Mtuhumiwa huyo mkazi wa Ngaramtoni, Arusha, alikamatwa Desemba 5, mwaka huu katika kile kinachoelezwa kuwa ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne wa kukomesha vitendo vya ujangili.

Pamoja naye, mtuhumiwa mwingine, Godfrey Sekito (God Mabita au God Mapesa), mwenye umri wa miaka 36; naye alikamatwa na sasa wanashikiliwa na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujangili chenye makao makuu yake Mikocheni, Dar es Salaam.

Wakati Ojungu alikamatiwa Mianzini, Sekito alikamatwa katika eneo la Sakina kwa Iddy jijini Arusha. Ojungu alikamatwa akiwa amevaa fulana yenye maandishi ya: ‘Money Talk’, yakinaamisha ‘Pesa Inazungumza’.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumeelezwa kuwa ni matokeo ya pamoja kati ya Kikosi Kazi cha Kanda cha Kupambana na Ujangili na askari wa Kikosi Kazi kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Ojungu anatajwa kuwa ni mtuhumiwa mkuu wa ujangili katika Hifadhi za Taifa za Serengeti (SENAPA), Tarangire, Manyara na katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mara kadhaa amekuwa akitiwa mbaroni na kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha. Mwaka 2013 alikamatwa na kuachiwa na tangu wakati huo amekuwa akiishi kwa kujificha.

Kukamatwa kwake ni matokeo ya kazi ya Kikosi Kazi cha Kupambana na Ujangili kinachoundwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha zinasema kukamatwa kwa Ojungu kumesaidia Kikosi hicho kuutambua mtandao wa ujangili. Hadi mwishoni mwa wiki, mtuhumiwa huyo alikuwa akiendelea kuhojiwa. 

Ojungu anatajwa kuwa mmoja wa vijana wenye utajiri mkubwa katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

“Frank (Ojungu) huyu ni papa. Amekuwa akikamatwa mara kwa mara na kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha; alikamatwa wakati wa Operesheni Tokomeza lakini akaachiwa.

“Mwaka juzi alikamatwa akiwa mafichoni katika nyumba eneo la Sakina mjini Arusha. Amekuwa akisakwa kwa muda mrefu. Mara ya mwisho aliponea chupuchupu kukamatwa wakati askari wa Kikosi Kazi walipokuwa wakifukuza gari la mmoja wa mabalozi wa nje waliopo hapa nchini ambalo lilikuwa na nyara za Serikali. Ojungu na mwenzake walifanikiwa kutoroka baada ya ajali,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa kutoka kwa maofisa wanaomhoji mtuhumiwa huyo zinasema wamefanikiwa kupata taarifa za “kustaajabisha” ambazo zinawahusisha kwenye ujangili wa tembo na faru baadhi ya wanasiasa nguli, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na wanasiasa kadhaa. JAMHURI imepata majina ya watuhumiwa hayo, lakini kwa sababu za kitaaluma, inayahifadhi kwa sasa. 

Mmoja wa maofisa wa Kikosi Kazi kutoka Dar es Salaam walioshiriki operesheni ya kumkamata Ojungu amesema mtuhumiwa huyo ndiye mwezeshaji mkuu wa majangili katika Kanda ya Kaskazini.

“Frank ndiye papa, ana bunduki nyingi lakini tulipomkamata tumefanikiwa kupata bunduki aina ya Rifle 375. Amekuwa akijihusisha na mauaji ya wanyamapori na usafirishaji nyara katika maeneo yote ya Afrika Mashariki, China na kwingineko duniani.

“Tulimkamata katika eneo la Mianzini. Muda wote ni mtu anayejihami, tulipokaribia alijaribu kukimbia kwa kutumia bodaboda akielekea Namanga, lakini tukafanikiwa kumtia mbaroni. Ana pesa nyingi sana. Ana pikipiki zaidi ya 300 Arusha, ana nyumba na magari mengi. Anajihusisha na biashara ya tanzanite kule Mirereni, ana depot za bia. God anatumiwa na Frank,” kimesema chanzo chetu. 

Mpaka wa Namanga unatajwa kama mlango mkuu wa mtandao wa Ojungu wa kutorosha nyara za Serikali kwenda Nairobi, Kenya na Kampala nchini Uganda.

Katika mahojiano na Polisi, imebainika kuwa Ojungu anamiliki bunduki nyingi ambazo amekuwa akiwakodisha walio kwenye mtandao wa ujangili kwa ajili ya kuua ndovu, faru na wanyamapori wengine.

“Ana mtandao na maaofisa wa juu kabisa wa Jeshi la Polisi, wengine wamo jeshini hadi sasa, na wengine ni wastaafu; kuna wanasiasa huwezi kuamini, kuna wafanyabiashara wa ngazi za juu hata wanajeshi kadhaa.

“Ojungu alikuwa Kenya, huko amekuwa akishirikiana na majangili wenye asili ya Kisomali, alipokimbizwa akarejea Arusha. Akajificha kwa sababu anajua amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Amekiri kuwa ujangili aliuanza miaka ya 2000. Anasema amepata fedha nyingi zilizomwezesha hata kumiliki migodi ya tanzanite huko Mererani,” kimesema chanzo chetu.

Mwaka juzi mtuhumiwa huyo alieleza mbinu anazotumia kushinda kesi au kupewa adhabu ndogo katika Mahakama.

“Anasema fedha anazo, washirika wake wanapokamatwa wanawahonga baadhi ya wanasheria na mahakimu, wanaachiwa. Ametoa mifano hadi tukabaki midomo wazi. Anasema sehemu nyingine wanakuwa na nyara, wakifika kwenye vizuizi wanatoa shilingi milioni moja au chini ya hapo na kuachiwa. Tena anasema kwa kujiamini kabisa kwamba polisi ndiyo wepesi zaidi,” kimesema chanzo chetu.

Kwa juzi, Jeshi la Polisi lilimwondoa mmoja wa mapolisi waliokuwa wakishiriki kwenye Kikosi Kazi mwenye cheo cha inspekta. 

“Alikuwa anayumbisha Kikosi, mara zote tulishindwa kujua ni nani anayetoa siri kwenye mtandao hadi tushindwe kuwanasa. Tumefanikiwa kumjua, ameondolewa na kurejeshwa Makao Mkuu, Dar es Salaam,” kilidokeza chanzo chetu.

 

Ujangili dhidi ya tembo

Kamati ya Kudumu ya Bunge imewahi kusema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa. 

“Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).

“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.

“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo,” ilionya Kamati.

Kamati hiyo iliongeza kusema: “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo. Kinachosikitisha ni kwamba wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne) iliyoitaka wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa wizara ambao wamepuuza kauli ya Mheshimiwa Rais.”

Kamati ilishauri Serikali kuendesha Operesheni Uhai kwa nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia ikapendekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali kwa watu wote watakaothibitika kujihusisha na ujangili.