Rais dikteta atatutoa hapa tulipo
Taifa lipo njia panda. Sheria hazifuatwi. Kila mmoja wetu anataka afanye au afanyiwe lile analotaka. Masikini wanazidi kuumia. Lakini kwa nafasi zao, nao wameamua kufanya kila wanaloweza alimradi nao wasiwe nje ya mparaganyiko huu.
Masikini wa vijijini na wale wanaoishi karibu na misitu hawajaachwa nyuma. Wameamua kuteketeza misitu kwa kuchoma mkaa na kukata kuni! Wanaoishi karibu na barabara kuu wamehakikisha wanang’oa alama za barabarani na vyuma vya madaraja. Kila kilicho mbele yao wanaona ni heri waambulie.
Wana hasira kuona maisha kwao yanazidi kuwa magumu, watoto wao wanasoma wakiwa wameketi chini, huku magari ya kifahari yanayotokana na kodi zao yakipita usiku na mchana.
Wanahujumu miundombinu ya umeme kwa kuiba mafuta kwenye transfoma. Wapo wanaowaona wakifanya uhalifu huo, lakini hawajishughulishi kuwazuia. Wanafanya hivyo kwa sababu wanaona wakubwa wanagawana nchi, wanasafiri kadri wanavyotaka, ilhali wakiwaacha wao wakiwa hoi bina taaban.
Dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma ndizo zinazouzwa kwenye maduka binafsi yaliyoenea hadi mlangoni mwa zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma. Wagonjwa wanajua. Wanalalamika kwenye uongozi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Wauguzi nao kwa kuona madaktari, wafamasia na wenzao wengine ndiyo wanaofaidi, nao hawako nyuma. Wameamua kuchukua kila kinachowezekana. Pale walipokosa chochote cha kuwafaa, wameamua, bila soni, kudai rushwa kutoka kwa wagonjwa au kwa ndugu wanaowahudumia.
Hata wapishi wanaopaswa kuwapikia wagonjwa wasio na uwezo, wamehakikisha ama wanagawana chakula na wagonjwa, au wanawakosesha kabisa hata hicho kidogo. Wagonjwa sasa wanasaidiwa na wagonjwa wenzao wodini.
Madereva wa magari ya umma ambao wanaona mabosi wao wanavyojitungia safari na kutumia magari hayo kukagua miradi yao binafsi, nao wameelekeza hasira zao kwenye ununuzi wa mafuta na matengenezo ya magari.
Kila wanapokwenda kuweka mafuta, sharti wawe na yao ya pembeni. Wameshirikiana na wakubwa wao wa kazi kuhakikisha kuwa karakana za Serikali zinakufa ili magari yatengenezwe chini ya miembe! Huko wanajua wanachofaidi.
Kwa miongo kadhaa sasa tunalia kuwa reli zetu zimekufa. Kuna habari kwamba barabara zinatumika kusafirisha asilimia zaidi ya 99 ya mizigo yote! Huwezi kujenga uchumi imara na kuwapa unafuu wa maisha wananchi kama unatumia mfumo huu. Kwanini reli hazitengenezwi? Kwanini hatupati reli mpya? Hapa tunaambiwa kuna nguvu za wakubwa.
Sakata lililotokea wiki kadhaa zilizopita la mgomo wa wamiliki wa malori ni dalili ya wazi kwamba kwa kuwaangukia matajiri hawa, hakuna reli wala treni itakayofanya kazi.
Wenye malori ni matajiri. Wenye malori wengi ni wanasiasa wanaopaswa kuibana Serikali ihakikishe kunakuwa na reli. Hapa ndipo ugumu wa mambo unapoanzia. Tunamhitaji kiongozi “kichaa” na mwenye roho ngumu kuweza kuweka mambo sawa.
Hatuhitaji ushahidi zaidi ya huu wa kuona leo wazazi wakiungana na wanafunzi kuwapiga walimu. Kupigwa kwa walimu kwa sababu tu ya kusimamia nidhamu ya masomo darasani, ni mparaganyiko katika Taifa.
Lakini kwanini walimu wasipigwe kama wao ndio hao wanaoongoza kuwatia mimba watoto wa kike? Juzi tumesoma habari za mwalimu aliyekamatwa akiuza bangi shuleni! Haya yote yanalifanya taifa letu liwe njia panda. Tuna wanafunzi wanaopiga walimu, lakini tuna walimu wanaowatia mimba wanafunzi na wengine wakiwauzia bangi wanafunzi na raia wengi wa kawaida.
Katika gazeti hili kuna habari ya maofisa wanyamapori wanaoshiriki ujangili. Hawa wamepewa bunduki na risasi ili wawalinde wanyamapori ambao ni chanzo kikuu cha mapato katika nchi yetu. Ndovu, nyati, simba na wanyamapori wengine ambao wangependa wakimbie kupata hifadhi kwa walinzi hao, sasa waende wapi?
Fikiria, watu wamepewa bunduki na risasi kuwakabili majangili, lakini sasa wameamua kushirkiana na majangili, na kwa kutumia bunduki na risasi hizo hizo za kuwalinda, wanawaua wanyama wasio na mtetezi.
Tunahangaika kusaka majangili ndani na nje ya hifadhi na mbuga, kumbe majangili wakuu ndiyo hao hao walioaminiwa na Serikali! Nchi imekwisha.
Polisi ambao kimsingi mwananchi mzalendo anapaswa kuwakimbilia kuomba hifadhi, leo ndiyo wahalifu wakuu. Heri ukutane na jambazi mtaani kuliko kukutana na polisi kituoni! Wamekuwa watesaji na washirika wakuu wa uhalifu.
Wao ndiyo wachora ramani za uhalifu. Ndiyo wanaowaelekeza wahalifu mahali kuliko na fedha. Wanapoitwa kwenye tukio la ujambazi hawahangaiki kuokoa roho na mali za wananchi, bali wanachoangalia na ma-fuko ya fedha zilizoporwa. Wanaondoka nayo na kwenda kugawana.
Polisi wamekuwa ndiyo wataalamu wa kuharibu kesi. Wamekuwa walimu wa wahalifu wakiendesha ‘mafunzo’ ya kuwawezesha kujinasua kutoka kwenye kesi. Wanasaidia kuharibu ushahidi na mwisho wa siku lawama zinaelekezwa kwa mahakimu na majaji.
Katika nchi ambayo unakuwa na polisi wanaotumia mafuvu ya watu kama vyanzo vya mapato, ujue hali si shwari. Tunahitaji mabadiliko ya kweli ya kuondoa na hatimaye kumaliza kadhia hii.
Na kweli haishangazi sasa kuwaona polisi wakitaka mlalamakijaji ndiye awe mtunzaji wa mtuhumiwa! Yaani, mtu aibiwe, amkamate mtuhumiwa, halafu huyo aliyeibiwa atakiwe kumhudumia kwa chakula, sabuni na mambo mengine huyo aliyekamatwa!
Mambo haya yanaweza kuonekana kuwa ni madogo, lakini ndiyo yanayochochea baadhi ya walalamikaji waone njia rahisi ya kupata haki ni kujichukulia sheria mkononi-maana haiwezekani mwenye tatizo ndiye tena aingizwe matatizoni kwa kumhudumia aliyemsababishia matatizo.
Tunapaswa kujitazama upya kuona kama kweli huu mwenendo wa polisi na wanajeshi kugeuka na kuwa waporaji utatufikisha tunakotaka. Walinzi wa amani wanapojigeuza na kuwa maadui wakuu wa hiyo amani, lazima tutafute njia ya kurejea kwenye mstari.
Mahakama zetu zina matatizo makubwa. Yapo yanayotokana na bajeti ya nchi, lakini mengine ni ya kutengenezwa. Tunao mahakimu na majaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu, lakini ni watenda haki. Lakini wapo wasio watenda haki. Hao wanalalamikiwa, na kwa kweli wanachangia kuwafanya wananchi waichukie Serikali.
Tunahitaji mabadiliko makubwa miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma. Tuondokane na hii tabia ya kuona kutenda haki kuwa ni jambo la hisani. Haki itendewe bila kujali hali ya mtu.
Je, haya yatamalizwa na Katiba mpya? Naweza kusema kwa kujiamini kabisa kuwa haya hayatamalizwa na Katiba mpya kama baadhi yetu wanavyoamini. Wapo wanaodhani kuwa kwa ujio wa Katiba hiyo, basi kila kitu kitakwenda sawa. Tunajidanganya.
Tatizo la nchi yetu kwa sasa ni mfumo. Kama Katiba mpya itasaidia kuufumua mfumo huu wa sasa, hilo litakuwa jambo jema, na kwa kweli hiyo Katiba itakuwa imekidhi kiu ya wengi.
Mfumo wa sasa hauruhusu watenda makosa kupata adhabu wanayostahili. Kuna mlolongo mrefu wa kumwadhibu mtumishi wa umma aliyefanya makosa. Kuna waziri mmoja wa zamani alipata kusema kuwa mfumo tulio nao unakwamisha mambo mengi serikalini.
Akatoa mfano kuwa hata kama dereva ataamua kumpiga waziri, waziri hatakuwa na uwezo wa kumwondoa kazini. Akasema hata kumwondoa mtumishi aliyekamatwa na mali ya wizi wa vifaa vya ofisi ni kazi ngumu. Kuna tume na mlolongo mrefu sana wa kumwadhibu mtu wa aina hiyo.
Waziri huyo akasema hata kwenye mlolongo wa utendaji kazi serikalini, Waziri anakuwa hana mamlaka ya kumbana Katibu Mkuu, Mkurugenzi na wateule wengine. Kwanini hawezi? Hawezi kwa sababu wote ni wateule wa Rais.
Mkuu wa Wilaya anakuwa mbabe mbele ya Mkuu wa Mkoa kwa sababu wote ni wateule wa Rais. Hakuna nidhamu. Hapo ndipo unapokuta mkurugenzi hamheshimu katibu mkuu, katibu mkuu hatii maelekezo ya naibu waziri, na naibu waziri hatii neno la waziri. Hakuna utii kwa sababu wote ni wateule wa rais.
Katiba mpya pamoja na kuainisha mambo mengi ya nchi, inapaswa itoe nguvu za kikatiba za kubadili mfumo mbovu tulionao sasa.
Waziri fulani wananchi kadha wa kadha walipata kumwomba Rais Jakaya Kikwete aongeze ukali. Wapo wanaosema hilo amelitekeleza, lakini wapo wanaoona hajafanikiwa.
Wapo wanaoamini kuwa rais ajaye anapaswa kuwa mkali. Anapaswa kufumua mfumo huu tulionao sasa ambao ni mfumo wa kulea maovu.
Tunapaswa kuwa na Serikali inayoheshimiwa, lakini inayoogopwa pia. Heshima inapaswa ianzie kwenye woga. Mataifa yaliyoendelea wananchi wake wengi wanaheshimu sheria. Heshima yao kwa sheria imetokana na kuogopa sheria. Wanajua kuvunja sheria si jambo la mchezo.
Dereva anayeendesha gari Marekani anajua asipoheshimu na kuogopa sheria, akinyang’anywa leseni ataabika. Hapa kwetu dereva wa basi akiua wanadamu 50 bado ataendelea kuendesha mabasi! Hakuna woga.
Kwa kadri hali ilivyo, tunahitaji kuwa na rais dikteta asiyechinja watu, lakini anayeweza kurejesha hali ya mambo kwenye mstari. Tulipo sasa ni pabaya mno. Tukiendelea hivi Tanzania itakuwa jamhuri ya wababe watakaofanya lolote na popote bila woga.