Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jenerali mstaafu George Waitara, amewatumia salamu wanasiasa na viongozi wa Serikali ambao, kwa namna moja ama nyingine, wamekuwa nyuma ya wahalifu wanaojihusisha na ujangili.

Waitara amewataka wote wanaojihusisha na ujangili kuacha mara moja biashara hiyo, na badala yake watafute kazi nyingine na wataokaidi onyo hilo basi wajiandae kukabiliana na vita.

Onyo hilo alilitoa hivi karibuni muda mfupi kabla ya kuanza safari ya siku sita kupanda Mlima Kilimanjaro, akiongoza kundi kubwa la wanahabari, wanajeshi na wanadiplomasia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wa Tanzania Bara.

“Natoa wito kwa viongozi wetu, wanasiasa na wafanyabiashara, tusaidieni kukabiliana na ujangili na msiwe wahamasishaji wa ujangili pamoja na kuwatetea wahalifu wanaojihusisha na ujangili,” amesema Waitara.

Jenerali Waitara amesema makundi ya wahalifu yanayoendesha ujangili wa kuua wanyama yanajulikana na wanaofanya uhalifu huo wanafahamika, kwani baadhi yao wanasaidiwa na wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi za Taifa ambako ujangili umekuwa ukifanyika.

Waitara aliweka wazi kuwa tatizo la ujangili wa kuua wanyama ni kubwa na kulitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kujipanga kikamilifu kupigana vita hiyo dhidi ya ujangili.

“Wanaoshiriki kwa namna moja ama nyingine katika vitendo hivyo vya ujangili wote ni wahalifu na watajumuishwa humo, niwaombe tu wote mnaoshiriki vitendo hivyo acheni; tafuteni kazi nyingine za kufanya; zipo nyingi tu,” ameonya Jenerali Waitara.

Agosti mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alizindua kitabu cha kuhamasisha ulinzi wa tembo na faru kiitwacho ‘Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania’ kilichoandaliwa na Kamati ya Amani ya viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Profesa Maghembe, ambaye alizindua kitabu hicho kwa niaba ya Rais John Magufuli, alinukuliwa akisema Tanzania ni nchi ya pili duniani yenye mbuga nzuri na bora ikitanguliwa na Brazil na kusisitiza umuhimu wa Watanzania kuzitunza rasilimali hizo zikiwamo mbuga na wanyamapori.

Aliongeza kuwa wanyamapori ni muhimu sana katika maisha ya kila Mtanzania kwa kupitia sekta ya utalii kutokana na kuchangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje, hivyo hakuna budi kwa kila Mtanzania kupiga vita ujangili.