Ujasiri huu wa ‘Wasukuma’ utufumbue macho Watanzania
Diwani wa Kisesa, Clement Mabina, ameuawa. Waliomuua ni wananchi, pengine wakiwamo wapigakura wake. Tumeziona picha zikimwonesha Mabina akiwa amepasuliwa kichwa na mwili wake ukiwa ndani ya dimbwi la damu na kando yake kukiwa na mawe makubwa. Waliomuua walifanya hivyo kana kwamba wanamuua mnyama hatari aliyeingia kwenye himaya ya binadamu! Ni jambo la kusikitisha.
Haya ya Kisesa yamepata nafasi kwenye vyombo vya habari kwa sababu wengi wanamjua Mabina alikuwa nani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikalini na katika jamii kwa jumla. Wengi yamewafika kama yaliyomfika Mabina. Yamewafika kwa aina inayofanana ya kuuawa na pengine kwa aina inayofanana ya chanzo cha mauaji. Tunaambiwa kuwa chanzo cha haya ya Kisesa ni mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na diwani huyo.
Mara ya mwisho Mabina nilimpiga picha Mei 25, 2009 alipokuwa akinyanyua mkono wa Lolensia Bukwimba, katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita baada ya Msimamizi wa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Busanda, Dani Mollel, kumtangaza mwanamama huyo kuwa mshindi wa kiti cha ubunge. Wakati huo Mabina alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Baada ya kuuawa kwake yamezungumzwa mengi yanayomhusu –mazuri na mabaya. Watuhumiwa kadhaa wamekamatwa juu ya mauaji ya mwanasiasa huyo. Tunaambiwa Mabina naye aliua kabla ya kuuawa. Sijui sheria inasemaje, kwani mtu hawezi kuhukumiwa hata kama keshafariki dunia alimradi kuweka rekodi sawa sawa?
Niliposikia Mabina kauawa kwa sababu ya ugomvi wa ardhi, sikushangaa! Nimerejea maandiko mengi niliyokwishayatoa katika makala zilizopita. Nimekuta kuna makala nyingi ambazo nimeshiriki kwenye kundi kubwa la Watanzania wanaoonya na kutoa hadhari juu ya hatari inayoikabili Tanzania –hatari ya vita itokanayo na ardhi.
Wakati tunapata Uhuru mwaka 1961, nchi hii ilikuwa na watu wasiozidi milioni kenda. Leo, miaka zaidi ya makumi matano, idadi yetu imevuka watu milioni 45. Ardhi ya wakati huo ya Tanganyika imebaki kuwa hiyo hiyo licha ya kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vita inayotokana na ardhi nchini Tanzania si jambo linalohitaji mtu kuwa mpiga ramli au mtaalamu wa utabiri. Ni hatari ambayo mweledi yeyote anaweza kukaa na kuiona bila msaada wa wataalamu.
Vurugu zinazoendelea Malinyi, Kilosa, Kilombero, Rufiji na kwingineko nchini ni kiashiria cha hatari iliyo mbele yetu. Haya yanafanyika wakati kuna Sera inayohimiza Matumizi Bora ya Ardhi, ambayo kimsingi hayawezekani bila kuishirikisha jamii ili wakulima wawe na maeneo yao, wafugaji wawe na maeneo yao na watu wengine wawe na maeneo kwa ajili ya shughuli zao.
Kwa hiyo, kuchelewa kutekeleza Sera ya Matumizi Bora ya Ardhi maana yake ni kuendeleza usugu wa migogoro na maafa kwa Taifa letu. Migogoro inayoendelea katika Pori Tengefu la Loliondo mkoani Arusha ni miongoni mwa matokeo ya kupuuzwa kwa sera hii.
Kutoheshimiwa kwa sera hiyo kumesababisha maafa kati ya wakulima na wafugaji. Wakati fulani watu zaidi ya 20 walipoteza maisha katika mapigano kati ya makundi ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa. Tangu wakati huo mauaji yameendelea huku viongozi wakionekana kukosa ujasiri na utashi wa kumaliza kadhia hii.
Kwenye migogoro mingi chanzo kimekuwa wafugaji wanaowafuata wakulima. Eneo kama la Kilosa, kwa asili wakazi wake ni wakulima, lakini kutokana na haki ya Watanzania kuishi wanakotaka kwenda kuishi, wafugaji wamejikuta wakifika eneo hilo bila kizuizi. Matokeo yake wenyeji ambao ni wakulima wamejikuta kwenye matatizo makubwa ya kuharibiwa mazao.
Wafugaji wamekuwa wakitetewa kwa hoja kuwa wana haki ya kuendesha shughuli zao katika maeneo hayo. Hilo si jambo baya. Kilichotakiwa hapo ni kwa Serikali kuhakikisha inatenga maeneo kwa ajili ya wenyeji wakulima na wageni (wafugaji).
Kufanya hivyo kungesaidia kupunguza na hatimaye kumaliza migogoro ya ardhi. Lakini pengine hiyo si suluhu kwa sababu wafugaji wana makundi makubwa ya mifugo. Wapo wafugaji ambao mmoja anaweza kuwa na ng’ombe 1,000! Dunia ya leo kuwa na ng’ombe 1,000 ambao mapato yake yanazidiwa na mfugaji mwenye ng’ombe 20, ni utumwa. Bado wafugaji wanaamini katika wingi na si ubora na tija ya mifugo michache. Dunia ya leo imeshatoka kwenye wingi.
Nakumbuka wakati fulani Edward Lowassa akiwa Waziri wa Maji na Mifugo, alipambana na maswali alipowataka wanakijiji wafugaji wa Kinyambwiga, Bunda mkoani Mara wapunguze mifugo. Mmoja wa wanakijiji alisimama na kuhoji, “Unasema tupunguze mifugo, mbona sisi hatusemi mpunguze fedha zenu benki? Tukipunguza wewe utasaidia kusomesha na kutibu watoto wetu?”
Hoja ya huyu mwananchi inadhihirisha wazi kuwa bado tuna safari ndefu kweli kweli ya kuwabadili hawa watu, hasa ikizingatiwa kuwa wapo wanasiasa wanaowatetea waendelee na ufugaji wa kutangatanga.
Kwa Mabina tunapata somo jingine tofauti. Somo tunalopata ni kwamba Tanzania, kama ilivyo Afrika, tuna tatizo kubwa la watu — wananchi na wageni — wapora ardhi. Hadi mwaka juzi, hekta milioni 29 za Afrika zilikuwa zimeishia kwenye milki ya wageni kutoka Ulaya pekee. ‘Wapora’ ardhi si raia wa Ulaya, Marekani na Asia pekee, bali kuna Watanzania wengi wenye ukwasi ambao wameamua kujitwalia ardhi kubwa kwa tamaa tu.
Wapo waliojipatia ardhi kwa sababu ya ukwasi wao, lakini wengine ni kwa ghiliba na vitisho. Sitaki kumhukumu, lakini mtu wa kaliba ya Mabina asingekosa jeuri ya kwenda popote anapopataka na akajitwalia ardhi. Anachoweza kufanya ni kupitia viongozi dhaifu wa vijiji.
Hao ndiyo wale wanaoshonewa suti na kupewa pikipiki kama chambo, ili kuwalainisha wawe radhi kuwaondoa wananchi katika maeneo yao na kuwapisha wanaoitaka ardhi. Pale mkoani Manyara, katika Kijiji cha Vilima Vitatu, viongozi mbumbumbu wamelipwa dola 5,000 (Sh milioni 7) na wao wamempatia ‘mwekezaji’.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, ameshawaonya wananchi wa Bagamoyo juu ya uuzaji ardhi. Hadhari ya Kipozi imechelewa kwa sababu sidhani bado kuna uwanja ambao hauna ‘mwekezaji’! Watu wameuza ardhi kana kwamba baada ya wao hakuna kizazi kingine.
Ukitaka kujua ardhi inakwisha, safiri kwa gari. Angaza kushoto na kulia. Kila mahali watu wamejiwekea alama za mipaka ya ardhi waliojitwalia. Hapo ni barabarani — huko ndani ni balaa tu. Maelfu kwa maelfu ya wananchi sasa hawana ardhi. Hawana wigo mpana wa kujishughulisha na kilimo au ufugaji.
Nimepata kuandika kuwa hizi pikipiki zimeingia nchini; si neema, bali ni laana. Vijana wengi wameipa kisogo ardhi. Wamekopeshwa pikipiki na kuzifanya kuwa chanzo kikuu cha mapato. Wanasiasa wanawadanganya vijana wakiwaambia pikipiki zinaweza kubadili maisha yao! Badala ya kutoa mikopo ya trekta na zana za kilimo, wameamua kuwakopesha pikipiki kwa riba kubwa.
Matokeo yake vijana wengi wamejazana mijini. Pikipiki zimewatoa kwenye ‘adhabu’ ya kilimo! Wengi wameishia kuumia kutokana na ajali. Siku vijana wa Tanzania watakapobaini kuwa pikipiki si lolote wala chochote kwa maendeleo yao ya kweli, wataamua kurejea vijijini. Huko watataka waendeshe kilimo maana mahitaji ya chakula yatakuwa makubwa kutokana na idadi ndogo ya wakulima.
Wakati wakiendesha pikipiki mijini, wazee wao ambao hawana uwezo tena wa kulima, watakuwa wameshauza ardhi yote ili kupata fedha za kujikimu. Vijana watakaporejea na kubaini hali hiyo, hawatakaa kimya. Watajiunga pamoja kuirejesha ardhi yao.
Walionunua watakuwa na hatimiliki. Hawatakuwa tayari kuiachia. Vijana hawatakubali. Kwa kuwa vijana watakuwa jeshi kubwa, hapo ndipo vita itakapozuka kati yao na hao waporaji waliopewa jina zuri la ‘wawekezaji’. Muda huo utakapowadia ndipo vitabu vya historia vitaanza kuwatendea haki viongozi kama kina Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambao iliwalazimu kuingia kwenye ugomvi mkubwa alimradi tu kuhakikisha wanairejesha ardhi mikononi mwa Waafrika kutoka mikononi mwa Wazungu walowezi.
Kuuawa kwa Mabina ni manyunyu yanayoashiria kuwa kuna mvua kubwa inayokuja! Nani aliyewaza kuwa kuna siku ndugu zetu Wasukuma wanaweza kuwa na mioyo migumu ya kumuua kiongozi wao kwa mawe? Nani aliyejua yale yaliyoifanya Arumeru ikawika hadi Umoja wa Mataifa yanaweza kutokea Mwanza, Kilosa, Rufiji au kwingineko Tanzania?
Tufanye nini? Pengine si vibaya tukawa na kiasi. Waumini wa Kikristo na Kiislamu wanafundishwa kuwa na kiasi. Na kutenda kwa kiasi. Kuna sababu gani ya mtu kumiliki ekari maelfu kwa maelfu –tena wakati mwingine bila kuzitumia? Kwanini mtu mmoja awe na viwanja katika kila mkoa wa Tanzania? Kwanini mtu awe na tamaa ya kupata kila anapopatamani?
Kifo cha Mabina kitusaidie kutufumbua macho. Tutambue kuwa kumbe wananchi wakiamua hawawezi kuzuiwa kwa risasi wala nguvu zozote hata kama ni za mizinga na vifaru. Isitoshe, kuuawa kwa Mabina ni matokeo chanya ya namna wananchi walivyokosa imani na vyombo vya utoaji haki katika nchi yetu. Kama wananchi wangekuwa na imani na Jeshi la Polisi na Mahakama, kitu gani kingewafanya wajichukulie sheria mkononi? Sitaki kuingilia uhuru wa Mahakama katika hili, lakini kuna dalili za wazi kwamba wananchi hawakuwa na imani na Polisi wala Mahakama.
Walijua Polisi hawawezi kumzuia Mabina kwa sababu yeye ni kiongozi — tena kiongozi wa CCM, na pia ni mtu mwenye fedha. Mambo ni hayo hayo katika Mahakama. Tume ya Jaji Warioba ilishamaliza kila kitu. Siku hizi wananchi masikini wanazijua hukumu kabla hata kesi haijafikishwa Polisi au mahakamani. Kwa kuwa hujua hukumu ‘feki’ kabla ya kufika mahakamani, wanachofanya ni kutoa hukumu wanayojua ndiyo ya ‘haki’.
Tunahitaji uongozi utakaosaidia kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya utoaji haki nchini. Bila haki, tusitarajie muujiza wa kudumu kwa amani na utulivu nchini mwetu. Pia tunapaswa kuishi kwa kiasi. Mapambano ya ardhi hayatakoma hadi tuwe na viongozi wenye dhamira ya kweli ya kusimamia sera, kanuni na sheria zinazotoa haki kwa raia wote.
Mauaji haya hayatakoma hadi hapo Polisi, Mahakama na vyombo vyote vya utoaji haki vitakapotoa haki kwa wananchi, hasa wanyonge. Mauaji haya hayatakoma hadi hapo viongozi watakapoacha kuwaonea wananchi wanyonge. Buriani Kada Mabina.