Mara nyingi ninapochambua masuala haya ya Biashara na Uchumi huwa ninakwama kupata maneno yaliyozoeleka katika Kiswahili ili kuelezea dhana fulani fulani. Hii haimaanishi kuwa Kiswahili hakina maneno hayo, la hasha! Isipokuwa kutumia maneno hayo kunaweza kuwapoteza wengi na kutoeleweka kirahisi.
Leo ninataka kuongelea uhakika wa maisha ya kesho ya mjasiriamali. Moja ya neno nitakalolitumia sana ni “hatari” ambalo kwa Kiingereza wanaita “risk”. “Risk’ ni kitendo ama utayari wa mjasiriamali kukubaliana na kuwa tayari kwa lolote baya linaloweza kutokea kabla, wakati na baada ya biashara anayoifanya.
Kwa mfano unapoanzisha duka upo uwezekano likaibwa ama kuungua, unaponunua gari la biashara upo uwezekano likaanguka ama kugonga watu, unapokopa mkopo benki unaweza kupatwa na bahati mbaya ukajikuta biashara uliyobuni haiendi na mkopo umeshindwa kurejesha; hivyo ukafilisiwa dhamana zako.
Vile vile unaweza kulima shamba la mahindi ya biashara halafu mvua zikagoma kunyesha. Pamoja na hatari hizi zote zilizopo mbele ya mjasiriamali na ambazo zinaweza kumpata; inapotokea mjasiriamali akaamua kuendelea kulifanya alilokusudia kufanya; huku ndiko tunaita kuchukua ‘risks’
Katika sayansi ya biashara tunashauri kuwa badala ya kuchukua ilimradi ‘risk’, ni vema mjasiriamali ukajihusisha na ‘risks’ ambazo zimekokotolewa (calculated risks). Hii inamaanisha angalau ujue ukomo wa lolote baya linaloweza kukupata wakati wa biashara hiyo na ujipange na mibadala ya kujiokoa (repair alternatives).
Kadiri unavyojihusisha na ‘risks’ kubwa ndivyo unavyojiongezea uwezekano wa kufaulu kwa kiwango kikubwa. Namna unavyoziona ‘risks’ unavyozipangia mbinu na kucheza nazo kwa kuzipunguza ama kuzifuta ndivyo unavyoongeza uhakika wa kufanikiwa katika biashara husika.
Kiukweli ujasiriamali unahitaji mtu kuwa na roho ya paka (roho ngumu na ya uvumilivu mkubwa). Leo kupata faida na kesho hasara ama kufilisika kabisa ni mambo ya kawaida sana. Wajasiriamali wengi tuna tatizo katika utunzaji na ukuzaji wa mitaji.
Yaani, mitaji inapanda na kushuka. Mtu unaweza kufanya biashara na kufikisha pengine mtaji wa milioni ishirini lakini baada ya muda fulani unashangaa mtaji unasoma milioni kumi. Inakuwa kama mchezo wa kubahatisha (kupata ama kukosa)
Wakati mwingine wajasiriamali tunaishi maisha ya misongo mikubwa kimawazo kutokana na mambo kwenda ndivyo sivyo. Unaweza kuchukua mkopo benki halafu biashara ulizotegemea zikakataa. Ikiwa uliwekea dhamana ya nyumba ama rasilimali nyingine lazima jasho lianze kukutoka. Ama wakati mwingine unaweza kufanikisha kulipa mkopo lakini ukajikuta mtaji haujaongezeka na pengine umeshuka; inakuwa kama ulikuwa unawafanyia kazi benki!
Uzoefu unaonesha kuwa usipokuwa makini katika ufanyaji wa ujasiriamali, unaweza kushindwa hata kumudu ndoa yako (kwa wale waliooa ama kuolewa). Kufanikiwa kibiashara inatakiwa kuendane na furaha katika familia na ustawi wa afya ya mwili wako. Unatakiwa kuwa na fedha ya kutosha pamoja na muda wa kutosha kupumzika ama kukaa na familia yako.
Kinachosikitisha ni kuwa wajasiriamali wengi wanakuwa na fedha (hata kama si nyingi za kutosha), lakini hawana muda wa kufurahi na familia wala ndoa zao. Hata wanapokuwa katika nyumba zao akili zao haziwi na wake zao, haziwi na watoto wao, zipo kwenye ujasiriamali ama zinawaza marejesho ya mikopo! Wajasiriamali wengi hawajui ni lini hasa watakuwa na furaha za kudumu. Kuwa na furaha katika maisha yao ni kama bahati nasibu!
Kupanda na kushuka kimafanikio, kuishi na vidonda vya tumbo ama presha kunakotokana na mawazo; pamoja na migogoro ya kifamilia sio stahili ya mjasiriamali na katu haifai kuwa hivyo. Pamoja na hayo, mazingira ya ujasiriamali tuliouzoea Tanzania yanatupelekea kuwa katika hali hizi, Je, tunajikwamuaje hapa?
Katika hili ninakumbuka habari ya rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa akifanya biashara ya nyanya, akizitoa Ilula-Iringa na kuzipeleka Dar es Salaam. Kila anapokuwa njiani (kwenye gari lililopakia hizo nyanya) alikuwa akitembea na miwani myeusi. Hebu nifuatilie kiumakini ujue kazi ya hiyo miwani myeusi.
Kikawaida nyanya hutakiwa kuingia Kariakoo kabla ya saa kumi na moja za alfajiri, ndipo biashara inafanyika, kinyume na hapo mzigo hudoda na kumwagwa. Inapotokea gari likaharibika njiani kwa muda mrefu, halafu iwe ni maeneo ya kuanzia Morogoro kwenye joto, utashuhudia kwa macho yako nyanya zikiiva na kuanza kuoza.
Hivyo inapotokea gari limeharibika yeye (rafiki yangu) hutia miwani myeusi machoni mwake. Unajua nini kinatokea? Ni kwamba, anapovaa miwani myeusi akitazama kwenye makasha yaliyowekwa hizo nyanya anaona kuwa nyanya bado ni za kijani (hazijaiva wala kuoza)! Hivyo alikuwa anajifariji kwa kujidanganya. Macho yake kupitia miwani myeusi yanaona nyanya hazijaoza lakini ukweli ni kuwa nyanya zimeshaoza!
Kwa maelezo yake hili lilikuwa linamwondolea presha! Kwa hiyo kuna wakati gari lilikuwa linaingia Kariakoo kwa kuchelewa na kujikuta anamwaga mzigo wote au wakati mwingine nyanya zinamwagwa njiani (kwa kuwa zinakuwa zimeshaoza) lakini yeye ‘anakomaa’ na miwani myeusi machoni akiamini nyanya zake hazikuoza!
Ili kuepuakana na hali kama hizi za ujasiriamali kuwa kama mchezo wa kubahatisha kuna mtindo wa ufanyaji wa biashara ambao wajasiriamali tunatakiwa kuuzoelea. Mtindo huu ni kuwekeza katika aina tofauti za biashara kwa wakati mmoja. Kwa kitaalamu mtindo huu tunauita ‘diversification’ ambapo zile biashara mbalimbali unakowekeza zinaitwa ‘portofolio’. Kufanya ‘diversification’ kunaondoa kubahatisha katika kupata faida kunapunguza msongo wa mawazo na kunakupa furaha ya ujasiriamali muda wote.
Kwa mfano, badala ya kuhangaika na biashara ya mbao pekee, ambayo ina mtindo wa kupanda na kushuka (kutegemea na msimu), ni vema mjasiriamali ukawekeza katika biashara zingine kama, majengo, usafirishaji na nyingine unazoweza kuzimudu. Kanuni itakayokusaidia katika ‘diversification’ ni kuhakikisha biashara unazowekeza zisiwe na kufanana ama kutegemeana.
Ipo hivi, ukiwa ni mfanyabiashara wa mazao, ‘diversification’ haitakuwa na tija kubwa kama utawekeza katika usafirishaji kwa kununua lori. Shida itakuwa ni moja, biashara zako zote mbili (ya mazao na usafirishaji) zitakuwa ni za msimu; msimu wa mazao ukiisha na biashara ya usafirishaji itasimama. (ikiwa lori hilo hukodishwa kusafirisha mazao)
Ndio maana ninasema katika kufanya hiki ninachokiita, ‘diversification’ mjasiriamali unatakiwa kutafuta biashara ambazo angalau moja inapoenda vibaya basi nyingine iwe inazalisha faida. Ukianza na kujizoesha kufanya, ‘diversification’ haimaanishi kuwa hautapita katika changamoto za kuyumba, lakini nakuthibitishia kuwa hautakuwa mtu wa kuyumba kiasi cha kufika sifuri.
Najua kuwa kuna watu watawaza mioyoni mwao mambo mengi kuhusu hii ‘diversification’. Unaweza kuniuliza, “Nitafanyaje biashara zaidi ya moja na mtaji unanikaba?” ama pengine unaweza kujisemea, “Biashara zaidi ya moja nitasimamiaje?” Kuhusu la usimamizi nitalieleza katika makala zijazo, lakini hili la mtaji ni rahisi.
Usisubiri kuwa na mtaji mkubwa ili ufanye ‘diversification’. Pale ulipo angalia ni biashara aina gani tofauti unaweza kuzifanya kwa wakati mmoja? Kwa mfano, unaweza kuwa na mgahawa wenye mtaji wa laki tatu halafu ukawa na saluni yenye mtaji wa laki tano, tayari hii ni ‘diversification’. Hii ni bora kuliko kupuuza na kujikuta unakuwa mjasiriamali wa kuyumba yumba katika biashara moja uliyoing’ang’ania.
Hata katika mambo ya mikopo, huwa inakuwa rahisi kwa mjasiriamali kurejesha mkopo kwa wakati ikiwa una biashara zaidi ya moja (za aina tofauti). Kuna wakati itatokea, biashara uliyochukulia mkopo ikagoma, lakini ukaweza kurejesha mkopo kupitia biashara nyingine. Lakini ukiacha hilo, mjasiriamali unakuwa na maisha yasiyo na mawazo ya kuumiza na unakuwa na uhakika kwa yale unayoyafanya. (Huhitaji kutembea na miwani myeusi!)
Tatizo la wajasiriamali wengi ni ubishi wa kung’ang’ania biashara moja miaka nenda rudi pamoja na kuigana. Biashara iliyokufaidisha jana sio lazima ikupe faida leo. Biashara inayompa faida mwenzio haimaanishi ukianzisha na wewe utapata faida. Mazingira yanabadilika, ushindani unaongezeka, hivyo ni lazima kukabili changamoto mpya na kuwa tayari kujaribu biashara mpya. Hili litasaidia sana mjasiriamali kuwa na uhakika kwa biashara zako na kuepuka maisha ya kubahatisha kiujasiriamali!
Kila mjasiriamali anastahili ushindi.