Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack amemuapisha Jasinta Venant Mboneko kuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga leo Jumatatu Agosti 6,2018.
Hafla fupi ya kuapishwa kwa mkuu huyo mpya wa wilaya ya Shinyanga imefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali,vyama vya siasa,taasisi na wadau mbalimbali.
Akizungumza baada kula kiapo,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,mheshimiwa Jasinta Venant Mboneko alisema amekuja wilayani humo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
 
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuniamini kuwa na mimi kuwatumikia wananchi wa Shinyanga,nipo tayari kuwatumikia wananchi na nitaendelea kuisimamia ilani ya uchaguzi ya CCM na kuhakikisha tunaifanya wilaya ya Shinyanga kuwa salama”,alisema Mboneko.
 
“Nimekuja Shinyanga kufanya kazi,na tumeelekezwa kuwatumikia wananchi,kazi hii sitaifanya peke yangu,wapo watu wataniwezesha ikiwemo kamati ya ulinzi na usalama lakini pia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ,viongozi wa dini pamoja na wananchi,naomba mwenyezi Mungu anisaidie sana na aniwezeshe”,aliongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alimtaka mkuu huyo wa wilaya na viongozi wengine kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuepuka urafiki katika kazi.
 
“Mwananchi akilalamika msikilize,hakikisha unafanyia kazi kila jambo linalokuja mbele yako,Shinyanga iko salama,naomba tushirikiane kufanya kazi”,alisema Telack.
 
“Najua utapata watu wengi wa kukukaribisha,kuwa makini na watu wanaokukaribisha,hizi kazi zetu hazina urafiki,nikumbushe tu kwamba mishahara mnayopewa na serikali inatosha msikubali kupewa rushwa”,aliongeza.