Nakukumbusha tu msomaji wa safu hii kuwa mwezi Oktoba huadhimishwa kwa kuinua uelewa kuhusu saratani ya titi.

Hii ni kutokana na kalenda ya magonjwa ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya afya (WHO) kwa lengo la si tu kuinua uelewa, bali kuongeza mapambano dhidi ya saratani ya titi, saratani ambayo huanzia kwenye tishu za titi.

Saratani ya titi imekuwa ikitishia uhai wa idadi kubwa ya wanawake duniani. Imeripotiwa kuwa wanawake waishio kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania, wamo hatarini zaidi kuugua aina hii ya saratani.

Sababu kubwa ikiwa ni kukosa uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huu. Ikiwa leo ni siku chache tangu tumalize mwezi Oktoba, ni vema tukakumbushana mambo machache kuhusu saratani ya titi.

Miezi kadhaa iliyopita kupitia safu ya Afya ni Mtaji, nilieleza kuhusu dalili za saratani ambazo hupaswi kuzifumbia macho kabisa. Kuhusu saratani ya titi nilieleza kuwa ni vema kuzitilia maanani dalili kama uvimbe kwenye titi, ngozi ya titi kubadilika rangi, kutokwa matone kweye chuchu, na hata maumivu madogo madogo kwenye chuchu. Hata hivyo kama unapata maumivu yoyote kwenye matiti kwanza ondoa hofu.

Maumivu kwenye matiti yanasababishwa na mambo mbalimbali, leo nitaeleza aina kuu tatu za maumivu ya matiti na sababu zake.

Aina ya kwanza ya maumivu yanayojitokeza kwenye matiti kitaalamu yanaitwa ‘cyclical breast pain’. Maumivu haya mara nyingi huwa yanakuja na kupotea kwa vipindi tofauti.

Maumivu haya hujitokeza mara nyingi wakati wa hedhi na hutoweka wakati hedhi inapokoma. Hivyo ni kawaida kwa mwanamke anapokuwa kwenye mzunguko wa hedhi, hasa akiwa kwenye umri wa miaka 30 hadi 40.

Aina nyingine ya maumivu kwenye matiti ni ile inayojitokeza mara kwa mara bila wakati maalumu. Aina hii kwa kitaalamu inaitwa non-cyclical breast pain. 

Aina hii ya maumivu huwapata wanawake wenye umri uliozidi miaka 40 na wale ambao wamefikia umri ambao hawawezi tena kuzaa. Hii inaweza kutokea kwenye titi moja au matiti yote. Ni muhimu kuchunguza kama maumivu haya yanatoka kwenye matiti yenyewe au kwenye misuli. Na ni vema kupata msaada wa daktari ili kutambua.

Aina ya mwisho ni yale maumivu yatokanayo na maambukizi ya magonjwa mbalimbali. Inaitwa mastitis and shingles. Maambukizi hayo mara nyingi hutokea wakati wa ujauzito kutokana na mabadiliko ya mfumo wa homoni yanayojitokeza kwa mjamzito mara kwa mara.

Mjamzito anashauriwa kupata ushauri wa kitaalamu katika kipindi hiki ili maambukizi na maaumivu haya kwenye matiti yasiathiri afya yake na mtoto.