Wizara ya Maliasili na Utalii imewatia mbaroni watuhumiwa wa ujangili katika Kijiji cha Mkata, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na juhudi zilizofanywa na JAMHURI za kuanika mtandao wa ujangili katika Kijijin hicho na maeneo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.


Mmoja wa waliokamatwa amejitambulisha kwa JAMHURI kuwa ni Mangi, au Mrosso Anthony, lakini namba yake ya simu imesajiliwa kwa jina la Christian Joseph. Namba yake ni simu ni 0655093795.


Habari za uhakika kutoka Morogoro zinasema mtuhumiwa huyo amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Dar es Salaam.


“Tumemkamata, rekodi zetu zinaonyesha kuwa mtu huyu tulikuwa tukimsaka kwa muda mrefu. Amekamatwa akiwa na nyamapori mbalimbali,” kimesema chanzo chetu.


Uuzaji nyamapori katika eneo hilo umekuwa ukifanywa kwa muda mrefu, ingawa baadhi ya viongozi wamekuwa wakijitetea kwa kudai kuwa nyama inayouzwa hapo ni ya ng’ombe na mbuzi.


Hata hivyo, JAMHURI iliweza kufika eneo hilo na kununua nyama ya pofu. Wataalamu wanyamapori walithibitisha kuwa nyama iliyonunuliwa ilikuwa ya pofu.


Kwa kawaida swala wadogo huuzwa Sh 75,000; ilhali wale wakubwa bai yake hufikia Sh 120,000. Mguu wa pofu unauzwa Sh 120,000.


Ujangili umeshamiri nchini, hali inayotishia uhai wa wanyapori katika mapori ya akiba, tengefu na Hifadhi za Taifa.