Dar es Salaam

Na Christopher Msekena

Omoyo ni miongoni mwa kadhaa nchini ambazo tangu kuwekwa kwake hadharani hazijawahi kuchuja. 

Wimbo huo uliotoka zaidi ya miaka 10 iliyopita umeendelea kuwa burudani na baraka kwa mamilioni ya watu kwenye maeneo ya starehe, sherehe na nyumba za ibada.

Mwimbaji wa wimbo huo, Jane Misso, amerudi kwa kasi kwenye chati za muziki Afrika Mashariki akiwa na ‘remix’ ya Omoyo akimshirikisha msanii wa Bongo Fleva, Harmonize.

Tayari Harmonize ametangaza kuwa licha ya kugharamia gharama za audio na video ya wimbo Omoyo Remix, hatachukua chochote kwenye mapato ya wimbo huo ili kumuenzi Jane Misso na akina mama wote wanaomtumikia Mungu.

Gazeti hili limekutana na mwimbaji huyo mkongwe wa nyimbo za Injili na kufanya naye mahojiano yafuatayo kuhusu muziki na ujio wake mpya wa kishindo.

JAMHURI: Ni sababu zipi zilizokufanya uwe kimya kwa muda mrefu?

JANE: Nilikuwa kimya kwa sababu nilikuwa najiandaa. Kama unavyojua muziki wetu si kama muziki mwingine, ni lazima ukae utulie na Mungu ili upate ujumbe wa kutoa kwa watu.

JAMHURI: Unadhani kwa nini wimbo Omoyo umeendelea kufanya vizuri tangu ulipoutoa miaka 10 iliyopita?

JANE: Kwa kweli ni neema tu ya Mungu, ni wimbo ambao unazungumza na mioyo ya watu, unaonekana una ujumbe mzito sana ingawa kuna watu walikuwa hawaelewi kwa sababu niliimba kilugha, ila nadhani wamefafanunuliwa kwenye hii ‘remix’.

JAMHURI: Kolabo yako na Harmonize imefanya nini kwenye maisha yako ya muziki?

JANE: Kwa kusema ukweli imenirudisha kwenye ramani, pia imefanya nione kwamba nathaminika na ninapendwa. Sikutegemea kabisa kama kuna watu wananiwazia mema, nilijua nimemaliza kufanya kazi yangu na watu wanaburudika kwenye klabu, baa na makanisani, kumbe kuna watu wananitazama kwa namna tofauti, imenitia moyo na nimekuja na mtazamo mpya kabisa wa kufanya kazi kwa bidii.

JAMHURI: Kwa nini ilikuwa rahisi kukubali kufanya kazi na Harmonize?

JANE: Kwa sababu alikuja moja kwa moja kwangu akiwa na malengo yake na nia ya kutaka kufanya huu wimbo. Akasema wimbo Omoyo anaupenda sana na kuupenda tu haitoshi, hivyo anaomba auenzi wimbo huu kwenye miaka zaidi ya 10 ili awe sehemu yake, niliona ni ‘surprise’ kubwa, nilimuelewa vizuri sana.

JAMHURI: Kushirikiana na msanii wa Bongo Fleva hakujakuletea shida katika imani yako?

JANE: Haijaniletea shida, sema tu watu hawakutegemea. Ila nataka niwaambie hiyo ndio kazi iliyomleta Yesu duniani, kuwasogeza karibu watu walio mbali na Mungu. Kwa hiyo mimi kufanya kazi na Harmonize ni kumwonyesha kuwa Mungu anampenda na Harmonize ni mtoto wa Mungu, watu wengi wameupokea vizuri wimbo nashukuru.

JAMHURI: Kwa jinsi ulivyofanya kazi na Harmonize, je, ni msanii wa aina gani?

JANE: Harmonize ni kijana mmoja ambaye kwanza ana upeo na ndiyo maana nimesema mwanzoni kwamba aliponiambia tu anataka kurudia wimbo wangu Omoyo nilimuelewa moja kwa moja. Ukiangalia maneno yake, ukimsikiliza anachokwambia unaelewa huyu kijana ufahamu wake upo mbali. Halafu ni kijana mnyenyekevu na kingine kilichonivutia kwake ana bidii ya kufanya kazi, anajituma na ni kijana mwenye mustakabali mwema na akisimamia jambo ni lazima ahakikishe limefika anapotaka liende. Kwa hiyo nikaona nikikamatana nguvu yangu na yake kuna sehemu mimi nitakwenda.

JAMHURI: Mipango yako ni ipi baada ya kuachia ‘Omoyo Remix’?

JANE: Kwenye hii ‘project’ na Harmonize kuna mipango mingi sana. Kabla ya hii nilikuwa nimeandaa nyimbo nyingi zenye ujumbe mzito ambazo zitakuja baadaye.