Unaweza kuwa na macho mawili bila maono. Unaweza kuwa na macho mawili yanayotazama lakini bila jicho la tatu linaloona: jicho la akili, jicho la moyo na jicho la imani. Kipindi cha siku 40 cha kufunga ni kipindi cha kufanya toba dhidi ya makosa ya kutoona.

Dharau ni kosa la kutoona thamani ya kitu au mtu. Majivuno ni kosa la kutoona saizi yako. Mazoea mabaya ni kosa la kutoona thamani ya kitu au mtu. Mazoea huzaa dharau. Ushirikina ni kutoona uwepo wa Mungu na nguvu ya Mungu kwa jicho la imani. Kutoshukuru au shukrani ya punda ni kosa la kutoona mazuri uliyofanyiwa. Mtazamo hasi ni kosa la kutoona mazuri, mema na neema.

Penye miti hakuna wajenzi. Watu wanaona miti lakini hawaoni milango, kabati, dawati, meza, viti vinavyoweza kutokana na miti hiyo.

“Jambo moja baya sana kuliko kuwa na upofu ni kuwa na macho bila kuwa na maono,” alisema Helen Keller aliyekuwa na upofu wa macho na uziwi wa masikio.  Yeye alikuwa na jicho la tatu linaloona. “Kuwa na macho matatu: mawili kwa ajili ya kutazama na moja kwa ajili ya kuona.” (Bellamor). Watazame watu na uwaone kwa jicho la tatu.

Bwana wetu Yesu Kristu alimtibu mtu mwenye upofu.  Tunasoma hivi katika Biblia: “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?” Naye akawajibu: “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: ‘Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu.’ Hapo, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.” (Yohana 9: 10).

Kwanza, alimuita Yesu mtu. Alikuwa hajamuona kwa jicho la tatu. Alimuona kama mtu. Lakini kumwona mtu kama mtu unakuwa haujaona vizuri. Ukimwona baba yako kama mtu tu na si kama baba, haujaona vizuri. Ukimwona mama yako kama mtu na si mama, haujaona vizuri. 

Huyu aliyeponyeshwa alimuona vizuri Yesu alimuita baadaye ‘nabii’. Lakini yote yanatagemea unataka kuona nini. “Tunachokiona kimsingi kinategemea tunachokitafuta,” alisema John Lubbock.

Ukiona kwa jicho la tatu, utakuwa mtu wa shukrani. Ukitazama na ukaona vizuri unazungumza kwa shukrani. Mwenye upofu aliyetibiwa na Yesu alikubali kuwa ndiye yule yule aliyekuwa na upofu.

“Macho yake yalivyokuwa yamefunguka yalibadili mwonekano wake: Lakini alisema mimi ndiye. Alisema kwa shukrani; kukataa kungemfanya ahukumiwe kuwa ni mtu wa kutoshukuru,” alisema Mt. Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini.

Baadhi ya watu wanaotazama kwa macho mawili na kutoona kwa jicho la tatu wana tabia ya kudharau. Tunasoma katika Biblia juu ya dharau ya mafarisayo ambao hawakuona kwa jicho la tatu dhidi ya aliyeponywa na kuanza kuinjilisha na kuhubiri.

Wao wakamjibu: “Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?” (Yohane 9: 34). Wenye dharau watakukumbusha historia yako mbaya ambayo ulishasamehewa na Mungu.  Watakukumbusha mambo yako ya zamani kabla ya kuwa Mkristu. Watakucheka. Lakini kumbuka Mungu anawacheka wao. “Mwenyezi Mungu atawalaye juu mbinguni, anawacheka na kuwadhihaki.” (Zaburi 2:4). 

Baadhi ya watu wanaotazama kwa macho mawili na kutoona kwa jicho la tatu wana tabia ya kutukana. Watakuita majina. Huyo mtu akawajibu: “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, nyinyi pia mnataka kuwa wafuasi wake? Lakini wao wakamtukana.” (Yohane 9: 27 -28).

Ukimkiri Yesu, watu watakuita majina ya kukukebehi. Wewe ni Papa. Wewe ni Mtakatifu Petro. Kama unasaidia maskini watakuita ni Teresa wa Calcutta. Watakuita deakoni. Endelea kusaidia.