Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Bagamoyo
SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Hamis Mtupa ametoa rai kwa watu wanaodhulumu mali za yatima ili kujinufaisha na kuwaacha watoto hao wakitangatanga ,waache dhuluma hiyo kwani ni sawa na kula moto utakaowachoma kesho kiama.
Aidha ameitaka jamii kuwapa Upendo na haki zao ambazo huwa zimeachwa kwa ajili yao badala ya kuwadhulumu .
Mtupa alitoa rai hiyo, Wilayani Bagamoyo wakati wa dhifa kwa ajili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, wajane na wazee iliyoandaliwa na Taasisi ya (SHAKIBA) Islamic Foundation ya Bagamoyo.
Alieleza ,baadhi ya watu wamekuwa wakiwanyanyasa na kudhulumu mali za wazazi wao na kuzitumia huku watoto hao wakiwa hawaruhusiwi kuzitumia.
“Watu wanaokula au kujinufaisha na yatima ni sawa na kula moto sawa na kaa la moto kulitia tumboni hivyo moto huo utawachoma na kila watakalolifanya halitafanikiwa,”alisema Mtupa.
Aidha alifafanua ,mtu anayekula mali ya yatima anamkanusha Mungu siku ya malipo atalipia dhuluma aliyoifanya kwa yatima hao ambao wanahitaji kusaidiwa.
“Tunapaswa kuwafadhi watoto yatima badala ya kuwatesa ili tupate thawabu wawekeni kwenye sehemu yao kwani ukimtunza kumpa faraja na kumlea utajiwekea mahala pema peponi,”alisema Mtupa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa SHAKIBA Alhaj Abdul Sharifu alisema kuwa taasisi hiyo ina lengo la kusaidia watu mbalimbali wenye mahitaji wakiwemo wajane, yatima na wazee.
Sharifu alisema kuwa tayari wameanzisha kituo cha kulea yatima ambapo 124 anawalea huku 24 akiwa anawsomesha wakiwa madarasa mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Firdaus Centre Kituo cha Kulea Yatima cha Kongowe Kipala Mpakani Dk Sheikh Sharifu Firdaus alisema kuwa hakuna jambo baya kama kufiwa na wazazi.
Dk Sheikh Firdaus alisema kuwa watoto yatima wanapata tabu sana na wanachangamoto nyingi sana wanazokutana nazo hivyo wanahitaji misaada mbalimbali.
Kwa upande wake mwenyekiti idara ya wanawake Jamila Suleiman alisema kuwa wanawake wanahitaji kusaidiwa na waume zao na siyo kuwapa mizigo wanawake.
Suleiman alisema kuwa wao wanapigania haki za wanawake ambapo dini haitaki wanawake wanyimwe haki zao ambapo vipigo huondoa upendo na kusababisha visasi na majadiliano ni suluhu ya ugomvi.
Mratibu wa SHAKIBA Taifa Dk Fakhad Mtonga alisema kuwa lengo la kuanzishwa ni kusaidia jamii kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya afya, elimu, kilimo, uvuvi na elimu ya dini.
Dk Mtonga alisema kuwa pia wamekuwa wakitoa elimu ya kukabili vitendo vya ukatili na ukatili wa jinsia, kujitambua na kukabili vitendo viovu na wanatarajia kuanzisha kituo cha afya ambapo wasiojiweza waratibiwa bure na watu wengine watalipia gharama za matibabu kwa bei nafuu kilianzishwa 2020.