Na Bashir Yakub
Wako wasimamizi wa mirathi wa aina mbili. Kwanza ni yule ambaye marehemu mwenyewe amemteua kabla ya kufa kwake na akaandika/kusema kwenye wosia kuwa fulani ndiye atakayesimamia mirathi yangu baada ya kuondoka.
Pili, ni yule ambaye hakuteuliwa na marehemu mwenyewe bali ameteuliwa na wanafamilia kwenye kikao cha familia. Kwa walio wengi huyu ndiye tunamjua kuwa ni lazima jina lake lipelekwe mahakamani kwa ajili ya kuthibitishwa ili aweze kuwa msimamizi kamili. Makala itapitia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi, Sura ya 352 na kanuni zake.
1. HAKI NA WAJIBU WA WASIMAMIZI WA MIRATHI
Haki na wajibu wa msimamia mirathi aliyeteuliwa na marehemu kabla ya kifo na ambaye hakuteuliwa na marehemu ni sawa. Awe aliteuliwa na marehemu mwenyewe au aliteuliwa na wanafamilia bado haki na wajibu alionao ni ule ule.
Wajibu mkuu wa msimamia mirathi ni kuwa mwadilifu, na kuenenda kwa mujibu wa sheria katika kila hatua anayopiga katika kusimamia kwake mirathi.
2. SIO LAZIMA MSIMAMIZI WA MIRATHI AWE NDUGU/MWANAFAMILIA
Hili ni muhimu zaidi kulieleza. Siyo kweli kuwa msimamizi wa mirathi lazima awe mtoto wa marehemu, shangazi, baba mdogo au mkubwa, mjomba, kaka, dada n.k. Bali msimamizi wa mirathi anaweza kuwa yeyote. Suala la msingi ni atimize sifa za kuwa msimamizi wa mirathi. Na katika sifa hamna undugu.
Hakuna haja ya kuwa na ugomvi kuwa msimamizi wa mirathi lazima atoke katika familia. Hakuna ulazima huo ikiwa mmeshindwa kuaminiana kwenye familia. Mnaweza kumteua hata kiongozi wa dini au mtu mwingine yeyote mwadilifu ambaye mnadhani ataweza kutenda haki katika usimamizi.
Jambo jingine, msimamizi wa mirathi siyo lazima awe mmoja. Ikiwa kuna pande mbili zinazozana, basi sheria inaruhusu kila upande kutoa msimamizi wa mirathi ili alinde maslahi ya upande wake. Kwa hiyo, wasimamizi watakuwa wawili na sheria haikatazi.
Nyongeza ya hapo ni kuwa hata kampuni au taasisi inaweza kuteuliwa kusimamia mirathi.
3. MSIMAMIZI ALIYETEULIWA KATIKA WOSIA KUTHIBITISHWA NA MAHAKAMA
Msimamizi aliyeteuliwa katika wosia naye ni lazima kuthibitishwa na Mahakama. Siyo kwamba kwa kuwa marehemu kabla ya kufa alimteua au kwa sababu ameandikwa kwenye wosia kama msimamizi wa mirathi, basi haina haja ya kwenda tena mahakamani.
Ni kweli aliteuliwa na marehemu kabla ya kifo, lakini athibitishwe na Mahakama. Hivyo ndivyo sura ya 352 inavyosema
Ikiwa hatathibitishwa na Mahakama, basi hawezi kusimamia mirathi. Lazima awe na fomu ya usimamizi wa mirathi itolewayo na Mahakama.
Fomu hii ndiyo inayoruhusu kuuza mali, inaruhusu kudai madeni, unaweza kuonesha benki na akaunti za marehemu zikafunguliwa ili mchukue hela, inaoneshwa kwenye kampuni kama kuna hisa ili kuweza kupewa hisa za marehemu nk. Huwezi kuonesha wosia ukaruhusiwa kufanya miamala kama hii.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.