Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema linachunguza tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya vijana wake kudaiwa kukiuka taratibu za kukamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali ikiwemo kuwapa vipigo na unyanyasaji wa kijinsia.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya unyanyasaji wa raia wa mtaa wa National Housing-Kanyamala Kata ya Makole ambapo watu wanaodhaniwa kuwa ni Polisi walifika na kufyatua risasi kwa lengo la kumchukua mtuhumiwa anayejulikana kwa jina la Kalamba Ramadhani(38 ).
Aidha mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa watu hao walifika kwenye eneo hilo wakiwa na gari yenye usajili wa namba za Serikali huku wakiwa na silaha za moto na kufyatua juu kusha kumkamata Kalamba na kuondoka naye bila kueleza kosa lake.
Hali hiyo iliwashtua wakazi wa mtaa huo na kupelekea kushindwa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kuhofia kuuawa.
Kutokana na tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma ACP Martin Otieno ameeleza tukio hilo kuwa huenda wahusika sio Polisi bali linaweza kufanywa na watu wengine huku akiahaidi kulifuatilia kwa undani suala hilo ili kujua undani wake.
“Nitafuatilia nijue ilikuwa nini na tatizo lilikuwa ni nini kwa sababu inawezekana wakawa kweli ni polisi na walikuwa na sababu za kupiga hizo risasi hewani kama walikutana na pingamizi la aina yoyote kama nikweli walikuwa ni polisi kwa hiyo hili mimi nitalifuatilia ili niweze kujua ilikuwa na huyo mwananchi aliyeenda kukamatwa alikuwa amefanya kosa gani na hiyo risasi ilipigwa kwasababu gani, “amesema Kamanda Otieno.
Amesema,”Risasi zinauzwa kwenye maduka kama vile mzinga na Tanganyika Arms wanauza kwa hiyo watu wengi tu wanamiliki silaha binafsi hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa ni Polisi , ” Amesema
Hata hivyo ameeleza kuwa inapotokea mtendaji ndani ya jeshi la hilo amefanya vitu vinavyoendana na utovu wa maadili wao kama jeshi la polisi kuna hatua ambazo kuwachukuliwa dhidi yao na kwamba hakuna sehemu inayomuelekeza Polisi kunyanyasa raia.
“Tunafingua jalada la uchunguzi kitu gani kimepelekea mwananchi huyo kulalamika lakini tutaendelea kuchunguza na tutakapopata ushahidi kwamba kuna askari amekiuka amefanya kitendo cha utovu wa nidhamu hiyo ni dhahiri kuwa ameenda tofauti na maadili ya kikazi inavyomtaka na hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao, “amesisitiza na kuongeza, ;
” Inapotokea haki za raia zimekiukwa na askari hatua zinachukuliwa,na hata wanaokuja kwenye vituo vya polisi kuna mabango na namba za simu za viongozi kama atafika pale hatapata huduma bora atatumia namba hizo kupiga kwani mwananchi anahaki ya kuongea na kiongozi na kueleza shida yake, “amesisitiza.
Pamoja na hayo ameeleza, ” Na wapo wengine tunaenda mbali zaidi inapoonekana amefanya suala ambalo lipo kisheria la kijinai tunamfukuza kazi na kumfukisha mahakamani lakini unapoenda kumkamata mtu unamwambia bwana nakukamata au upo chini ya ulinzi na lazima unamwambia unamkamata kwasababu zipi,
Unapaswa kumwambia bwana unatuhumiwa kwakufanya kosa moja mbili tatu kwa hiyo tunakuhitaji twende kituoni tukafanye mahojiano kuhusiana na malalamiko ambayo umefunguliwa pale kituoni kwahiyo ni haki na ni wajibu wa askari kumwambia raia pale unapomkamata na umueleze kosa lake ni nini, “amesisitiza .
Pamoja na hayo aliwataka watendaji wa Jeshi hilo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ,kanuni na miongozo inayowaongoza kiutendaji bila kuleta hofu wala unyanyasaji kwa raia
Kwa upande wake msemaji wa Jeshi la Polisi nchini SACP David Misime ametilia mkazo kuwa kupitia tuhuma hizo jeshi hilo litashirikiana na wataalam wengine wa haki jinai kuchunguza malalamiko yote ili haki itendeke.
Misime ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye ushahidi kulingana na malalamiko yalivyo wasisite kujitokeza ili uchunguzi huo ukamilike mapema na hatua nyingine za kisheria zifuatwe.
Ikumbukwe kuwa hayo yametokea kutokana na Mhanga wa ukatili huo Kalamba Ramadhani(38 )mkazi wa mtaa wa National Housing-Kanyamala Kata ya Makole kulalamikia Jeshi hilo kumteswa na kumchukua kinguvu na kumfanyia vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa mpaka kujeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wake nyumbani kwake Disemba 17 mwaka huu.
Kalamba ameomba msaada wa kisheria kutokana na kufanyiwa vitendo vya kikatili na watu hao wanaowadhania ni askari polisi na kueleza kuwa yeye anajishughulisha na ufugaji wa Ng’ombe,Bata,Sungura,kuku na Mbwa,lakini alishangaa siku ya Jumapili Disemba 17,2023 anapigiwa hodi nyumbani kwake alipofungua mlango mtu mmoja akamkunja nguo ya juu shingoni(akamkwida)na kumvuta nje .
“Nikamwambia unanivuta wewe ni nani,kosa langu nini hakuniambia kosa langu akaniambia wewe twende utajua huko huko,nikawambia sasa nitajua huko huko nyie wakina nani ,nikawambia kama polisi basi twendeni kwa mwenyekiti wangu wa mtaa ili ajue kama naondoka mtaani,akaniambia hatujui habari ya mwenyekiti wa mtaa wala nini,
Wakaanza kutumia nguvu,nikawambia kama mnatumia nguvu mimi siwezi kwenda,tukaanza kuvutana kwasababu Mwenyekiti hakai mbali na mimi hadi kufika kwa mwenyekiti wenyewe wakawa wamenizidi nguvu wakanikaba mimi nikawa naita tu mwenyekiti,
“Mwenyekiti akatoka anawauliza vipi? Wakaanza kupiga risasi hewani hakumsikiliza kulikuwa kunakipaimara ya watoto,watoto wakaanza kukimbia,mwisho wa siku wakanifunga pingu miguuni na mikononi wakanitupia kwenye kruza mkonge wakaondoka na mimi,njiani sijui nilikuwa naelekea wapi nashangaa tu magunia ya mkaa yanarushiwa humo ndani nikiwa nimelala chini nikichungulia naona magunia yale yanawekwa kwa wauza chipsi,mama ntilie , “anaeleza Kalamba
Vilevile anasema,”Yale magunia yalivyoisha nikapelekwa kituo kimoja kinaitwa Nkuhungu wakaniingiza huko ndani wakanivua nguo zote wakanivalisha pingu tena miguuni na mikononi wakaniingiza lile chuma katikati yule jamaa alikuwa anakunywa maji huku kanivua nguo ananimwagia makalioni na mwingine ananipiga sana mpaka nikapoteza fahamu damu zinatoka puani,walivyoona siwezi kuongea ndiyo wakanipeleka nje kwenye upepo ,nilipopata fahamu kuzinduka wakaniingiza kwenye gari tena wakanipeleka centro wakaniacha hapo centro,”anaeleza
Pia anadai kuwa,”Nilipokuwa ndani kule sikuelewa kitu chochote kilichotokea nikaja kuambiwa wewe unatuhumiwa kuvunja duka ,nikawaliza mimi nimevunja duka vipi,basi kilichoendelea nikaa mule ndani siku tatu na ndugu zangu wakaja kunitoa, “amesema.
Mnenge anaeleza kuwa licha majeraha makubwa waliyomsababishia sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kushindwa kutembea na kuongea vizuri lakini ameathirika kwa kiasi kikubwa kwasababu ndani ya siku hizo nne ,huwa anakamua ng’ombe maziwa asubuhi na jioni na huwa wanatoa lita saba hadi nane lakini muda wa siku nne zote hizo ng’ombe hawakukamuliwa wala chochote kile hakikufanyika na nyumbani amekuta baadhi ya mifugo yake imekufa mingine imepotea .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo Asha Athman amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wakati Kalamba anachukuliwa watu hao wanao sadikiwa kuwa askari polisi hawakutaka kumsikiliza licha ya kuhitaji kuongea nao kabla ya kuondoka.
“Walitukosea sana, tunajua ukifika mtaani mwenyeji wako ni mwenyekiti, lakini wao walikuja wakaanza kututisha na kuwavuruga watoto, hadi sasa watoto wa mtaa huu hawana amani, tunaomba Jeshi letu litumie hili tukio kama funzo kwao, ” amesema