Na Daniel Limbe,Chato

MKAZI wa kijiji cha Bwanga,wilayani Chato mkoani Geita, Faida Enocka,amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi milioni 3, baada ya kupatikana na hatia ya kumkata na kumjeruhi, Monica Laurent Nonga, mkazi wa kijiji cha Butobela Buseresere.

Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya Wilaya ya Chato kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na pande mbili kati ya mwendesha mashitaka wa Jamhuri, na mshitakiwa katika kesi hiyo namba 757 ya mwaka 2023 ambapo baada ya kujiridhisha pasipo shaka mahakama ikafikia uamuzi huo.

Awali mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Mauzi Lyawatwa,amesema mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 20, 2022 majira ya saa 2, usiku, baada ya kumkuta Monica ambaye ni mama yake mdogo akiwa nje ya nyumba akiandaa chakula cha usiku.

Baada ya kutekeleza unyama huo mshitakiwa aliondoka na kwenda kujificha kabla ya kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani Oktoba 26, 2023 kwa ajili ya kusomewa shitaka linalomkabili.

Amesema kitendo cha kujeruhi mtu mwingine ni kinyume na kifungu cha namba 225 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Licha ya mshitakiwa kukana kutenda kosa hilo,bado haikumsaidia kukwepa mkono wa sheria baada ya ushahidi kuwasilishwa mahakamani hapo ikiwemo mtu aliyejeruhiwa na kuithibitishia mahakama hiyo.

Baada ya mahakama kujiridhisha pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo akiwa na nia ovu, upande wa Jamhuri ukaiomba mahakama hiyo kutenda haki kwa kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ikiwa ni pamoja na kumlipa fidia majeruhi.

Hatua hiyo inatokana na mjeruhiwa kupoteza viganja vya mikono yake kutokana na imani za kishirikiana hata hivyo kutokana na ukatili huo mtuhumiwa amekuwa tegemezi kwa watu wengine ikilinganishwa na awali alipokuwa akifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe.

Hata hivyo baada ya mahakama kumpa nafasi ya kuomba kupunguziwa adhabu, mshitakiwa huyo amesema anaishi na watoto pamoja na mama yake mzazi ambaye ni mlemavu na kwamba wote wanamtegemea katika malezi na matunzo hivyo mahakama hiyo imuonee huruma.

Akisoma hukumu ,Hakimu mkazi wa mahakama hiyo,Erick Kagimbo, amesema kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa na pande zote ikiwemo utetezi wa mshitakiwa mwenyewe, mahakama hiyo inamhukumu kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi milioni 3 ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia kama hiyo.

Hata hivyo,mahakama hiyo imesema mshitakiwa bado anayo fursa ya kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na adhabu iliyotolewa dhidi yake.

Baada ya hukumu hiyo,mshitakiwa amechukuliwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi na kupelekwa kwenye gereza la wilaya ya Chato kuanza kutumikia kifungo chake.

    
Please follow and like us:
Pin Share