao amesema kuwa wameiomba serikali kumtaka mwekezaji aliyepewa mradi kukubali kushirikiana na jiji kuuendesha.
“Tutatumia fedha ya jiji kuagiza mabasi 100. Jiji lina fedha za kununua mabasi zaidi ya 100 ambayo yanaweza kusaidia kupunguza adha iliyopo kwa sasa, tunachosubiri ni kupata kibali ili tuanze utekelezaji.
“Fedha inayowekwa Benki Kuu na jiji si yetu bali ni ya wananchi, kwa hiyo, sisi tunaomba kuongeza magari ili kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa jiji letu,” amesema Mwita.
Kutokana na suala hilo kuwa kwenye hatua za awali amesema hawajafikia mchakato wa kuandaa taratibu za kuendesha mradi huo.
Amesema mchakato huo wa namna ya kuundesha utaanza mara moja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sulemani Jafo, atakapokubali na kutoa kibali.
“Ikiwa tutapewa kibali na serikali kuu, tutakaa chini na mkandarasi na kupanga utaratibu mzuri wa kufanya kazi katika mradi wa mwendokasi,” amesema Mwita.
Ameongeza kuwa kila kitu kinahitaji usimamizi na mipango mizuri, hivyo watakapopewa mradi watawaita wadau husika ili kujadiliana namna nzuri ya kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ukienda pale kivukoni utaona kuna utaratibu mzuri wa kupita kwenye vizuizi wakati wa kuingia kwenye kivuko, kwa hali hiyo tukikubaliwa kufanya kazi na mwekezaji aliyepo kwenye haya magari ya mwendokasi tutahakikisha huduma ya usafiri huu inaboreshwa kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema Mwita.
Ameongeza kuwa hata kama wasipokubaliwa kushirikiana na mwekezaji katika mradi uliopo kwa sasa, wataomba kusimamia huduma ya mabasi katika mradi wa mabasi yaendayo haraka unaotarajiwa kuanza kujengwa kuelekea Mbagala na Gongo la Mboto.
Amesema lengo la kutaka kuendesha mradi huo ni kutaka kuionyesha serikali kwamba uwezo wa kuendesha mradi wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka wanao, na wanaweza kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi bila kuleta adha kwa wananchi, kinyume cha hali ilivyo kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita Jiji la Dar es Salaam limepokea ugeni wa watu 27 kutoka Kisumu, Kenya uliokuja nchini kujifunza mambo mbalimbali yanayotekelezwa jijini. Pamoja na mambo mengine, wageni hao walifurahishwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Meya Mwita wakati wa ugeni huo alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi wa Dar es Salaam kutokana na adha wanayoipata kuhusu usafiri wa mwendokasi. Vilevile aliongeza kuwa mradi wa mabasi yaendayo haraka ni mradi wa kisasa, hivyo kinachotakiwa ni kuuboresha na kuwa na wasimamizi makini ambao watausimamia ipasavyo.