Hivi karibuni gazeti hili liliandika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinavyoathiri taaluma kwa ya wanafunzi wa Shule za Msingi Ikandilo iliyopo katika Kijiji cha Ikandilo, Kata ya Nyaruyeye, wilayani Geita na kusababisha baadhi ya wanafunzi kutokuhudhuria masomo ipasavyo.

Makala hiyo pia ilieleza changamoto za kielimu zinazozikabili shule mbalimbali zilizopo katika maeneo yanayozunguka migodi ikiwemo ukosefu wa madawati, nyumba za walimu na vyoo hali inayowafanya wanafunzi kusoma katika mazingira hatarishi. 

Kwenye makala hiyo, lilimunukuu Mkurugenzi wa Kampuni ya Onesmo Gold Mine Project, iliyofadhili ujenzi wa darasa na ofisi ya walimu Shule ya Msingi Ikandilo, Onesmo Malugu akiwataka wadau mbalimbali kuwa na moyo wa kujitolea kusaidia shule zilizopo katika kata za Nyarugusu na Nyaruyeye si kuibebesha mzigo huo serikali pekee.

Siku chache baada ya taarifa hiyo kutoka Gazetini, baadhi ya wamiliki wa migodi Kata ya Nyarugusu wamejitolea kuanza kupunguza changamoto hizo kwa kuchangia madawati, kujenga madarasa na vyoo hatua ambayo imepongezwa na wananchi.

 

Kijiji cha Ililika

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ililika kilichopo kwenye Kata ya Nyarugusu, Daniel Ng’wiigulu anasema kijiji chake kinao wachimbaji wenye leseni zaidi ya 150, wakazi 467 ikiwa ni pamoja na migodi minane ya kuchenjua marudio ya dhahabu ambapo wawekezaji wa kuchangia wametoa madawati 80 yenye thamani ya Sh milion 6, ujenzi wa nyumba ya mwalimu, ukarabati madarasa katika Shule ya Msingi Ililika na kuchimba matundu 12 ya choo.

‘’Tunawashukuru baadhi ya wawekezaji kwa michango yao wanayotoa japo kuna  wengine ndani ya kijiji chetu ni wakorofi hawataki kuchangia shughuli za maendeleo na ndiyo maana unaona utekelezaji wake ni wa kususasua na wamekuwa wakidharau ofisi zetu. Wanaona wa kuongea naye ni Mkurugenzi wa Halmashauri au Mkuu wa Wilaya huku wakitoa kisingizio cha kutoa mapato serikalini,” amesema Ng’wiigulu.

Mtendaji wa kijiji hicho, Fabian Lukas, amesema iwapo wawekezaji wote katika kijiji hicho wangekuwa na moyo wa kujitolea kusingekuwa na changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu kijijini hapo.

 

Kijiji cha Ziwani

Mtendaji wa Kijiji cha Ziwani, chenye wakazi 5,226, Kata ya Nyarugusu Wilayani Geita, Emmanuel Godfrey amesema mwekezaji mmoja tu Evarist Paschal, ndiye amekuwa akichangia maendeleo ya elimu kwenye shule hiyo ambapo amechangia madawati 240.

“Huyu bwana ana moyo kweli wa kujitolea maana baada ya kunipatia madawati hayo niliyagawa kwenye shule mbili zilizopo katika kijiji changu na mengine 100 niliwagawia jirani zangu wa shule jirani ya Zahanati,” anasema Godfrey.

Pia Evarist amejenga darasa moja na ofisi katika Shule ya Msingi ya Nyarugusu aliyosomea na kwamba hata mwaka 2013 amewahi kuchangia ujenzi wa choo katika shule ya msingi Ziwani.

Amewaomba wawekezaji wengine kuiga mfano wake kwani bado wanakabiliwa na changamoto kwenye sekta ya elimu ikiwemo upungufu wa nyumba za walimu na madarasa.

 

Kijiji cha Mawemeru

Mtendaji wa Kijiji cha Mawemeru, Safari Lweyo amesema kijiji chake kina migodi 6 ya kuchenjua marudio ya dhahabu.

“Wapo wawekezaji ambao angalau wanakumbuka kutusaidia katika sekta ya elimu, lakini sio kwa kasi kama ambayo tuliitarajia kama wananchi. Angalau wametusaidia kuboresha majengo (madarasa), lakini bado hitaji ni kubwa,” anasema.

 

Kijiji cha Nyarugusu

Mtendaji wa kijiji cha Nyarugusu, Binas Malekela amesema kijiji hicho kinayo migodi mitatu ya kuchenjua marudio ya dhahabu.

Kati ya migodi hiyo mmoja umetoa madawati 100 yaliyotengenezwa kwa chuma ambapo  umekwishakabidhi 75 huku mengine 25 ameahidi kuyamalizia hivi karibuni.

Pia wamefanikiwa kusaidiwa ujenzi wa darasa moja, nyumba moja ya mwalimu. Mkurugenzi wa Onesimo Gold Mine, uliopo katika Kijiji cha Mawemeru katika kata hiyo ya Nyarugusu, Malugu Onesimo, anasema kinachomsukuma kuchangia maendeleo ya elimu ni kutokana hatari ya uchimbaji wa madini kuwa mgumu miaka ijayo.

‘’Tungekuwa tunaona ushirikiano wa serikali wakati wa ujenzi na kufungua miradi yetu nadhani wengi wangetamani kuchangia kwenye elimu, lakini hilo halifanyiki kwani badala ya viongozi wa juu wa wilaya na mkoa kuja kushirikiana nasi kwenye ufunguzi wa miradi tunayowekeza kwenye jamii tumekuwa tukiwaona madiwani, watendaji, waratibu elimu na hata makatibu Tarafa hali inayotukatisha tamaa,’’ anasema Malugu.

Evarist Paschal anasema amechangia katika shule mbalimbali zilizopo katika Kata ya Nyarugusu, wilayani Geita ikiwemo ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Nyarugusu, shule aliyosomea na ofisi ya mwalimu viliyogharimu zaidi ya Sh milioni 20.

Evarist pia amechangia matofari 1,500 kwenye ujenzi wa shule mpya ya msingi Buziba, Nyaruyeye Sekondari mifuko 100 na mifuko 200 ya saruji sekondari ya Nyarugusu kwa ujenzi wa maabara.

Pia amechangia madawati 100 kwenye shule mbili za msingi za Kibima A na B za Kagongwa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Colnel Simba Gold Mine uliopo katika kijiji cha Ililika Elias Simba, anasema amesaidia ujenzi wa maabara sekondari ya Nyarugusu kwa kutoa mifuko 100 ya saruji na anatarajia kuvuta umeme kwenye shule ya msingi Ililika kutoka mgodini kwake utakaogharimu zaidi ya Sh milioni 16.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Tawi la Geita (GEREAMA), Paul Shenye aliiomba Serikali kusaidia wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo ya kuchimba na kwa kufanya hivyo watakuwa msitari wa mbele kuchangia maendeleo ya nchi hususani suala la elimu tofauti na ilivyo sasa ambapo ni kama wametelekezwa.

Katibu Mkuu wa GEREAMA Mkoa wa Geita, Golden Hainga mbali na kulipongeza Gazeti la JAMHURI kwa juhudi linazofanya kuhamasisha maendeleo, amesema katika utekelezaji kwa vitendo agizo la Rais la kuhakikisha tatizo la madawati linabaki historia hapa nchini na watoto kusoma wakiwa wamekaa kwenye madawati, chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wadau mbalimbali hususani wachimbaji kuchangia.