Na Mussa Augustine., JamhuriMedia
Jamii imeshauriwa kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili kusaidia watu wenye uhitaji wakiwemo akina mama wajawazito, wagonjwa wa saratani pamoja na wagonjwa mbalimbali waliolazwa hospitali.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam April 30,2023 na Dkt Samwel Mduma kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika zoezi la uchangiaji wa damu na upimaji wa afya lililofanyika katika kanisa la Universal la Ufalme wa Mungu lililopo Keko, Chang’ombe Manispaa ya Temeke.
Dkt Mduma amesema kwamba bado kuna uhitaji mkubwa wa damu kwa wahitaji wa damu Mahospitalini hivyo ni vyema kwa jamii kutilia maanani kampeni za uchangiaji damu wa hiari kwani unasaidia kuokoa maisha ya watanzania wanaosumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Universal la Ufalme wa Mungu,Bishop Gilson Costa amesema kwamba zoezi la uchangiaji wa damu kanisani hapo limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuisaidia jamii inayosumbuka na matatizo ya kupungukiwa na damu nakuhatarisha maisha kutokana na kupoteza damu nyingi.
Aidha amesema kwamba Kanisa hilo litaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhamasisha waumini na wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya jamii na nguvu kazi ya Taifa.
Halikadhalika Mchungaji wa kanisa hilo Makao Makuu, Mchungaji Makange John Kitua amesema kwamba wameandaa shughuli hiyo kuonyesha waumini wao kwamba afya ni muhimu zaidi kwani kanisani siyo Sehemu ya kupata huduma za kiroho pekee,bali pia huduma nyingine zikiwemo za kiafya.
Naye Mratibu Mkuu wa kampeni hiyo ya uchangiaji damu, Dkt Joel Temba ametoa wito kwa madhehebu mengine ya dini na kiroho kuongeza hamasa kwa jamii ili ijitokeze kuchangia damu kwa hiari.
“Leo tunatarajia kukusanya chupa 200 za damu hivyo napenda kutumia fursa hii kuiasa jamii iwe na hamasa ya kuchangia damu kwa hiari na tunataka kuufanya mkoa wa Dar es salaam Kuwa Mkoa wa kimkakati katika suala la Uchangiaji wa damu kwani hospitali kubwa kama Muhimbili, pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean road zipo hapa Dar es salaam”amesema Dkt Temba
Baadhi ya Wananchi na Waumini wa Kanisa hilo waliojitokeza kuchangia damu na kupima afya zao akiwemo James Joshua Mkazi wa Mbagala ,Bi Edda Malamsha aliyeongozana na mumewe Josephat Malamsha kutoka Ukonga wamesema kwa nyakati tofauti kuwa utamaduni wa kuchangia damu ni muhimu kwani unasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.