MWANZA

Na Mwandishi Wetu

Ifikapo Desemba kila mwaka huwa kuna mabishano yanaibuka kuhusu tarehe ya Sikukuu ya Krismasi ilivyopatikana. 

Mwaka 1743, Profesa Paul Jablonski, alihubiri kwamba Desemba 25 ilikuwa sikukuu ya kipagani lakini Kanisa Katoliki likaigeuza kuwa siku ya Krismasi (ya kuzaliwa Yesu Kristo).

Japo wengi wanaifahamu zaidi Desemba 25, lakini tarehe za Krisimasi zipo tatu; yaani Januari 6, Januari 7 na hii ya Desemba 25. 

Walioleta tarehe hizi ni Clement wa Alexandria na Mtakatifu Hippolytus wa Roma.

Ilipofika Desemba 31, 192 (mwaka 192), Clement aliona zimepita siku 70,852 tangu Yesu Kristo kuzaliwa, akaandika kwenye kitabu chake Stromata 1:21. Jibu lake linaonyesha Yesu alizaliwa Jumatano Januari 6.

Hata wewe ukianzia Desemba 31 ya miaka 2192, 4192, 6192, 8192 ukahesabu siku 70,852 kurudi nyuma, kama alivyofanya Clement, utapata jibu linalokuleta kwenye Jumatano ya Januari 6 ya miaka 1999, 3999, 5999, 7999.

Wakristo kadhaa walizikubali hizi hesabu za Clement, wakaifanya Januari 6 kuwa siku ya Krismasi. 

Nchini Armenia wanaziamini hesabu za Clement na hadi leo Januari 6 ndiyo Krismasi inayoadhimishwa na kanisa liitwalo ’Armenian Apostolic Church’.

Tarehe nyingine ya Krismasi ni Desemba 25 na hii ndiyo wengi tunaifahamu. Je, hii ilipatikanaje? Jibu ni refu kidogo.

Mwaka 2000 wakati Papa Benedict XVI akiwa bado anaitwa Mwadhama Joseph Kardinali Ratzinger, aliandika kitabu kiitwacho Spirit of the Liturgy. Tarehe za Krismasi alizozisema Benedict XVI kitabuni humo ndizo alizosema Mtakatifu Hippolytus ambaye mwaka 204  aliandika hivi:

“Tarehe ya kuzaliwa Yesu, Bethlehem, ilikuwa Desemba 25, Jumatano, wakati utawala wa Augustus ulipofikisha miaka 42, ikiwa ni miaka 5,500 baada ya Adam.”

Hippolytus alifanya hesabu zake kwa kutumia tukio la Malaika Gabriel kumtokea Zakaria hekaluni na kumwambia kwamba mkewe, yaani Elizabeth, atapata mtoto naye atamwita Yohane (Luka 1:5-13, 19, 24). 

Je, pale hekaluni Zakaria alikuwa anafanya nini?

Zakariaalitokea katika kizazi cha Harun kilichoagizwa hivi:

“Mara moja kila mwaka Harun atafanya ibada ya malipizi kwa ajili ya dhambi, atafanya mara moja kwa ajili ya malipizi ya altare. Nanyi mfanye hivi katika vizazi vijavyo. Altare hiyo, iliyo takatifu, iwekwe wakfu kwa Bwana.” (Kutoka 30:10). 

Hivyo pale hekaluni Zakaria alikuwa kwenye ibada ya “malipizi ya dhambi” iliyoitwa “Yom Kippur”.

Kwa kalenda ya Kiebrania “Yom Kippur” iliadhimishwa tarehe 10 ya mwezi wa saba unaoitwa “Tishri”, ninanukuu:

“Hii itakuwa kwenye amri ya milele. Katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajinyima nafsi zenu, hamtafanya kazi yoyote tangu mzaliwa mpaka mgeni akaaye kati yenu.” (Walawi 16:29).

Kwa kalenda yetu ya sasa “Yom Kippur” ni Septemba 24. Hii maana yake ni kwamba Elizabeth alianza ujauzito wa Yohane katika sikukuu hii ya “Yom Kippur” yaani “Septemba 24”. 

Je, hii “Septemba 24” aliyoanza huo ujauzito wa Yohane inahusianaje na Krismasi? Uhusiano wa “Septemba 24” ndio unatupa jibu kwamba Yesu alizaliwa tarehe ipi. Tuendelee.

Miezi sita baadaye malaika huyo huyo (Gabriel) alimtokea Bikira Maria na kumwambia atapata mimba kama ambavyo Elizabeth ana mimba ya miezi sita japo ni mzee (Luka 1:24-39).

 Hivyo mtoto Yohane ambaye ujauzito wake ulianza Septemba 24 alimtangulia umri mtoto Yesu kwa miezi sita kama anavyosema Malaika Gabriel.

Narudia; mimba ya Yohane ilipofikisha miezi sita ndipo mimba ya mtoto Yesu ikaanza kama alivyosema Malaika Gabriel (Luka 1: 24-39). Hii inaturahisishia kujua mimba ya mtoto Yesu ilianza tarehe ipi.

Maadam mimba ya mtoto Yohane ilianza “Septemba 24”, hivyo miezi sita baadaye ni Machi 25 ndipo Bikira Maria naye anapashwa habari ya Yesu. Hivyo mimba ya mtoto Yesu ilianza Machi 25.

Hii ndiyo sababu kila ifikapo Machi 25 Wakatoliki tuna sherehe ziitwazo “Annunciation” yaani “kupashwa habari ya kuzaliwa Yesu”.

Tumeona ujauzito wa mtoto Yohane ukianza Septemba 24. Hivyo mimba ya Yohane iliishi hiyo miezi tisa akazaliwa Juni 24 na ndiye ukubwani akaitwa Yohane Mbatizaji. Hii ndiyo sababu kila Juni 24 Wakatoliki tuna sikukuu ya kuzaliwa Yohane Mbatizaji.

Tumeona kwamba mtoto Yohane alimtangulia mtoto Yesu umri kwa miezi sita. Tumeona kwamba Yohane alizaliwa Juni 24, hivyo miezi sita inayofuata ni tarehe ya mtoto Yesu kuzaliwa. Hivyo Yesu alizaliwa Desemba 25, yaani miezi sita baada ya kuzaliwa Yohane Mbatizaji.

Vilevile unaweza kupata tarehe ya kuzaliwa Yesu kwa kujumlisha miezi tisa tangu siku Malaika Gabriel alipomtaarifu Bikira Maria kupata ujauzito wa mtoto Yesu. 

Malaika alimtokea Bikira Maria Machi 25, hivyo miezi tisa ya mimba ya mtoto Yesu kukaa tumboni inaisha Desemba 25.

Hivi ndivyo tarehe ya Krismasi yaani “Desemba 25” ilivyopatikana. Wote Clement na Hippolytus wanaonyesha kwamba Yesu alizaliwa Jumatano.

Wapo Wakristo wanaoadhimisha Krismasi kila Januari 7. Tarehe hii inahitaji maelezo marefu kama ifuatavyo:- 

Mwaka 46KK Julius Caesar aliunda kalenda ili iendane na mzunguko wa jua uliotumia siku 365.25, wakati kalenda ina siku 365 tu. 

Hivyo kila mwaka uliogawanyika kwa nne Julius Caesar aliongeza siku moja, yaani ‘Februari 29’ ukawa na siku 366. Kalenda hii ikaitwa ‘Julian Calendar’.

Baadaye wanasayansi waligundua mzunguko si siku 365.25 bali ni siku 365.24218967. Ukifanya hesabu utaona kwamba kila ifikapo miaka 128.0355631583 mzunguko huo uliitangulia kalenda kwa siku moja.

Ukiachilia mbali wanasayansi, Kanisa Katoliki lilianza kuutumia mzunguko wa jua mwaka 325. Tangu mwaka 325 hadi 1582 ni jumla ya miaka 1257. 

Kimahesabu ni kwamba kufikia huo mwaka 1582  mzunguko ulishaitangulia kalenda kwa siku 9.81758481 ambazo ni siku 10. Hivyo Papa Gregory XIII aliunda kalenda mpya ikaitwa ‘Gregorian Calendar’.

Baadhi ya Wakristo waliikataa kalenda hii wakaendelea na Julian Calendar. Matokeo yake  kutokea mwaka 325 hadi leo imepita miaka 1694, hivyo tumekwisha kuwatangulia kwa siku 13.230699019971 ambazo ukikadiria ni siku 13. 

Hivyo Wakristo wanaofuata Julian Calendar tumewatangulia kwa hizo siku 13. Sisi tunaposherehekea Krismasi Desemba 25 wao wanaisubiri hadi Januari 7.

Nchi ambazo Krismasi ni Januari 7 ni Belarus, Misri, Ethiopia, Georgia, Kazakhstan, Macedonia, Moldova, Montenegro, Urusi, Serbia na Ukraine. 

Itakapofika Mei 2117, yaani miaka 98 (96) ijayo, nchi hizo zitaanza kuadhimisha Krismasi Januari 8, kwa sababu itakuwa imeongezeka siku moja zaidi na kuwa siku 14. Itakapofika Juni 2245, zitaadhimisha Krismasi Januari 9.

Sasa tuone jiografia tunapokaribia Desemba 25. Dunia inapolizunguka jua huleta solistasi na ikwinoksi. Ikwinoksi ni usiku na mchana kulingana. Solistasi ni mchana au usiku kuwa mrefu zaidi. 

Ulaya waliona solistasi ikitokea Juni 25 na Desemba 25 wakati ikwinoksi ilitokea Machi 25 na Septemba 25.

Desemba ni baada ya mavuno, hivyo sherehe, michezo, vinywaji, likizo ndiyo wakati wake. Roma wamesherehekea namna hiyo tangu miaka 500 kabla ya Yesu kuzaliwa. Sherehe zilizoitwa Saturnalia zilifanyika Desemba 17 hadi Desemba 23.

Solistasi ya  Desemba 25 ilileta usiku mrefu na hata jua kupotea wiki kadhaa na jua huanza kurudi kaskazini. Ipo dini iliyoitwa Mithra iliamini tukio hilo ni kuzaliwa Mungu wa Jua anayelirudisha angani, kwa Kilatini akaitwa Sol Invictus.

Hivyo ratiba ya Desemba ilienda hivi. Sherehe za Saturnalia zilianza Desemba 17 zikaisha Desemba 23. Ilipofika Desemba 25 ikawa ni Krismasi tangu mwaka 204. 

Hivyo, Krismasi ilivyokuja ilikuta siku ya Desemba 25 haina sikukuu wala shamrashamra yoyote. Kimsingi watu walikuwa wako katika siku ya pili ya mapumziko baada ya sherehe za Saturnalia kumalizika.

Kadiri Krismasi ilivyozidi kushamiri ndipo serikali ya Roma ikashituka na mwaka 274  ikaamua kuitangaza Desemba 25 iwe sikukuu ya kitaifa ya Sol Invictus. Serikali ilitarajia Krismasi ipoteze umaarufu maana sasa taifa zima litalazimika kusherehekea Sol Invictus.

Mwaka 336 serikali ya Roma iliitangaza Krismasi kuwa sikukuu ya taifa. Hii maana yake serikali iliitangaza wakati Wakatoliki walikwisha kuisherehekea kwa zaidi ya miaka 132 tangu mwaka 204.

Hivyo Kanisa Katoliki halikugeuza sherehe za kipagani iwe Krismasi. Kinyume chake siku ya kipagani (Sol Invictus) iliyotangazwa mwaka 274 ndiyo imeikuta Krismasi tayari ipo tangu mwaka 204 kama tulivyoona.

Kimahesabu hiyo sikukuu ya kipagani (Sol Invictus) imekuta Wakatoliki wanaisherehekea kwa zaidi ya miaka 70.

Hadi hapa tumeshajua mambo mawili. Jambo la kwanza ni kwamba kumbe tarehe za Krismasi ziko tatu ingawa inayojulikana na wegi ni moja tu, yaani Desemba 25, kumbe zipo pia Januari 6 na Januari 7.

Jambo la pili ni kwamba makala hii inakuonyesha kwamba mtu wa kwanza kuifanya Desemba 25 iwe ni Krismasi alikuwa ni Mtakatifu Hippolytus na alifanya hivyo mwaka 204.

Sasa mbona huyu Hippolytus hajulikani wala hatajwi sana? Sababu ya kwanza ni kwamba lugha aliyotumia Hippolytus kuyaandika hayo ilikuwa ni Kigiriki wakati Roma walitumia zaidi Kilatini.

Matokeo yake wasomi walioandika kwa Kigiriki kama yeye, walijikuta maandiko yao hayasomwi na wengi kwa karne nyingi.

Sababu ya pili ni kwamba historia ya Mtakatifu Hippolytus inaonyesha kuwa aligombana na kuchukiwa sana na wenzake kanisani. Hivyo wengi kanisani hawakumpenda, hivyo hawakujisumbua kusoma maandishi yake.

Pamoja na yote hayo, ukweli unabaki kwamba Mtakatifu Hippolytus ndiye aliyefanya hesabu zilizoipata Desemba 25 kuwa sikukuu ya Krismasi.

Natumaini umeelewa jinsi tarehe ya Krismasi, yaani Desemba 25 ilivyopatikana. Nawatakia Krismasi njema na heri ya mwaka mpya.

MUHIMU

Makala hii imeandikwa na Joseph Magata na kuchapwa kwa mara ya kwanza Desemba 2019 katika Gazeti la RAIA MWEMA. Mwandishi huyu anapatikana kupitia 0754 710 684 na  [email protected]