Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia wanafamilia wa ukurasa wa TUZUNGUMZE na wasomaji wote wa Gazeti la JAMHURI heri ya Noeli na Mwaka Mpya wa 2020.
Napenda kuwatakia miezi 12 ya furaha, wiki 52 za baraka, siku 366 za mafanikio, saa 8,784 za afya, dakika 527,040 za amani na sekunde 31,622,400 za upendo. Heri ya Mwaka Mpya 2020.
Kusamehe ni siri ya mafanikio katika maisha. Kila mmoja wetu ameitwa kuwa mponyaji wa majeraha ya wengine licha ya kwamba yeye mwenyewe anayo majeraha yake. Binadamu wote tunayo majeraha ya kihisia, kiakili, kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia.
Inawezekana una majeraha ya kusalitiwa na mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kufiwa na mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kuishiwa mtaji wa biashara. Inawezekana una majeraha ya kiuchumi. Majeraha ni mengi. Nafasi hainiruhusu kuyataja majeraha yote. Itoshe kusema kwamba, makala hii ina nia ya kuyaponya majeraha yako ya kihisia, kiuchumi, kifamilia, kiafya na kiroho.
Nilipotoa makala yangu iliyokuwa inasema: ‘Nguvu ya msamaha’ katika Gazeti la JAMHURI linalotolewa nchini Tanzania na kuchapishwa na JAMHURI Media, Toleo No. 249, ISSN1821-8156, Julai 5-11, 2016, msomaji mmoja ambaye kwa sababu maalumu sitataja jina lake, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi:
Nimeumizwa sana katika maisha yangu. Tena nimeumizwa mno. Sina furaha kabisa katika maisha yangu. Nina mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka kumi na mitatu (13). Nilipata ujauzito nikiwa chuoni mwaka wa tatu. Kwa sasa nipo naishi na mwanagu. Kila mwisho wa mwezi ninamtumia mama yangu mzazi pesa za matumizi. Baba yangu simtumii kwa sababu hatupatani kabisa. Baba alinibaka na kunipa ujauzito wa huyu mtoto wangu.
Baba alipogundua kwamba nina ujauzito wake alinilazimisha kuitoa mimba. Nilikataa kwa sababu nilihofia kufa. Niliamua kuhama nyumbani na kwenda kuanza maisha ya peke yangu. Namshukuru sana Mungu nilijifungua salama. Mtoto amekua, lakini baba yangu hataki hata kuniona. Hataki hata niende nyumbani. Ndugu na majirani wanashindwa kufahamu chanzo cha ugomvi wangu na baba yangu. Mama yangu humlilia baba yangu anisamehe kama nilimkosea lakini baba hataki.
Siri kubwa niliyoiweka moyoni ni kwamba, baba yangu ndiye aliyenibaka mpaka nikashika mimba ya huyu mtoto. Mpaka leo mimi na baba ndio tunajua jambo hili. Kiukweli ninamchukia sana baba yangu. Aliniumiza sana. Mama, ndugu na jamaa hawamfahamu baba wa mtoto wangu. Baba hataki kumwona mjukuu wake. Mtoto wangu anataka kumfahamu baba yake. Je, niiambie jamii baba alinibaka au nimwambie baba yako ni baba yangu? William nimechanganyikiwa kabisa.
Jibu la msamaha ni msamaha. Kusamehe ni kupita njia aliyoipita Yesu Kristo. Mwana michezo Jonathan Lockwood aliwahi kusema: “Wasamehe wengine si kwa sababu wanastahili, bali kwa sababu wewe unastahili amani.”
Msamaha ni amani. Msamaha ni uponyaji. Msamaha ni manukato kwa walioumizwa kihisia, kiupendo, kiafya na kiimani. Jifunze kusamehe. Jifunze kuwa na amani ndani ya moyo wako. Kusamehe ni kumuachilia mtu uliyemshikilia katika moyo wako.
Kumbuka: Kutokusamehe ni kuendelea kuyakumbatia maumivu ndani ya moyo wako. Achilia uchungu ulionao. Usiuweke moyoni. Mchungaji Joel Osteen anasema: “Tusiposamehe, hatumuumizi mtu mwingine, hatuiumizi kampuni iliyotukosea, hatumuumizi Mungu. Tunajiumiza sisi wenyewe.”
Papa Fransisko anasema: “Asiyesamehe anaugua kimwili, kihisia na kiroho.” Katika makala hii nitauzungumzia msamaha. Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni za kuwania urais alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu mpinzani wake aliitwa Edwin McMasters Stanton. Edwin McMasters Stanton alikuwa tayari kufanya lolote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa Baraza la Mawaziri, alimteua Stanton kuwa Waziri wa Ulinzi. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ili Stanton asiteuliwe kuwa waziri. Hata hivyo, rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za wasaidizi wake.
Rais akasema: “Huyu ananichukia mimi ila si Marekani. Huyu ana sifa za kuiongoza Marekani na watu wake.” Akamteua kuwa waziri wa ulinzi. Stanton aliposikia uteuzi wake alishangaa mshangao mkubwa. Akaukubali ule wadhifa na akaifanya hiyo kazi kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema: “Hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa huku akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.”