Mwaka jana niliwaalika baadhi ya walimu
wangu wapendwa walionifundisha shule ya
msingi. Miongoni mwao alikuwamo
aliyenifundisha darasa la kwanza.
Sina maneno mazuri ya kueleza furaha
niliyokuwa nayo, na zaidi ya yote,
waliyokuwa nayo walimu wangu. Pamoja
nao, niliwaita baadhi ya wanafunzi
wenzangu tuliosoma pamoja.
Lilikuwa tukio lililotutoa machozi ya furaha
baadhi yetu tuliofundishwa na walimu hao
miaka mingi iliyopita. Nilifanya hivyo ili
kutambua, kuthamini, kuenzi na kusharifu
mchango wao usiopimika – waliouweka
katika maisha yetu.
Kati ya walimu zaidi ya 10 waliohudhuria,
wawili tu ndio walikuwa hawajastaafu.

Mmoja amestaafu Julai, mwaka huu.
Wakati wa mazungumzo yetu kilio cha
walimu wangu hawa kilifanana. Kilio cha
mafao na pensheni. Wote walizungumzia
ugumu wa maisha baada ya kustaafu.
Waliokuwa hawajastaafu shaka yao ikawa
kwamba hayo yanayowapata wenzao
yatawapata pia. Kweli, mmoja ameanza
kuugulia maumivu. Tangu amestaafu Julai,
mwaka huu, leo ni Oktoba hajapokea mafao
wala pensheni.
Nilizungumza na walimu wangu, japo
hawakutamka kuwa wananituma nikafikishe
kilio chao kwa wahusika, maelezo yao
yalitosha kunifanya nitambue kuwa
wamenituma.
Nami kwa kutambua kuwa ni wao
walionifundisha kusoma na kuandika, basi
niwasilishe kilio hiki kwa mamlaka
zinazohusika.
Kilio cha walimu wangu hawa ni tone tu
katika bahari ya manung’uniko ya walimu
kote nchini.
Nimepitia kauli za viongozi wetu wakuu na
kusoma baadhi ya maneno na ahadi
walizokwishatoa.
Desemba, mwaka jana Rais John Magufuli,

akiwa Dodoma, alizungumza na walimu kwa
urefu na mapana. Akawaahidi mengi yenye
neema, na yeye akaeleza matarajio
aliyonayo kutoka kwao kwa ajili ya ustawi
wa taifa letu.
Miongoni mwa mambo aliyowatoa shaka ni
lile la kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi
ya jamii. Akasema michango yao ipo
salama na mafao yao watayapata kama
kawaida.
Kauli kama hii imekwisha kutolewa na
wasaidizi wake pia ikiwalenga walimu na
watumishi wa umma wengine.
Hata hivyo mafao na pensheni ya walimu
vimeendelea kuwa kilio chao kikuu. Hali hii
inawafanya waishi kwa taabu, hasa
ikizingatiwa kuwa kada hii ni ya watumishi
wasiokuwa na kipato kikubwa.
Walimu wengi, kwa asili ya kazi yao,
wamejikuta wakistaafu wakiwa na maisha
ya kawaida mno. Kwa sababu hiyo,
hutegemea mafao na pensheni ili walau
ziwasaidie kuhitimisha safari ya maisha yao
duniani.
Katika kufuatilia kilio cha walimu, yupo
mwingine aliyestaafu mwaka 2016, lakini
hadi Aprili, mwaka huu alikuwa hajalipwa
mafao. Nimeambiwa hadi wiki iliyopita

alikuwa akiendelea kutaabika. Nimepigiwa
simu na walimu wengi waliostaafu Julai,
mwaka huu, kilio chao ni hicho hicho.
Walimu wengi hufika kwenye ofisi za malipo
lakini majibu wanayopewa ni kuwa Hazina
haijatoa fedha!
Kwa namna ya pekee nimeona
niwakumbuke walimu kwa kuwafikishia kilio
chao kwa wahusika nikiamini watatendewa
haki, hasa ikizingatiwa kuwa kada hii ndiyo
injini na chimbuko la maarifa, vyeo na
tambo za wengi wetu.
Hakuna yeyote awaye miongoni mwetu
anayeweza kutambia mafanikio aliyonayo
bila kuwataja walimu waliomwezesha kuwa
hivyo alivyo. Walimu ndiyo injini ya
mafanikio yote tunayojivunia – mtu mmoja
mmoja, jamii, taifa na hata ulimwengu
mzima.
Walimu si watu wa kupata shida
zinazoepukika kama hizi za kulipwa mafao
au pensheni zao. Walimu si watu wa
kuhangaika kwenye korido au ngazi
wakibisha hodi mlango mmoja baada ya
mwingine wakiulizia malipo yao, na wakati
mwingine wakijibiwa vibaya.
Walimu si watu wa kutaabika kiasi cha
kuwafanya baadhi yao wajinyonge kutokana

na danadana za watumishi wanaostahili
kuwatendea haki kwa mujibu wa sheria.
Walimu, kama walivyo watumishi wengine
wa umma, kustaafu kwao kuko kwenye
shajara. Inajulikana lini mwalimu aliajiriwa
na lini atastaafu kwa mujibu wa sheria.
Kama hivyo ndivyo, iweje mafao yao
yasiandaliwe mapema – ikiwezekana
mwaka mmoja kabla ya kustaafu ili muda
wa kustaafu unapowadia apate stahiki zake
mara moja?
Kwa hakika inatia simanzi kuwaona walimu
waliokwisha kuzeeka wakitaabika njiani na
ofisini kwa kufuatilia mafao. Inaumiza
kuwaona wakipata ajali au wakikosa namna
ya kuishi kwa sababu tu wamesafiri kutoka
mbali kwenda Hazina, Utumishi au PSSSF
kufuatilia mafao na pensheni zao.
Bahati nzuri tunaye rais ambaye kitaaluma
ni mwalimu. Matarajio ya walimu wenzake
ni kuona anawaondolea kero hii ya mafao
na pensheni. Walimu wetu wengi wanaishi
wakiwa na shakawa (masumbuko).
Wataalamu wanasema hali ya namna hiyo,
hali iliyojaa dhiki inafupisha maisha ya
binadamu.
Natoa mwito kwa mamlaka zinazohusika
ziwatazame walimu wetu wote nchini kwa

jicho la huruma. Walipwe mafao na
pensheni zao kwa muda unaotakiwa
kisheria, maana kazi waliyoifanya kwa taifa
letu ni kubwa na inastahili kuenziwa.

..tamati…