Wiki iliyopita nilichambua kwa kina kifungu cha 32 hadi 46A cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya madaraka ya Rais. Sitarejea niliyoyaandika lakini nashukuru kwa mrejesho mzuri wenye mshindo nilioupata. Wakati toleo hilo linatoka nilikuwa Lushoto mkoani Tanga, kwenye mafunzo yanayohusiana na masuala ya Katiba yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Mafunzo haya yanalenga kutafuta mbinu mpya za jinsi ya kuifanya Serikali ikubali kutunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari. Haki hii inapiganiwa kwa karibu miaka sasa lakini wakubwa wanaikalia. Nikupe kibwagizo mpendwa msomaji. Siku zote nilikuwa nikisifia Mlima wa Kitonga lakini nilichokiona Lushoto akina January Makamba wanajua. Wala sisemi. Si mlima ule ni balaa.

Naiacha Lushoto nikitumaini kuwa hatimaye MCT, kwa kushirikiana na wadau kwa mikakati tuliyoiweka, iwe isiwe Serikali itabana lakini mwisho wa siku itaachia. Hapa yatatokea yaliyowakuta Bayern Munich mbele ya Chelsea kwenye Klabu Bingwa ya Ulaya siku tisa zilizopita. Tunachodai sisi kama wanahabari ni haki ya kupata habari na si vinginevyo. Wala hatudai ukuu wa wilaya ama wa mikoa, tunataka mliopo huko itungwe sheria inayowawajibisha kutupa habari, basi.

Nikirejea katika hoja ya msingi kwa nini nadai Jaji Joseph Warioba ndani ya Katiba mpya ashawishi wenzake kuirejesha Tanganyika yetu, nasisitiza si ubaguzi wala kupinga na ‘Fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM’, bali ni kujipa fursa ya kufikiri tu na kuheshimu uhuru wa mawazo. Kwamba hivi leo Zanzibar ikipata kero ndani ya Muungano inazungumza, na nani mshirika wake katika Muungano?

Ukitaka kweli, Rais wa Muungano ndiye Rais wa Tanganyika kwa sasa, hivyo hata kama Zanzibar ingekuwa na sherehe inamkosa mshirika wake wa kuandaa naye shajara. Kitendawili hiki kilitukumba wakati tunasherehekea miaka 50 ya Uhuru. Ilikuwa kizungumkuti. Tunapotosha historia wazi wazi tena bila aibu hata kidogo.

Eti tunawaambia watoto wetu tunasherehekea Uhuru wa Tanzania Bara, wakati huo ni mchanyato wa aina yake. Ukitamka Tanzania tayari unakuwa umetamka Muungano wa maneno mawili – Tanganyika na Zanzibar. Kwa kuongeza neno Bara unakuwa tayari umezaa muungano mpya ndani ya Muungano uliopo wa nchi mbili, kwa maana unaongeza nchi ya tatu inayoitwa Bara.

Sijui hii ni akili ya wapi! Tuwe wakweli tu kwamba katika hili hizi zilikuwa fikra lakini si fikra sahihi. Busara ituongoze tu kuwa kama ni upotoshaji kiwango tulichopotosha kinatosha. Watoto wetu tusiwageuze mazuzu. Kwa utaratibu huu tutafika mahali tutapotosha na kuwaambia watoto wetu kuwa mababu zetu hawakuwahi kuuzwa utumwani. Hii si sahihi.

Narudia. Tuwe na Muungano wenye Serikali tatu – moja iitwe Tanganyika, ya pili iwe Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya mwisho iwe Serikali ya Tanzania. Kisha ndani ya Serikali hizi tuunde serikali za majimbo. Swali la jinsi ya kuimarisha umoja wetu tusipate mpasuko, nimelijibu katika makala zilizotangulia na zinapatikana katika wavuti yetu www.jamhurimedia.co.tz.

Swali moja tu najiuliza bila majibu, nalo ni kama Zanzibar hawaoni aibu kulinda historia yao ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 sisi nini kinatufanya tuone soni kutamka neno Tanganyika? Ajabu na kweli, sheria nyingi inazoongoza nchi hii zimeandikwa Tanganyika kama hazihusu Muungano. Wala leo sitahoji Mzanzibari Dk. Hussein Mwinyi kushika wadhifa wa Uwaziri wa Afya, ilhali sisi huwezi kuwa hata Sheha huko Zanzibar.

Kifungu cha 47 hadi 50 cha Katiba ya Tanzania (1977) ndicho kinachoanzisha wadhifa wa Makamu wa Rais. Vifungu hivi vinanikera. Makamu wa Rais pamoja na kutajwa kama msaidizi mkuu wa Rais, Katiba yetu ya sasa haimtambui kama sehemu ya Bunge. Siku akitaka kwenda Bungeni ili aweze kuingia kwenye ukumbi wa Bunge lazima Mnadhamu wa Chama tawala atoe hoja ya kutengua kanuni ya Bunge kumruhusu aingie bungeni.

Si hilo tu. Makamu wa Rais anabaki kuwa mtu wa kufungua semina na makongamano. Hizi zinazoitwa za Muungano mipaka yake haijulikani. Unakuta mazingira nayo anaingiliwa maana anajikuta wizara hiyo inasimamia mambo ya Tanganyika pia, akienda kwenye wizara nyingine anaweza akakutana na waziri mkorofi akamwambia yeye anashughulikia masuala ya Tanganyika hivyo hamhusu, na mengine mengi.

Kimsingi, Makamu wa Rais anajikuta hata Waziri Mkuu kwa ujiko ni zaidi yake. Hivi nani aliwahi kusikia Makamu wa Rais anakwenda popote katika nchi hii watu wakachachawa? Bajeti yake ni mkia wa mbuzi, hapewi fursa ya kuhutubia hata wabunge angalau mara moja ndani ya miaka mitano, yaani cheo hiki kwa sasa kilivyo ni ‘danganya toto’.

Wala sisiti kusema hata kikifutwa hakuna hasara tutakayoipata. Hapa ndipo ninaposema turejee katika misingi ya mkataba. Mkataba wa Aprili 26, 1964 uliliona hili. Ulibaini kuwa bila viongozi wakuu wa Tanganyika na Zanzibar kuwa wasaidizi wakuu wa Rais kwa utaratibu wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais, nchi ingekuwa inaelea.

Hoja dhaifu iliyotolewa kuwa upande mmoja wa Muungano unaweza kushinda chama kingine hasa CUF, kwa Zanzibar nadhani sasa tunao uzoefu wa kutosha kuipangua hoja hii. Angalia, kwa Zanzibar aliyeshinda ni Dk. Ali Mohamed Shein, lakini chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif Shariff Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais na mambo yanakwenda.

Vivyo hivyo chini ya mfumo wa Serikali tatu, Rais akitokea Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais anatokea Tanganyika na Makamu wa Pili anatokea Zanzibar. Sasa tatizo liko wapi? Mbona Zanzibar Dk. Shein na Maalim Seif wote wanatokea Pemba na mambo yanakwenda? Tuache woga. Tubadili haraka mfumo huu kwa kufuta cheo cha Waziri Mkuu katika ngazi ya Muungano, tubaki na makamu wawili wa Rais wamsaidie Rais na hawa makamu wawili ndiyo waongoze Serikali za Zanzibar na Tanganyika.

Najua wengi wanaifuatilia mada hii na wangependa kuona hitimisho. Kwa mantiki hiyo, wiki ijayo nitazungumzia Bunge, wabunge na Tume ya Uchaguzi. Usikose nakala ya Gazeti lako la JAMHURI.Tusione aibu kudai Tanganyika yetu kwa nia ya kuleta usawa na haki kwenye Muungano. Tuache mfumo huu usioelezeka kama umeshonwa kwa katani au nyaya.