Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji imempa jina la barabara Mwanamazingira maarufu duniani Mama Jane Goodall kwa mchango wake katika uhifadhi na utunzaji mazingira mkoani Kigoma sambamba na mchango wake wa kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Uzinduzi wa jina hilo la mtaa umefanywa na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ambaye amesema kupewa jina la barabara kwa mwanamazingira huyo kunatokana na mchango wake mkubwa katika kuhifadhi mazingira na kutangaza utalii.
Amesema hifadhi ya Taifa ya Gombe imejulikana duniani kwa kazi kubwa aliyofanya katika suala la uhifadhi wa wanyama aina ya sokwe mtu katika hifadhi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Baraka Lupoli amesema awali barabara hiyo ilikuwa ikijulikana kama Barabara ya Kibirizi inayoelekea bandari ndogo ya Kibirizi na hifadhi ya Gombe.