Mawazo yametuama kwenye bodaboda
Tanzania haikosi mambo yanayoibua mijadala. Tukimaliza moja, lazima litaibuka jingine. Tumekuwa Taifa la mijadala ambayo mingi haina tija.
Kama ilivyo ada ya kuwapo matukio ya ajabu ajabu nchini mwetu, kumetolewa habari kuwa majambazi wamevamia Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza.
Uvamizi haukuwa wa kupiga risasi na kuondoka. Walioshiriki tukio hilo waliingia hadi kwenye vyumba nyeti, wakaondoka na mafaili ya kesi na vitu vingine walivyotaka.
Kilichovamiwa si kituo cha polisi tu bali kituo kikuu! Hii ni dhihaka. Wajinga ndiyo wanaokubali na kuamini kuwa kweli tukio hilo limefanywa na majambazi. Haihitaji kipaji cha ujuzi kutambua kwamba wavamizi wa kituo ni polisi wenyewe! Hivi inawezekana vipi majambazi wavamie kituo kikuu cha polisi? Kuna nini humo hadi wafanye uhalifu wa aina hiyo? Gerezani unaweza kuamini kuwa huenda mpango ulikuwa kuwatorosha wahalifu. Tukio la Mwanza hawakwenda mahabusu, kwa hiyo hatuwezi kuamini kuwa lengo lao lilikuwa kuwatorosha mahabusu!
Kumekuwapo kauli kwamba Chadema waliapa kuwa nchi haitatawalika. Kauli hii imetumiwa sana na wasiokipenda chama hicho. Kwenye mikutano ya wapinzani wanaoanzisha vurugu ni polisi, lakini hatimaye tunaambiwa wapinzani wanatekeleza azma yao ya kuhakikisha nchi haitawailiki. Hizi ni porojo.
Tanzania tumekuwa na viongozi kadhaa wachovu, wabinafsi na wasiojua wapi nchi inapaswa kupelekwa. Kama alivyowahi kusema Mzee Kolimba, hatuna dira wala mwelekeo. Tunasukasuka kama jahazi lililokatika tanga! Hatujui tuendako, na kwa sababu hiyo hatuoni kama tunapotea. Mara zote wanasema ukijua unakwenda wapi, unaweza kufika mahali ukashtuka kwamba uko sawa sawa au umepotea. Kwa vile hatujui tunakokwenda, hatuoni kama tunapotea! Kila tunapogeuka na kutazama, tunajiona tu salama na tuko kwenye mwelekeo.
Nchi kutotawalika kuna maana nyingi. Moja, inaweza kuwa hiyo wanayoisema wapinzani, hasa Chadema. Lakini katika mazingira ya Tanzania, Chadema kutekeleza dhana hiyo ni jambo gumu. Kwa sababu hiyo, napuuza propaganda zote zinazoelekezwa kwa chama hicho kuhusu kauli yake.
Wanaofanya, na ambao kwa kweli wameifanya Tanzania isitawalike, ni watawala wenyewe. Nani anaweza kubisha ukweli huu?
Serikali imeamua kwa dhati kabisa kuwaaminisha vijana wa Tanzania kwamba bodaboda ndiyo ajira ya kuwaletea maendeleo! Wanasiasa wamegundua mtaji wa ushindi uko kwa vijana. Kwa sababu hiyo, wanapigana vikumbo kuwateka kupitia ulimbo wa pikipiki. Wanajitahidi kuwavuta kwa kuwapa mikopo ya kifo na vilema.
Benki ambazo kwa kawaida ni mawakala wa matajiri, zimeanzisha mikopo maalum ya bodaboda na bajaj kwa vijana. Kampuni za simu zinapigia upatu mikopo ya bajaj na bodaboda!
Hakuna benki inayotoa trekta kwa kijana. Hakuna kampuni ya simu inayoendesha shindano la kupata trekta! Hawa wametusoma akili zetu na kuona ni za ki-bajaj bajaj. Ni za ki-bodaboda!
Mawakala wa ubepari wanatoa misaada ya vitu hivi ili vijana wengi wamalize muda wao barabarani, na wao matajiri wautumie kwenda vijijini kujitwalia ardhi. Ardhi sasa inauzwa kama njugu. Kwa kasi hii ya ununuzi wa bajaj na bodabida, vijana malaki kwa malaki wameweka kando kilimo. Wazee ndiyo walioachiwa dhima hiyo.
Wakati vijana watakapobaini kuwa bajaj na bodaboda si lolote wala chochote kwa maisha yao, watarejea vijijini. Huko watakuta ardhi yote imeshatwaliwa na matajiri wachache. Vijana hao hawatavumilia. Watajiunga kuendesha mapambano ya kurejesha ardhi iliyopokwa wakati wakiwa kwenye bodaboda na bajaj. Matajiri watalindwa kwa nguvu zote – za kisheria na za mitutu.
Kwa kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vina watu kadhaa wanaoabudu fedha na matajiri, hawatasita kutumia maguvu kuwazima vijana. Lakini jeshi la vijana litakuwa kubwa! Kutakuwapo mapambano makali na ya hatari. Hapo Tanzania itakuwa kwenye ukurasa mmoja na Zimbabwe. Nchi itakuwa haitawaliki. Watakaokuwa wamebariki dhambi hiyo ni hawa hawa viongozi wetu wabinafsi.
Tanzania haitawaliki kwa sababu ya rushwa ambayo mwasisi wake si Chadema wala chama chochote cha upinzani. Tunalia ujangili. Tembo wanamalizwa. Wanyamapori wanatoweka. Majangili wanakamatwa kila siku, lakini wanaachiwa huru. Hivi karibuni kulikamatwa majangili hatari mkoani Arusha. Wakataja mtandao wao. Walipanga kuwaachiwa kinyemela. Vyombo vya habari vikaandika. Mpango ukaahirishwa. Wiki kadhaa zilizopita, kwa kutambua “ulikuwa upepo tu”, watuhumiwa wote wamepewa dhamana. Siku mbili tu baada ya dhamana, wakaingia Manyara na Tarangire wakaua tembo wakubwa!
Polisi na wanajeshi wamekuwa majangili. Juzi tu, tumemwona mwanajeshi mwenye sare tukufu za jeshi letu akiwa na pembe za tembo akizisafirisha. Mwaka jana gari la jeshi lilikamatwa likiwa na pembe za tembo mkoani Arusha.
Polisi wamekamatwa wakisafirisha shehena kubwa ya bangi kwa kutumia gari la mkuu wao wa kazi. Wengine walikamatwa mkoani Morogoro wakiwa na fuvu la binadamu wakilitumia kama chanzo cha mapato! Fikiria, hawa ndiyo walinzi wetu wa amani. Hawa ndiyo eti wamekula kiapo cha utii!
Lakini nani asiyejua kuwa haya yanayofanywa na polisi na wanajeshi wa chini ni madogo mno yakilinganishwa na yanayofanywa na wakubwa wao? Nani asiyejua kuna hesabu zinazowasilishwa kwa polisi wenye vyeo vikubwa? Wanajeshi wanaohojiwa kwa kuwa na fedha ughaibuni, wamezitoa wapi? Hata ikibainika walikula rushwa, watafanywa nini?
Je, haya ni matokeo ya Chadema kuifanya nchi isitawalike? Chadema ndiyo wenye Mahakama, Polisi, Usalama wa Taifa, Takukuru na kwa hiyo wameamuru vyombo hivyo visifanye kazi kwa mujibu wa viapo? Jibu ni hapana. Nani wahusika? Ni Serikali ya CCM.
Nchi hii imekuwa pepo kwa wahujumu uchumi. Kwa mara ya kwanza sasa tunaona watu wanaokabiliwa na kesi za uhujumu uchumi wakiwa nje ya mahabusu. Anayebisha arejee kwenye kesi iliyokuwa ikimkabili Iddi Simba, mtu aliyejitwalia fedha za umma – Sh milioni 320.
Wakati vibaka wakisota rumande, Simba tukawa naye mtaani bila kujali kwamba anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi! Kana kwamba haitoshi, DPP akamwachia huru (scot free)! Hakuna kesi. Kwa kuachiwa kwake, Takukuru na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wameonekana bure tu!
Uamuzi huu una athari hasi kwa mustakabali wa ulinzi wa mali za umma. Kwa maneno mengine ni kwamba sasa mtu unaruhusiwa kula chochote pale ulipo bila kuhojiwa. Sasa mtu yeyote anaweza kukwapua mali ya umma bila wasiwasi maana anajua atafanya anavyotaka, mwishowe hataadhibiwa. Je, haya ndiyo matokeo ya Chadema iliposema nchi haitatawalika? Hapana.
Juzi tumeandika habari ya matumizi ya Sh bilioni 8 kwenye mkutano wa Smart Partnership. Tumeonesha namna mamilioni yalivyotafunwa. Tumeonesha kampuni hewa zilizolipwa mamilioni ya shilingi, lakini kwa kuwa ni hewa, hazikulipa hata shilingi moja kama kodi!
Badala ya vyombo vya dola kuwashupalia waliofanya madudu hayo, kibao kimetugeukia sisi kwa sababu kwenye gazeti tulichapisha barua ya Ikulu yenye neno “secret”. Polisi wametukamata. Wametuhoji na tunasumbuka sasa kwa sababu tu ya hilo neno “secret”.
Kwao, hizo herufi sita ni hatari kwa usalama wa nchi na wananchi kuliko hao waliotafuna mabilioni! Kwao, hilo neno ni hatari sana kuliko hawa waliokula fedha ambazo zingeweza kutengeneza madawati na kuwaondolea adha watoto wetu wanaoketi chini na wengine wanaosomea chini ya miti! Kwao, hilo neno ni hatari sana kuliko ile hatari inayowakabili kina mama wanaokwenda kujifungua wakiwa na ndoo za maji!
Hawa wanaofanya haya wanataka Serikali yao ipendwe. Ipigiwe makofi. Ishangiliwe. Wanapokosa hayo mambo, wanawageukia Chadema na kusema, “Ninyi ndiyo mnaofanya nchi isitawalike. Mliahidi, na sasa mnatekeleza!”
Ndugu zangu, nchi ambayo rushwa imebarikiwa, na wala rushwa wanaenziwa, haiwezi kutawalika. Ndiyo maana leo utasikia kampuni za simu zinaiba umeme. Badala ya kulipa Sh milioni 70 kwa mnara mmoja kwa mwezi, zinalipa Sh milioni 1.5. Wanaobainika wanaachiwa hivi hivi. Wanaachiwa, ama kwa sababu sheria zetu ni butu, au kwa sababu ya rushwa. Watumishi shupavu wanaowasaka hawa wanaandamwa. Wanavunjwa moyo. Unapofikia hatua hiyo, huwezi kuwazuia polisi nao kuiba umeme kutoka kituoni na kuwaunganishia watu kinyemela. Tanzania ndipo tulipofika.
Nchi ambayo polisi au mwanajeshi ana “cheti” kinachomruhusu kuvunja sheria, huwezi kutaraji iwe na usawa katika kuheshimu na kutii sheria. Kama polisi mwenyewe anaendesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu, huyu mwananchi wa kawaida ataanza vipi kuheshimu sheria hiyo? Kama “majambazi” wanaingia Makao Makuu ya Polisi, nyumba gani ya masikini itapona?
Nchi ambayo wakubwa wameona mbinu ya kukabiliana na foleni ni kuongeza idadi ya vimulimuli ili kina kabwela wawapishe, itakuwa na amani kweli? Yaani wakubwa wao wapite kwa kasi, masikini wamejazana ndani ya daladala wakibadilishana harufu za vikwapa, unadhani kutakuwa na upendo miongoni mwetu kweli?
Kwanini wakubwa kila wanapojenga mahekalu yao wanazungusha kuta ndefu? Wanaogopa nini? Kama hawawafanyii dhuluma makabwela hawa, nini kinawatia hofu? Kama wahadhulumu, shaka ya nini hata wajilinde kiasi hicho? Kama wao wakubwa ndiyo wanaoshiriki biashara ya mihadarati, kwanini wakwepe adha za kuvamiwa na vijana walevi wa dawa hizo?
Ndugu zangu, ninachotaka kusema hapa ni kwamba tunapaswa kuketi na kuona namna ya kuondokana na haya “mazingaombwe”. Namna nzuri ni kuwa na viongozi makini na wenye dhamira ya kweli ya kutenda haki.
Bila kuwapo haki, hata haya makambi ya JKT tunayojitahidi kuyaanzisha ni kazi bure. Kama haki ni kwa wakubwa tu, masikini shauri yao, sioni ni kwa namna gani huo uzalendo unaweza kujengwa na upande mmoja.
Badala ya watawala kuishutumu Chadema kwamba inaifanya nchi isitawalike, tukubali kuwa wanaofanya kazi hiyo kwa uadilifu na umakini mkubwa ni Serikali hii hii ambayo haijawahi kuongozwa na wapinzani.
Mwaka 2015 ni wa maana sana kwa kila Mtanzania mpenda maendeleo. Tunahitaji mabadiliko. Muhimu ni kuhakikisha kila mmoja wetu mwenye haki ya kupiga kura, anaanza maandalizi sasa. Aibu ya Arusha ya idadi ndogo ya wapigakura isitupate tena. Tudhamirie kuwa na viongozi walio tayari kuondoa dosari hizi. Hadi muda huo utakapowadia, bado nitaendelea kuamini wanaofanya nchi isitawalike, ni hawa hawa – Serikali ya CCM.