JESHI la Bangladesh limechukuwa rasmi udhibiti wa nchi Jumanne, baada ya maandamano makubwa ya umma kumlazimisha mtawala wa muda mrefu wa taifa hilo kujiuzulu na kukimbilia uhamishoni

Rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin tayari amelivunja bunge katika utekelezaji wa hatua ambayo ni moja ya matakwa muhimu ya wanafunzi walioandamana. Taarifa ya kuvunjwa kwa bunge hilo imetolewa na katibu wa habari wa Rais Shiplu Zaman.

Mkuu wa jeshi Jenerali Waker-Uz-Zaman anatazamiwa kukutana na viongozi wa maandamano ya wanafunzi wakati taifa hilo likisubiri kuundwa kwa serikali mpya. Viongozi wa wanafunzi wamempendekeza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus kuongoza serikali ya mpito.

Pendekezo la mratibu muhimu wa maandamano yaliyofanywa na wanafunzi Nahid Islam kuwa Muhammad Yunus aongoze serikali ya mpito limetolewa siku moja baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu.