Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Igunga
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemuhukumu Hamisi Ndari (33) mkazi wa kitongoji cha Mizanza, Kata ya Sungwizi kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mtoto wa miaka 14 mkazi wa kijiji cha Buhekera kitongoji cha Mizanza.
Kabla ya kutoa hukumu, Mwendesha Mashitaka kutoka ofisi ya mashitaka Wilaya ya Igunga Albanus Ndunguru aliiambia mahakama mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Igunga Edda Kahindi kuwa mshitakiwa Hamisi Ndari alitenda kosa hilo kati ya Agosti, 2023 hadi Oktoba 18, 2023
Ndunguru aliendelea kuiambia mahakama kuwa katika tarehe hizo tofauti, mshitakiwa huyo alikuwa akimwingilia mtoto huyo (Jina limehifadhiwa).
Aidha, Ndunguru alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 na 131 kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2022 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na ndipo upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi wanne ambao wote walitoa ushahidi wao.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, hakimu Edda Kahindi alisema pasipo shaka ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umemuona mshitakiwa ana hatia.
Alisema kwa kuwa vitendo hivi vimekuwa vikijirudia mara kwa mara kwa baadhi ya wananchi licha ya Serikali kukemea vitendo hivyo, kwa hivyo mshitakiwa atakwenda jela miaka 30 ili iwe fundisho kwa watu wengine.