Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), imemng’oa katika madaraka Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Said Amir, na kuwasimamisha kazi maofisa wengine watatu waandamizi ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi zinazowakabili.

Kwa wiki kadhaa, JAMHURI imeandika kwa kina taarifa za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi uliopindukia kwenye matumizi ya fedha za kampuni hiyo ya umma.


Miongoni mwa mikataba hiyo ni ule wa Sh milioni zaidi ya 700 ambao uongozi wa TTCL, chini ya Amir uingia na kampuni ya ulinzi ya Supreme ilhali ikiwa haina walinzi wa kutosha, upungufu wa silaha na walinzi kadhaa wenye sifa za wizi ambao wana kesi polisi.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Enos Bukuku; nafasi ya Amir imechukuliwa na Dk Kamugisha Kazaura. Mabadiliko hayo yameanza rasmi Februari mosi, mwaka huu.


Miongoni mwa waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Fedha, Mrisho Shabani; Mkurugenzi wa Biashara na Masoko, Ernest Nangi; na Mkaguzi wa Hesabu za Ndani, Godfrey Kilenga.


Pamoja na Dk. Kazaura, wengine walioteuliwa kukaimu nafasi mbalimbali ni  Alinanuswe Mwakitalima (Kaimu Mkurugenzi wa Fedha);, Peter Ngota (Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Masoko); David Kalayi (Kaimu Mkaguzi wa Hesabu za Ndani), Jotham Lujara (Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi); na Mkurugenzi anayesimamia Mkongo wa Taifa, Adin Mgendi.


Bodi imewataka wafanyakazi wawape ushirikiano viongozi hao wapya.