Jeshi lisilo rasmi la vijana zaidi ya 60 wanaofanya kazi ya kubeba abiria kwa kutumia pikipiki (bodaboda), huku wakiimba kibwagizo cha ‘wapigwe tu’, wameteka mtaa na kutembeza kipigo kikali kwa abiria wao mmoja.
Abiria huyo, Peter Mwininga, daktari katika Hospitali ya Wilaya ya Geita alishushiwa kipigo na kutakiwa kulipa nauli zaidi ya ile waliyokubaliana awali.
Imeelezwa kuwa wakati bei halisi na iliyozoeleka hapa mjini Geita kwa tripu moja ya pikipiki ni Sh 1,000; mwendesha bodaboda aliyekuwa akidai Sh 2,000 kwa tripu mbili, aligoma kupokea kiasi hicho cha pesa kutoka kwa daktari huyo akitaka apewe Sh 3,000 kwa madai kuwa 1,000 ilikuwa ni ya usumbufu, ndipo mzozo ulipotokea na kuzusha vurugu hizo.
Jambo hilo la kuogofya na lililoonesha kushangaza wengi, lilitokea wiki iliyopita saa 1:30 usiku katika Mtaa wa Misheni, Kata ya Kalangalala.
Gazeti hili lilifika eneo hilo muda mfupi na kukuta daktari huyo anatokwa na damu nyingi puani, kutokana na kipigo alichokipata huku akiwa kifua wazi baada ya nguo zake kuchanwa.
Wakati huo Dk. Mwininga alikuwa amehifadhiwa ndani ya kibanda kimoja chenye milango ya vioo kinachotumika kwa biashara ya Internet kumnusuru asiuawe, huku ‘bodaboda’ hao wakiwa wanapiga yowe wakimtaka mmiliki wa kibanda hicho amtoe nje ili wamuue kwa kile walichodai Serikali imeshabariki watu kama daktari huyo kupigwa na hata kuuawa.
“Tunaomba umtoe nje jambazi huyo…hao ndiyo wanauza dawa zetu hospitali…tutavunja kibanda chako…unafuga wezi siyoo…tumekwishaambiwa watu kama hao ni kipigo tu, tumechoka,” walisikika vijana hao wa bodaboda wakipiga yowe kushinikiza daktari huyo atolewe nje ya kibanda hicho ili wamuue.
Kutokana na hali hiyo, gazeti hili liliwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, Leonard Makona, na kumueleza hali halisi ilivyokuwa eneo hilo, ndipo akatuma askari wakafika eneo hilo na kumuokoa daktari huyo na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.
Mganga wa zamu aliyempokea majeruhi huyo, Juvenari Mganyizi, alilieleza gazeti hili kwamba vipimo vilibaini kuwa taya zake zilikuwa zimelegea kutokana na kipigo alichokipata, lakini akasema hali yake inaendelea vizuri baada ya kumpatia matibabu.
Jeshi la Polisi wilayani Geita limethibitisha kuwatia mbaroni waendesha bodaboda wawili, wakihusishwa na tuhuma za shambulio la kudhuru mwili, huku likiendelea kuwasaka wengine. Watuhumiwa walitarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika.
Hata hivyo, baadhi ya watu akiwamo Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Hospitali ya Wilaya ya Geita, Mary Muntu, wamelaani tukio hilo na kuiomba Serikali kufanya uamuzi mgumu wa kufuta biashara ya bodaboda kabla madhara makubwa hayajatokea, kutokana na ukweli kuwa matukio ya waendesha bodaboda kuwashambulia raia yamekuwa yakiongezeka kwa kwasi mkoani Geita.
“Tunaiomba Serikali ijaribu kuliona hili, maana matukio ya vijana wa bodaboda kuwashambulia raia yamezidi bila kujali wao ndiyo wakosaji…. Mkuu wetu wa Mkoa, Magalula Said, kama aliweza kufuta biashara ya magari madogo (mchomoko) yaliyokuwa yanamaliza watu kwa ajali za kila siku na akafanikiwa, tunaamini hata akiamua kufuta bodaboda atafanikiwa, vinginevyo wanaandaa bomu jingine,” alisema Muntu.