Msomaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson, alinitumia pongezi na kuniuliza swali hili: “Sanga, kwanini wataalamu mnasema biashara ni kipaji? Usemi huu una maana gani? Na mfano hai, tazama jamaa zetu Wahindi, kwa Watanzania angalia Kanda ya Kaskazini – Wachagga; kwa Nyanda za Juu Kusini angalia Wakinga. Unasemaje hapo?”
Katika makala ya leo nitajikita kulijibu swali hili.
Bahati nzuri ni kwamba nimesoma Shahada ya Biashara nikiwa chuo kikuu na huu mjadala wa ikiwa biashara ni kipaji ama la ulikuwa ni sehemu ya ‘assignments’ zetu katika somo la Ujasiriamali (Entrepreneurship). Mjadala huu unapatikana katika kitu wanachokiita tetesi (myths) kuhusu ujasiriamali.
Ni katika myths hizi ndipo utakutana na swali lisemalo: Je, wajasiriamali huzaliwa ama hutengenezwa? (Are entrepreneurs made or born?) Swali hili huambatana na malumbano makali yenye ushahidi kutoka kila upande (ikiwa wanazaliwa ama wanatengenezwa).
Bila shaka ni katika mjadala ama maandiko ya namna hii ndipo msomaji wetu Jackson akadadisi ili kujiridhisha ikiwa biashara ni kipaji ama la?
Katika swali hili sitakuwa na jibu la moja kwa moja na hatua kwa hatua naweza kupishana na wataalamu wengine wa masuala ya biashara. Hata hivyo, mjadala wangu utaegemea upande wa uzoefu wa kivitendo katika eneo hili la biashara.
Bahati nzuri ni kuwa mimi ni Mkinga na tena ni mfanyabiashara. Hivyo, kwa sehemu fulani nina wasaa wa kueleza hiki kinachoitwa siri ya mafanikio na vipaji vya Wakinga (na ndugu zao Wachagga) katika biashara.
Katika makala haya nitawagusa Wakinga na Wachagga kwanza na ndugu zetu Wahindi nitawapumzisha kidogo leo.
Kitakwimu ni kwamba watu kutoka makabila mbalimbali nchini Tanzania miaka ya zamani (na hasa miaka ya sasa) wamekuwa wakijishughulisha na biashara. Kwa hiyo si Wakinga na Wachagga pekee waliobobea kwenye biashara; ingawa kuna ushahidi usio na shaka kwamba wengi wa Wakinga na Wachagga wanaokuwa kwenye biashara, hung’aa na kufanikiwa kwa kasi.
Kuna utafiti nimepata kuufanya ulioniwezesha kupata misukumo ya kimafanikio kwenye biashara baina ya Wachagga na Wakinga. Katika utafiti wangu nilibaini misukumo ya aina mbili; “push power” na “pull power”.
“Push power” ni ule msukumo unaomlazimisha mtu kutoka eneo duni kiuchumi kuingia kulitafuta eneo bora kiuchumi. “Pull power” ni msukumo anaokuwa nao mtu unaotokana na namna anavyoona hatua za wenzie kiuchumi.
Kihistoria Wachagga waliwahi kujanjaruka ukilinganisha na Wakinga. Kuwahi kwa dini maeneo ya Uchaggani, kuwahi kwa shule, kuingizwa kwa mazao ya biashara na uimara wa tawala za kichifu kulisababisha Wachagga wengi wawahi kujitambua. Wengi wao tangu zamani wakabahatika kusoma, wakabahatika kuwa na imani za kidini na kutambua umuhimu na thamani ya ardhi.
Kwa kadiri miaka ilivyokuwa inaenda, watoto wa Kichagga wanavyokua walibahatika kuwa na watu wa mfano wa kujifunzia namna ya kuishi kiimani, kukazana masomoni na kutumia ardhi kwa umakini; kitu ambacho kilisababisha wengi kuwa katika mtazamo wa kibiashara.
Kutokana na hili vijana wengi wa Kichagga wakawa na cha kujisemea moyoni; mathalani; “Nataka na mimi nisome niwe kama fulani aliyepo sehemu fulani” ama “nataka na mimi nianzishe biashara niwe kama fulani aliyepo sehemu fulani.” Hiki ndicho ambacho tunakiita “Pull Power”.
Kwa upande wa Wakinga, wao mambo hayakuwaendea sawa tangu zamani. Maeneo ya Ukingani (kule Makete na Njombe) mwamko wa elimu ulichelewa, mila na imani za kishirikina zilikuwa na mizizi mikubwa kiasi kwamba dini nyingi hazikujikita tangu zamani.
Hili lilisababisha Wakinga wengi kutokwenda shule, walichelewa kutambua thamani na nguvu ya ardhi; na mwisho wengi walijikuta kuwa hali za kiuchumi ni ngumu na mbaya.
Historia inatueleza kwamba kutokana na ugumu wa maisha, asilimia kubwa ya vijana wa Kikinga walikuwa wakilazimika kuchukuliwa kama manamba na kwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya miwa (Kilombero na Mtibwa), kwenye mashamba ya katani (Tanga na Morogoro), kwenye mashamba ya chai (Mufindi na Njombe).
Hivyo, utagundua kuwa kilichokuwa kikiwalazimisha kwenda huku na huko kutafuta maisha kilikuwa ugumu wa maisha wa mahali walipokuwapo. Hii hali ya mtu kujikuta huna namna isipokuwa kuondoka na kwenda kutafuta ndicho tunachokiita “Push Power”.
Wakinga wengi walipokuwa wakifika maeneo hayo ya mashamba (wakiwa kama manamba), wengi walikuwa wakipaona mahali hapo kama “peponi” wakilinganisha na mazingira ya kifukara waliyoyaacha kule kwao Ukingani. Kutokana na hili wengi wao walikuwa wakilazimika kupambana kufa na kupona ili kutorudia ufukara waliokuwa nao kule kwao.
Wengi wa Wakinga waliokuwa katika maeneo haya walikuwa wanakataa kurudi kwao ule muda wa msimu unapoisha. Kwa kuwa walikuwa wanabaki katika maeneo yale, na kwa kuwa walikuwa wana shauku ya kujikwamua na ufukara, na kwa kuwa wengi hawakuwa na elimu ya kuweza kuajiriwa, ilikuwa wanalazimika kuanza biashara.
Mara zote ili mtu ufanikiwe na kukabiliana na changamoto ni lazima kuwe na msukumo mkubwa ndani yako unaokulazimisha kuendelea kufanya kile unachokifanya. “Push Power” ndani ya Wakinga ilikuwa kubwa kiasi kwamba mtu alikuwa anaona ni bora afe yeye kuliko kupoteza mtaji alionao kwenye biashara.
Baada ya kutambua ‘backgrounds’ zilizofanya makabila haya mawili kuanza kupenda na kujifunza biashara, nije sasa katika eneo linalowaunganisha Wakinga na Wachagga, hata tunaona mafanikio yao katika biashara. Tabia nyingi (kama si zote) walizonazo Wakinga na Wachagga zinafanana na ndizo zinazowafanya kufanikiwa katika biashara.
Wakinga na Wachagga wana tabia ya kupendana na kushirikiana. Ukiona Mkinga ameanzisha duka sehemu basi muda si mrefu ataenda kule kwao kijijini na kumchukua ndugu ama mdogo wake. Akishamchukua atamweka dukani awe anauza, atamfundisha biashara na mwisho wa siku atamgawia mtaji.
Hulka hii pia ipo kwa wingi kwa Wachagga. Kutokana na moyo huu wa kupendana, kupeana mitaji na kufundishana biashara ndiko kunakosababisha watu wengi wa makabila haya kupata wasaa wa kuanzisha biashara kwa wingi. Mkinga na Mchagga huona fahari kubwa anapoona mtu wa kabila lake amefanikiwa.
Sisemi kuwa Wakinga na Wachagga wana ukabila, la hasha! Lakini ninachokithibitisha ni kuwa hawana wivu wa kifitina. Ukiona Mchagga ama Mkinga ana wivu kwa mwenzake basi ujue ni wa kimaendeleo. Hiki ni kitu kizuri ambacho watu wengine wote yafaa wajifunze.
Kitu kingine ambacho Wakinga na Wachagga wanacho ni katika eneo la kusimamia malengo. Mkinga akishapanga kuwa mwaka huu lazima afungue duka la pili; hayumbi, hatetereki na wala haahirishi, lengo lake hilo mpaka aone limetimia.
Na asilimia kubwa (kama si wote) ya Wakinga licha ya kwamba wengi hawakubahatika kwenda shule; lakini kuna utamaduni imara wa kufanya biashara kwa malengo. Mtafute mfanyabiashara yeyote wa Kikinga popote alipo muulize: Una malengo gani mwaka huu; yaani hata kama yupo usingizini atashtuka na kukutajia malengo yake.
Utamaduni huu wa kupanga na kusimamia malengo upo kwa wingi kwa Wachagga pia. Watafute Wachagga uone watakavyokuorodheshea mambo wanayopanga kuyatekeleza kule kwao Uchaggani na katika maeneo wanayoishi – utafurahi mwenyewe! Na hili sote tunalifahamu. Ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote hakikisha unapanga na kuyasimamia malengo.
Hulka nyingine inayochagiza watu wa makabila haya kufanikiwa kibiashara ni kuweka na kuheshimu akiba. Kwa upande wa Wakinga, watoto tangu wanapozaliwa na kuendelea kukua huwa wanafundishwa tabia ya kuweka na kuheshimu akiba – iwe ni ya mazao ama fedha.
Ukienda kule Ukingani utakutana na vijumba vidogo vidogo viitwavyo “vibana” ambavyo vinatumika kuhifadhi mazao mbalimbali. Kanuni kubwa ni kuwa hutakiwi kutumia akiba ya mazao hayo kabla ya kufika kwa msimu mwingine wa kuvuna. Unapoitumia akiba iliyomo kwenye “kibana” ni lazima uhakikishe kuwa umeshavuna mazao mengine ya kubadilishia humo.
Wakinga wanaamini kuwa mtu unayetegemewa kwenye jamii unatakiwa kuwa na vitu wakati wote. Sifahamu kwa Wachagga wanafanyaje katika suala la akiba ya mazao lakini ninafahamu sifa yao katika akiba ya fedha.
Pia Wakinga katika suala la fedha kuna akiba huwa inaitwa “ekhefumbato”. Hii ni fedha ambayo inakuwamo ndani ama benki ambayo haitakiwi kuguswa kwa namna yoyote ile bila kuwapo ya kubadilishia. Kama akiba hiyo imewekwa kwa lengo la kugharimia ujenzi wa nyumba hapo baadaye, Mkinga (halisi) hatathubutu kuigusa akiba hiyo hata kama imetokea mtoto amefukuzwa shule kwa kukosa ada.
Mkinga yupo tayari kwenda kukopa kwa jirani alipe ada ya mtoto lakini si kugusa akiba kinyume na malengo ya msingi. Hata Wachagga huwa hawana mchezo katika suala la kuheshimu akiba zao – iwe ni nyumbani ama benki. Hii ni siri nyingine kubwa inayosababisha wafanyabiashara wa makabila haya mawili kufanikiwa kibiashara.
Jingine linalowafanikisha hawa jamaa ni nidhamu ya matumizi. Hii nidhamu ya matumizi watu wengi huitafsiri vibaya kwa kusema ni ubahili. Watu wengi wanaamini kuwa Wachagga na Wakinga ni wabahili. Huwa nasikia wanauita “Umangi” na “Ukinga”.
Kimsingi, hili neno ubahili mimi huwa nalitafsiri kwa namna hii: “Ni kutumia fedha kwa kadiri ya ilivyokusudiwa na kupuuza mahitaji yanayoibuka nje ya makusudi na yasiyo na umuhimu mkubwa hata kama yakipuuzwa”.
Unapotumia fedha kwa kadiri ya ulivyokusudia wewe na unapokuwa na utamaduni wa kutomridhisha kila anayekuomba fedha ‘automatically’ utaitwa bahili! Lakini nidhamu ya matumizi iliyopo miongoni mwa Wakinga na Wachagga ni pana na inawasaidia kwa namna nzuri.
Mkinga na Mchagga huwezi kumkuta akiendekeza starehe ama matumizi yanayozidi faida yake katika biashara. Mkinga ni bingwa wa kubana matumizi kiasi kwamba hata awe na duka, chakula cha kula dukani kinatoka nyumbani, akisafiri kibiashara halali hoteli za gharama kubwa. Katika haya yote kwanini wasifanikiwe?
Natambua kuwa kuna ‘myths’ mbalimbali kuhusu mafanikio ya makabila haya kibiashara. Wakinga wanasemwa kwamba wanatumia ushirikina katika biashara zao na Wachagga wanatuhumiwa kwa ujambazi.
Licha ya kwamba makala zijazo nitachambua ‘myths’ hizi lakini niharakishe kusema kuwa hayo ni mambo ya kupuuzwa badala yake tujifunze kutoka haya mazuri niliyoyachambua.
Watanzania wote tunastahili ushindi kiuchumi!
Email: [email protected]
+255 719 127 901.