Mwaka jana niliwaalika baadhi ya walimu wangu wapendwa walionifundisha shule ya msingi. Miongoni mwao alikuwamo aliyenifundisha darasa la kwanza.
Sina maneno mazuri ya kueleza furaha niliyokuwa nayo, na zaidi ya yote, waliyokuwa nayo walimu wangu. Pamoja nao, niliwaita baadhi ya wanafunzi wenzangu tuliosoma pamoja.
Lilikuwa tukio lililotutoa machozi ya furaha baadhi yetu tuliofundishwa na walimu hao miaka mingi iliyopita. Nilifanya hivyo ili kutambua, kuthamini, kuenzi na kusharifu mchango wao usiopimika – waliouweka katika maisha yetu.
Kati ya walimu zaidi ya 10 waliohudhuria, wawili tu ndio walikuwa hawajastaafu. Mmoja amestaafu Julai, mwaka huu.
Wakati wa mazungumzo yetu kilio cha walimu wangu hawa kilifanana. Kilio cha mafao na pensheni. Wote walizungumzia ugumu wa maisha baada ya kustaafu. Waliokuwa hawajastaafu shaka yao ikawa kwamba hayo yanayowapata wenzao yatawapata pia. Kweli, mmoja ameanza kuugulia maumivu. Tangu amestaafu Julai, mwaka huu, leo ni Oktoba hajapokea mafao wala pensheni.
Nilizungumza na walimu wangu, japo hawakutamka kuwa wananituma nikafikishe kilio chao kwa wahusika, maelezo yao yalitosha kunifanya nitambue kuwa wamenituma.
Nami kwa kutambua kuwa ni wao walionifundisha kusoma na kuandika, basi niwasilishe kilio hiki kwa mamlaka zinazohusika.
Kilio cha walimu wangu hawa ni tone tu katika bahari ya manung’uniko ya walimu kote nchini.
Nimepitia kauli za viongozi wetu wakuu na kusoma baadhi ya maneno na ahadi walizokwishatoa.
Desemba, mwaka jana Rais John Magufuli, akiwa Dodoma, alizungumza na walimu kwa urefu na mapana. Akawaahidi mengi yenye neema, na yeye akaeleza matarajio aliyonayo kutoka kwao kwa ajili ya ustawi wa taifa letu.
Miongoni mwa mambo aliyowatoa shaka ni lile la kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. Akasema michango yao ipo salama na mafao yao watayapata kama kawaida.
Kauli kama hii imekwisha kutolewa na wasaidizi wake pia ikiwalenga walimu na watumishi wa umma wengine.
Hata hivyo mafao na pensheni ya walimu vimeendelea kuwa kilio chao kikuu. Hali hii inawafanya waishi kwa taabu, hasa ikizingatiwa kuwa kada hii ni ya watumishi wasiokuwa na kipato kikubwa.
Walimu wengi, kwa asili ya kazi yao, wamejikuta wakistaafu wakiwa na maisha ya kawaida mno. Kwa sababu hiyo, hutegemea mafao na pensheni ili walau ziwasaidie kuhitimisha safari ya maisha yao duniani.
Katika kufuatilia kilio cha walimu, yupo mwingine aliyestaafu mwaka 2016, lakini hadi Aprili, mwaka huu alikuwa hajalipwa mafao. Nimeambiwa hadi wiki iliyopita alikuwa akiendelea kutaabika. Nimepigiwa simu na walimu wengi waliostaafu Julai, mwaka huu, kilio chao ni hicho hicho.
Walimu wengi hufika kwenye ofisi za malipo lakini majibu wanayopewa ni kuwa Hazina haijatoa fedha!
Kwa namna ya pekee nimeona niwakumbuke walimu kwa kuwafikishia kilio chao kwa wahusika nikiamini watatendewa haki, hasa ikizingatiwa kuwa kada hii ndiyo injini na chimbuko la maarifa, vyeo na tambo za wengi wetu.
Hakuna yeyote awaye miongoni mwetu anayeweza kutambia mafanikio aliyonayo bila kuwataja walimu waliomwezesha kuwa hivyo alivyo. Walimu ndiyo injini ya mafanikio yote tunayojivunia – mtu mmoja mmoja, jamii, taifa na hata ulimwengu mzima.
Walimu si watu wa kupata shida zinazoepukika kama hizi za kulipwa mafao au pensheni zao. Walimu si watu wa kuhangaika kwenye korido au ngazi wakibisha hodi mlango mmoja baada ya mwingine wakiulizia malipo yao, na wakati mwingine wakijibiwa vibaya.
Walimu si watu wa kutaabika kiasi cha kuwafanya baadhi yao wajinyonge kutokana na danadana za watumishi wanaostahili kuwatendea haki kwa mujibu wa sheria.
Walimu, kama walivyo watumishi wengine wa umma, kustaafu kwao kuko kwenye shajara. Inajulikana lini mwalimu aliajiriwa na lini atastaafu kwa mujibu wa sheria. Kama hivyo ndivyo, iweje mafao yao yasiandaliwe mapema – ikiwezekana mwaka mmoja kabla ya kustaafu ili muda wa kustaafu unapowadia apate stahiki zake mara moja?
Kwa hakika inatia simanzi kuwaona walimu waliokwisha kuzeeka wakitaabika njiani na ofisini kwa kufuatilia mafao. Inaumiza kuwaona wakipata ajali au wakikosa namna ya kuishi kwa sababu tu wamesafiri kutoka mbali kwenda Hazina, Utumishi au PSSSF kufuatilia mafao na pensheni zao.
Bahati nzuri tunaye rais ambaye kitaaluma ni mwalimu. Matarajio ya walimu wenzake ni kuona anawaondolea kero hii ya mafao na pensheni. Walimu wetu wengi wanaishi wakiwa na shakawa (masumbuko). Wataalamu wanasema hali ya namna hiyo, hali iliyojaa dhiki inafupisha maisha ya binadamu.
Natoa mwito kwa mamlaka zinazohusika ziwatazame walimu wetu wote nchini kwa jicho la huruma. Walipwe mafao na pensheni zao kwa muda unaotakiwa kisheria, maana kazi waliyoifanya kwa taifa letu ni kubwa na inastahili kuenziwa.