Kitaalamu, lugha ni mfumo wa ishara za sauti za nasibu zilizochimbuka kiholela, baadaye zikakubalika kwa mawasiliano baina ya wanajumuia wa jamii moja. Ni chombo katika kuunganisha pande mbili kifikra, kielimu, kiujuzi na kadhalika.
Ni mfumo unaotumika kwa utaratibu wa utii, usanifu na nidhamu kuepuka kutokea vurumai. Lugha yoyote duniani inajengwa, inakua, inatunzwa na inakufa. Baadhi ya lugha zimepotea na watu kupoteza lugha mama zao.
Watanzania tunazo lugha nyingi mbalimbali, yaani lugha mama zitokanazo na makabila yetu yapatayo 125. Lugha zote hizo zinatumika katika shughuli za kazi, matambiko, misiba, michezo, utamaduni na maendeleo yetu.
Baada ya nchi yetu kupata uhuru na kuanza kurudisha utu na utamaduni wetu, tuliamua kujenga lugha yetu ya Kiswahili na kuipa hadhi ya kitaifa. Desemba 10, 1962, Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipolihutubia Bunge la Tanganyika kwa mara ya kwanza alitumia Kiswahili na kuacha kutumia Kiingereza.
Katika kuonyesha nia na kujali lugha na utamaduni wetu, mwaka huohuo kuliundwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Mwaka 1963 Kiswahili kilianza kutumika rasmi katika Bunge. Fumba fumbua liliundwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), mwaka 1967.
Baraza la Kiswahili la Taifa – BAKITA – lilipewa majukumu ya kustawisha Kiswahili kuwa lugha ya taifa, pamoja na kusimamia matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili kwa kuzuia upotoshaji wake kwa njia ya uelimishaji.
Hapo awali nimesema lugha inajengwa. Kwa maana watumiaji lugha wanatoa maneno na maana mpya wakati wa matumizi. Lugha inakua. Kwa maana inapata matumizi bora, sanifu na mashiko. Lugha inakufa. Kwa maana inakosa kitaalamu utunzaji, ubunifu na msamiati wakati wa matumizi.
Mtaalamu na gwiji wa Kiswahili mmoja nchini, Zacharia Mochiwa (sasa ni marehemu), amesema: “Ni muhimu kuona mabadiliko ya lugha kutokana na kubadilika kwa wakati. Ni kweli kwamba lugha inabadilika kila siku.”
Anaendelea kusema: “Kiswahili cha miaka hamsini iliyopita hakiwezi kuwa sawa na hiki kilichopo hivi leo. Ukubwa wa mabadiliko haya huzidiana kwa kadiri nyakati zinazohusika zinavyoachana.”
Hivi sasa tunavyozungumza vijana wetu, ukiwasikiliza katika mazungumzo yao, simulizi za nyimbo, ushairi na ngonjera zao, utabaini mambo mapya katika matumizi ya nahau, istilahi na msamiati kwa kupewa fasili na maana mpya. Na pengine ukashindwa kuwaelewa wana maana ipi.
Mathalani, neno ‘BAHARIA’ kwao lina mshiko na maana tofauti na ile unayoifahamu wewe kiuzoefu. Kamusi Kuu ya Kiswahili katika uk. 56 inasema: “baharia – mtu anayefanya kazi kwenye chombo cha baharini.” Kwa maana ile ile – mwanapwa au mwanamaji.
Vijana wanaeleza: “baharia ni mtu wa kujituma, mwenye kupambana na hali ilivyo katika mazingira aliyomo.” Wanasema Zaidi: “Mshikaji anayejimudu bila kutetereka katika maisha yake.” Anakomaa na hali halisi ilivyo hususan ni mwanamume.
Nimefanya utafiti kwa vijana wa kiume wachache na kupata sampuli mbalimbali zenye maana hiyo. Vijana wa kike wachache wanasema: “Baharia ni sifa na mambo yanayowahusu wanamume.” Lo! Salalaa! Haya ni majambo. Twendeni, lakini tutafika.
Nawaomba wadau wa lugha ya Kiswahili pamoja na BAKITA, UKUTA, TATAKI na Kamusi Kuu ya Kiswahili kutupia jicho neno baharia na maneno mengine katika lugha yetu ya Kiswahili, tuweze kwenda na wakati.