Wakati mwingine Wakristo
wanaanzisha chokochoko

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imewasilisha mapendekezo, ikitaka kubadilishwa kwa siku ya kupiga kura ya maoni kutoka siku ya ibada – Jumapili. Mapendekezo ya CCT yamewasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Mwakilishi wa CCT, Mchungaji Lazaro Rohho, anasema mabadiliko hayo yanatakiwa kuwekwa kwenye muswada wa kura ya maoni unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Bunge.

Hii si mara ya kwanza kwa Wakristo kutaka Jumapili isiingiliwe na kazi nyingine, zaidi ya kuwa maalum kwa ibada.

 

Niseme wazi kwamba ingawa naheshimu maudhui ya CCT kwa siku ya Jumapili, bado hawajatoa sababu za kunishawishi kuwaunga mkono. Kwa maana hiyo, napingana nao.

 

Mjadala huu umekuwa ukijitokeza mara kwa mara. Wakristo wamekuwa wakitaka Jumapili isiwe siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani. Hoja yao mara zote imekuwa kwamba kutokana na Jumapili kuwa siku ya ibada, inawawia vigumu kushiriki uchaguzi huo vizuri.

 

Hili jambo ni muhimu tukalijadili. Umuhimu wa mjadala huu, tena kwa wakati huu ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba tunajitahidi kuijenga Tanzania yenye utengamano, mshikamano na zaidi ya yote-kuvumiliana.

 

Ni ukweli ulio wazi kwamba kwa sasa jambo lolote linalohusu imani limekuwa likipokewa kwa mitazamo tofauti kulingana na madhehebu.

 

Ndugu zangu, mara zote Watanzania wema wanaoitakia mema nchi yetu wamesisitiza sana kuvumiliana. Uvumilivu unaozungumzwa hapa unawahusu Watanzania wote – Wakristo, Waislamu na wale wasioamini huyu Mungu wa kwenye Korani na Biblia.

 

Kelele hizi za Wakristo za kuanza kuhamasisha Jumapili isiguswe, zinaweza kuibua madai mazito kutoka kwa Waislamu. Waislamu wanaamini kabisa kwamba Ijumaa kwao ni siku takatifu. Ndiyo siku yao kuu ya ibada.

 

Pamoja na ukweli huo, bado wameridhia Ijumaa isiwe siku yao maalum ya mapumziko. Ndiyo maana utawaona wakiwa katika ofisi za umma na ofisi binafsi wakichapa kazi. Hawajawahi kusema Ijumaa isiguswe kwa namna yoyote ile na shughuli za kiserikali au za kijamii. Wamekuwa wakiswali na kisha kuendelea na mambo mengine kadri inavyowezekana.

 

Kitendo cha wao kukubali siku yao ya ibada – Ijumaa – itumike kwa shughuli nyingine, ni uvumilivu wao kwa ndugu zao Wakristo. Wakikomaa tunaweza kujikuta tukiwa na siku tatu za mapumziko katika nchi hii, yaani Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

 

Watanzania sasa tupo kwenye maandalizi ya kuwa na Katiba mpya. Suala la Uchaguzi Mkuu linaweza kuwa la kikatiba. Kwa hiyo si vema sana kulijadili hapa. Lakini hoja yangu kwa desturi tuliyokwishakuwa nayo ya kuifanya Jumapili kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu, ni kwamba jambo hilo halijaathiri kitu chochote miongoni mwa Wakristo. Sana sana ni uamuzi uliosaidia kujenga mshikamano na uvumilivu miongoni mwa Watanzania wa madhehebu haya makubwa.

 

Tukianza na hili la Uchaguzi Mkuu, sikuona ubaya wowote kwa miaka mitano, Wakristo kutenga siku moja ya Jumapili kwa ajili ya upigaji kura.

 

Miaka mitano ina wastani wa siku 1,825. Kutenga siku moja ndani ya siku zote hizo kwa ajili ya kupiga kura, sioni kama ni jambo la kutusumbua vichwa.

 

Miaka mitano ina Ijumaa 260 hivi. Ndani ya siku 1,825 Waislamu wamekubali siku zao 260 ziingiliwe na mambo mengine ya umma. Kama wao wameweza kuvumilia kwa siku 260, kwanini Wakristo wawake kwa siku moja tu?

 

Sina hakika, lakini akili ya kawaida inanifanya niamini kuwa mtu huwezi kuhukumiwa kwenda motoni kwa sababu Jumapili moja ndani ya miaka mitano hukuhudhuria ibada kanisani! Kwenye maandiko utawala huu Serikali umetambuliwa, je, kweli ni kosa kubwa la mtu kuukosa ufalme wa mbinguni kwa sababu tu ya kukosa au kuchelewa kwenda kanisani mara moja ndani ya siku zaidi ya 1,800?

 

Bado najiuliza, kama uchaguzi ni Jumapili, wapi kumeandikwa kuwa ibada lazima ifanyike asubuhi? Wapi kunakosema Mungu hapokei sala za jioni? Kama sivyo, kuna ubaya gani kuwahi kupiga kura, kisha waamini wakaenda kwenye ibada? Au kuna ubaya gani kuwahi kwenye ibada, kisha mtu akajielekeza kwenye uchaguzi?

 

Hili la kura za maoni linaloweza kufanyika mara moja baada ya miaka mingi sana, kuna ubaya gani kwa Wakristo kuridhia lifanywe siku ya Jumapili?

 

Wakristo wa kweli ni watu weledi. Ni wavumilivu. Kunapoanza kutolewa madai ya aina hii, ni wazi kuwa upande wa pili nao wanaambiwa waanze kuleta madai yao. Sote tukitaka tutendewe kadiri ya matakwa yetu, tutaivuruga nchi yetu.

 

Mei 30, 2010 katika gazeti la Mtanzania, niliandika makala inayofanana na hii. Mmoja wa viongozi waandamizi katika Taifa letu alipoisoma, alinitumia barua pepe ya kunipongeza. Napenda kunukuu maandishi yake hapa, lakini kwa kuwa hakunipa ridhaa ya kuichapisha, naomba nilihifadhi jina lake. Alisema hivi:

 

Ndugu Manyerere Jackton,

Nimeipenda sana makala yako iliyochapishwa katika gazeti la Mtanzania la leo Jumapili, tarehe 30 Mei 2010. Uk. wa 7. Nimeipenda kwa sababu ni makala ambayo ina sifa ya kuwa na “nguvu ya hoja”, kutokana na utafiti ulioufanya katika maandiko matakatifu ili kuimarisha hoja yako.

 

Kusema kweli, hilo “Jukwaa la Maaskofu” lilitoa kauli ya kukataa uchaguzi usifanyike siku za Jumapili, limefanya kosa la kujielekeza kwenye tatizo ambalo halipo kabisa, kwani siyo tatizo halisi, bali ni tatizo la kufikirika tu.

 

Mimi ni Mkristo, na nimekuwa nikipiga kura (pamoja na Wakristo wenzangu wengi tu) katika kila uchaguzi mkuu uliofanyika siku za Jumapili kila miaka mitano tangu mwaka wa 1965. Vile vile, nimekuwa nikipiga kura pamoja na Wakristo wenzangu wengi tu, katika chaguzi ndogo nyingi sana za Ubunge na Udiwani, ambazo zimekuwa zikifanyika siku za Jumapili tangu wakati huo hadi leo. Lakini mimi na Wakrito wenzangu hao hatujawahi hata mara moja kushindwa kwenda kanisani kusali katika siku hizo, eti kwa sababu ya kukosa nafasi ya kufanya hivyo kwa kuwa tulikwenda kupiga kura!

 

Nimetaja mapema hapo juu kwamba makala yako ina nguvu ya hoja. Kinyume cha maneno hayo “nguvu ya hoja”, ni “hoja ya nguvu”. Kwa hakika, Jukwaa la Maaskofu limetumia “hoja ya nguvu” katika kuzungumzia jambo hili.

 

Kama ulivyoeleza  wewe katika makala yako, kura zinapigwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi jioni, ambao ni muda wa kutosha kabisa kuwezesha mambo yote mawili kufanyika. Napenda kuongeza kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi inao utaratibu mzuri tu wa kupanga idadi ya wapiga kura katika kila kituo cha kupigia kura wasizidi watu 350. Idadi hiyo inawezesha wahusika kufanya shughuli zao nyingine kabla au baada ya kupiga kura, bila hofu ya kuikosa nafasi hiyo ya kutekeleza wajibu wao wa kiraia.

 

Siku aliyoingia madarakani kama Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe. Tony Blair alisema maneno ya busara yafuatayo, katika mkutano wake na waandishi wa habari wa nchi hiyo:

 

“What is good and working well, we will keep.

What is not, we will change”

Utaratibu wa kupiga kura siku za Jumapili ni mzuri. Na umefanya kazi vizuri tangu mwaka 1965. Yafaa tuendelee nao.

Mwisho.

 

Baada ya kuyasikiliza mapendekezo ya CCT nimejiridhisha kuwa hayana mashiko. Hayalengi kujenga utangamano miongoni mwetu Watanzania. Yanaibua hisia za kila madhehebu kuanza kudai mambo ambayo mustakabali wake ni mbaya kwa Taifa letu.

 

Kalenda inayotumika sasa (Gregorian) inatambulika kama kalenda ya Kimagharibi au kalenda ya Kikristo. Wakati Waislamu wengi wakiwa wamekubali kuutambua mwaka huu kama mwaka 2013, kwenye kalenda yao huu ni mwaka 1432.

 

Pamoja na ukweli huo, Waislamu hawasikiki wakitaka sasa kalenda yao ndiyo itambulike hapa nchini. Wameamua kuikubali ile ya Kikristo kama sehemu tu ya uvumilivu na staha; wakitambua kuwa hawawezi kupata wanayotaka kwa asilimia 100. Kadhalika, Wakristo nao wanapaswa kuwa na moyo wa aina hiyo.