Utangulizi
Ni kawaida unapopita mitaani au sehemu mbalimbali mijini au vijijini hasa kwa wingi kabisa katika miaka ya hivi karibuni, kuona maneno kama Company Limted. Sijui kama uliwahi kujiuliza maana ya neno hili Limited (Ltd).
Pasi kuwaongelea raia wa kawaida wa mitaani ambao husoma neno hili katika mbao za matangazo na kwenye mabango mbalimbali ya kibiashara ambayo hubandikwa mitaani au nje ya ofisi mbalimbali, wapo watu ambao wana makampuni na wanalitumia pia neno hili lakini inawezekana wakawa hawajui hata maana yake. Ni wakati sasa wa kufahamu maana na matumizi ya neno hili.
Awali ya yote ni vyema kufahamu kuwa neno hili lina maana kisheria na limewekwa kwa mujibu wa sheria na matumizi yake ni ya kisheria. Unapolikuta pahala ujue halijakaa kwa bahati mbaya au halijawekwa kwa ajili ya urembo au kupamba matamshi.
Nini maana ya neno Limited (Ltd)
Kwa tafsiri ya moja kwa moja ya Kiswahili twaweza kusema ‘Limited’ ni kikomo, ukomo, au mipaka. Zote ni maana za neno hilo na hutumika kwa utofauti kutokana na kinachoelezwa. Katika makala haya tutatumia neno ukomo ili kumaanisha ‘Limited’.
Katika sheria hasa Sheria ya Makampuni ambayo hasa ndiyo inayoangaziwa leo, neno ‘limited’ linapotumika humaanisha ukomo wa hatia au ukomo wa uwajibikaji wa wanachama katika kampuni (Limited Liability). Ni kwa namna gani kuna ukomo wa uwajibikaji kwa wanachama katika kampuni na katika lipi wanawajibika tutaona baadaye.
Aina za Limited
Ni vyema kufahamu kuwa ‘Limited’ nazo zina aina. Si kila limited unayoiona inafanana na nyingine. Mara nyingi hutegemea kampuni imeundwa kwa limited ipi. Zipo aina mbili za limited.
Kwanza kuna limited ya hisa, hii hujulikana kwa jina la kitaalamu kama (Company limited by shares). Pili kuna limited ya makubaliano ambayo kwa kitaalamu huitwa (Company limited by guarantee). Pamoja na aina hizo kutofautiana lakini bado zote katika matumizi huwakilishwa na neno moja tu yaani (limited). Hii ni kumaanisha kuwa utofauti wake hauondoi msingi wa limited. Katika kuandika matangazo au mabango sote tutaandika, Mfano Co Ltd au … & Co. Ltd na si vinginevyo. Tofauti hujionesha katika katiba. Uchambuzi kuhusu aina hizi za limited nitazionesha kipengele kinachofuata.
Neno limited humaanisha nini litumikapo katika kampuni?
Utaratibu wa Limited upo kulinda maslahi ya baadaye ya kampuni hasa kipindi kampuni inapokuwa inakufa au inafilisika. Kwa kawaida kampuni inapokuwa inakufa au kufilisika hujikuta ikiwa na madeni mengi kutoka kwa wadai mbalimbali. Kufa kwa kampuni hakumaanishi kufa kwa deni la wadai, hapana. Wadeni wanatakiwa kupata haki zao. Katika kuhakikisha wadeni wanapata haki zao ndipo huu mpango wa limited ukaanzishwa. Hapo juu tumeona aina za limited kuwa kuna limited ya hisa (limited by shares) na tukaona kuwa kuna limited ya makubaliano (limited by guarantee). Sasa kwa undani kiasi tuangalie mojamoja.
(a) Limited ya hisa (Company limited by shares). Maana yake ni ukomo uliofungamana na hisa. Katika kampuni kila mwanachama (member) anakuwa na hisa zake. Hisa hizo huwa unaomba na unapewa. Kila hisa anayopewa mwanchama huwa inalipiwa na ina thamani yake. Kwa hiyo, mwanachama anaweza kuwa na hisa ambazo anazimiliki akiwa tayari amezilipia au hajazilipia au amezilipia nusu.
Katika hali hii kama inatokea kuwa kampuni inakufa aidha kwa kufilisika au sababu nyingine yoyote, zile hisa za wanachama ambazo walikuwa wanazimiliki lakini hawajazilipia ndizo zitakazokamatwa na kuingizwa katika kampuni ili zitumike kulipia madeni. Aidha zile hisa ambazo mwanachama alikuwa amezilipia haziwezi kutumika kulipa madeni ya kampuni na kamwe haziwezi kukamatwa.
Na kama kuna mwanachama ambaye alikuwa amelipia hisa zake zote kwa ukamilifu, basi hakuna hisa zake zitakazokamatwa atabaki salama na hawezi hata kidogo kulazimishwa kutoa mali yake nyingine yoyote ili kuchangia deni la kampuni. Hapa ndipo tunapopata maana ya kwanza ya neno limited ikiwa na maana ya ukomo wa uwajibijikaji. Katika kuweka sawa zaidi hapa tunaona kuwa ukomo au limited wa kuwajibishwa kwa mwanachama umehusisha kukamatwa kwa hisa zake ambazo hajalipia.
Kwa maana kama kampuni isingekuwa na ukomo kwa maana isingekuwa limited’ ingewezekana kukatwa hisa zote ambazo zimelipiwa na ambazo hazijalipiwa na hata ikiwezekana mali zake nyingine binafsi, lakini kwa sababu kuna ukomo (limited) basi kikomo kinalazimisha kukamata zile hisa ambazo hazijalipiwa tu na si vinginevyo. Msisitizo ni kuwa uwajibikaji wa mwanachama katika kulipa deni upo kwenye hisa na maalum kabisa hisa ambazo hazijalipiwa.
Mwanachama hawezi kuitwa kuchangia chochote isipokuwa zitatumika hisa zake ambazo alikuwa hajalipia na kama amelipia zote hachangii kingine chochote. Na hii ni hata kama deni la kampuni ni kubwa kuliko hata mali zote ilizobaki nazo, aliyelipia hisa zake zote kwa ukamilifu hachangii kingine chochote. Ndiyo maana huitwa uwajibikaji wenye ukomo (Limited Liability).
(b) Limited ya makubaliano (Limited by guarantee), kwa ufupi hii humaanisha kuwa kampuni itaendesha shughuli zake kama kawaida ila itakapotokea kuwa kampuni imekufa kwa sababu ya kufilisika au sababu nyingine, wanachama (members) watatoa michango yao kila mmoja ili kuiwezesha kampuni kukidhi mahitaji yake ikiwamo madeni. Uwajibikaji wa wanachama katika kampuni za namna hii upo katika kuchangia. Pesa wanayochangia huitwa “guarantee fund”.
Katika limited hii wanachama hawachangii chochote mpaka kampuni isemwe kuwa imefilisika kabisa. Ikiwa kampuni inaelekea kufilisika lakini haijafilisika wanachama hawawezi kuchangia. Limited hii huwa haipendwi sana na ni mara chache kukuta kampuni imesajiliwa namna hii. Kampuni za aina hii ni chache. Na hazipendwi. Kampuni za namna hii mara nyingi hazina mtaji wa hisa (share capital) na hivyo wakati wa kufilisika inapotakiwa kulipa deni panakuwa hamna cha kukamata na hivyo wanachama kutakiwa kuchangia.
Je, yawezekana kuwapo kampuni bila limited?
Tumeona hapo juu maana hasa ya limited na mazingira yake na tukasema kuwa hiyo ni kwa mujibu wa sheria. Pia tunaona makampuni mengi ni limited na kila anayeanzisha kampuni lazima aandike Limited (Ltd). Swali ni je, lazima kampuni iwe limited?
Jibu ni hapana, si lazima kila kampuni iwe limited. Yawezekana ikaundwa kampuni bila kuwa limited. Kampuni ya aina hii huitwa ‘Unlimited Company’. Hivyo basi kama limited company maana yake ni kampuni zenye ukomo basi unlimited company ni kampuni isiyo na ukomo. Tumeona kuwa neno limited linatumika kueleza uwajibikaji wa wanachama kampuni inapokuwa katika msukosuko wa kufa.
Hivyo basi ukomo wa uwajibikaji katika kampuni za namna hii hauna mipaka(unlimited). Hii ina maana kuwa hata mali binafsi za wanachama zinaweza kutumika kulipa deni la kampuni. Wakati katika ‘limited’ hilo haliwezekana na hiyo ndiyo mipaka yake. Hii haina mipaka, wanachama wanalazimika kulipia kampuni deni. Kampuni za aina hii nazo hazipendwi sana.
Nimalizie kwa kusema kuwa neno ‘limited’ unapoliona limeandikwa huwa limaanisha nilichoeleza hapa juu. Halitumiki kunogesha matamshi au kuelezea ufahari.
Barua pepe ; [email protected]