Wakati gumzo la mkataba wa uwekezaji Bandarini Dar es Salaam likiendelea, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mita ji ya Umma (PIC) ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa ameelezea mengi ikiwemo hoja za kisheria ambazo amedai baadhi ya wanasheria wanaozijadili aidha hawazijui au wanafanya makusudi.

“Ukiwasikiliza wengi mtu anaweza kuongea kwa dakika 15 lakini hakuna sehemu yoyote anafika kuzungumzia yale makubaliano yenyewe yaliyoingia kati ya Serikali yetu na Serikali ya Dubai na wanafanya hivyo kwa makusudi kwa sababu yapo maneno mengi ambayo unaweza kuongea na ukatengeneza sintofahamu na taharuki.

“Zipo hoja za kisheria ambazo na zenyewe ninasikitishwa baadhi ya wanasheria kuzijadili katika mrengo ambao aidha hawazifahamu au wanafanya makusudi, kwa mfano IGA ni makubaliano ya Kimataifa”

“IGA ukiisoma hakuna eneo lolote bandari inaenda kubinafsishwa, IGA inaenda kujenga msingi wa kwenda kuingia kwenye mkataba wa uendeshaji, swali ni je hii ni mara ya kwanza?, leo ukienda Uwanja wa Ndege wa Mwl Nyerere unamilikiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege lakini ukienda kuangalia operesheni za uwanja zinafanywa na Sekta binafsi”

“Swali linakuja je pale Airport masuala ya ulinzi na usalama yanasimamiwa na nani?, yanasimamiwa na Serikali chini ya Vyombo vyetu pale kuna Kituo cha Polisi , je kodi inakusanywa na nani pale Airport?, inakusanywa na TRA”

“Wiki iliyopita serikali iliingia mkataba na Uropean Union ya Budget Support, mliona watu wakijadili kuwa fedha hizi zinatoka kwa Mzungu? Juzi tumepitisha bungeni bajeti ya Sh Trilioni 44.39. Lakini watu wameshika jambo moja tu, hivyo nashawishika kusema kuwa kuna nguvu inatumika nyuma ya hawa wanaopotosha. Ndio maana nimeona nije hapa kutoa wito kwa serikali juu ya suala hili la bandari,”Jerry Silaa Mbunge Ukonga.

“Jamii ya Kitanzania ni watu wenye busara na kuheshimiana sana na watu wanaojadiliana mambo kwa hoja. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) tulipata maoni mengi kutoka kwa Watanzania na wasomi wengi. Maoni mengi yanahusika zaidi na mikataba ya utekelezaji na yamepelekwa serikalini yazingatiwe kwenye uaandaaji wa mikataba hiyo. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maeneo yote hayo yatazingatiwa.” Jerry.