*Mtendaji TBA aagiza afukuzwe alikopanga
*Yono wakabidhiwa kazi ya kumwondoa
*Amri ya Mahakama inayomlinda yapuuzwa
*Yeye asema hadaiwi, polisi wasita kumwondoa
NA MANYERERE JACKTON
Waziri Mkuu na Makamu wa Rais (mstaafu), Jaji Joseph Warioba, anafukuzwa kwenye nyumba alimopanga, mali ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), JAMHURI limethibitishiwa.
Jaji Warioba ambaye pia amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeamuriwa afukuzwe katika nyumba hiyo Na. 501/13 iliyopo Barabara ya Ghuba, Oysterbay, jijini Dar es Salaam kutokana na mgogoro wa kodi ya pango.
Taarifa kutoka TBA zinasema Jaji Warioba, kupitia kampuni yake ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates anadaiwa kodi ya pango ya Sh milioni 54.7; lakini taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo zinasema hadaiwi kiasi chochote cha fedha, kwani mara ya mwisho malipo ameyafanya ya mwaka mzima – Desemba 2017 hadi Desemba 2018.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, ameiandikia barua kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, akiiagiza itumie nguvu kuiondoa kampuni ya kiongozi huyo haraka iwezekanavyo.
Barua ya Mwakalinga ya Machi 19, mwaka huu ambayo JAMHURI limepata nakala yake, Mtendaji Mkuu huyo anawaagiza Yono kwa kusema, “Kwa barua hii unatakiwa kuandaa utaratibu wa kumuondoa kwa nguvu mpangaji huyu, ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha Polisi pamoja na taarifa kwa Serikali za Mitaa, kwani nyumba hiyo inahitajika haraka iwezekanavyo kwa ajili ya matumizi ya Serikali.”
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa chanzo cha mgogoro kwa pande hizo mbili ni uamuzi wa TBA kupandisha kodi kutoka Sh 700,000 hadi Sh milioni 3.5; kiwango ambacho kampuni hiyo ilisema ni kikubwa mno. Kwa kuheshimu mkataba wa awali usio na mgogoro, kampuni hiyo imeendelea kulipa kodi zote kuanzia mwaka 2001 hadi Desemba, mwaka huu.
Kutokana na mvutano huo, kampuni ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates ilifungua shauri katika Mahakama ya Ardhi, ikipinga ongezeko hilo la kodi ya pango.
Wakati shauri la msingi Na. 91/2014 likiendelea mahakamani, inaelezwa kuwa TBA walianza kufanya juhudi za kumwondoa mpangaji katika nyumba hiyo, na ndipo kampuni hiyo ilifungua kesi ya pili Na. 136/2015 kupinga hatua hiyo.
Desemba 30, 2015 Mahakama ya Ardhi chini ya Jaji Winfrida Korosso, ilitoa uamuzi wa kuzuia mpango wowote wa kuibugudhi au kuindoa kampuni hiyo kwenye nyumba husika hadi hapo kesi ya msingi itakapokuwa imetolewa uamuzi.
Hukumu hiyo inatoa maelekezo mahususi matatu, ikisema, “1. Mjibu maombi anapewa siku 14 za kujibu maombi; 2. Baada ya kupokea majibu, Mleta maombi ajibu (kama analo la kujibu) ndani ya siku 7; na 3. Kwa sasa hali ibaki kama ilivyokuwa ili Waombaji wasisumbuliwe au kuondolewa katika nyumba Na 501/13 iliyopo katika kona ya barabara za Haile Selasie na Ghuba, Oysterbay hadi Maombi ya Shauri la Ardhi No. 136 ya Mwaka 2015 yatakapoamuriwa. ”
Hadi sasa hukumu ya kesi hii haijatolewa. Kesi ya msingi imepangwa kuendelea katika Mahakama ya Ardhi mbele ya Jaji Edson Mkasimangwa mnamo Mei 28, mwaka huu. Wakili upande wa mlalamikaji ni Michael Ngalo.
Licha ya kuwapo hukumu ya Mahakama ya kuzuia kuiondoa kampuni ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates, TBA imeendelea kushikilia msimamo kwa kusema, “…Mpangaji alipewa notisi ya kusitisha mkataba na kukabidhi nyumba tangu Desemba 2015, jambo ambalo hajatekeleza hadi leo [Machi 19, 2018]. Pamoja na kutotekeleza agizo hilo amelimbikiza kiasi cha Sh 54,700,000.00 hadi Februari 2018.
Taarifa kutoka kampuni ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates, zinasema kodi zote za pango kwa muda huo ambazo ni Sh milioni 1.1 kwa mwezi zimekuwa zikilipwa kama kawaida, na kwamba hadi sasa haidaiwi senti yoyote. Fedha hizo zimekuwa zikiingizwa kwenye akaunti ya TBA kama ilivyokuwa kwenye mkataba baina ya pande hizo mbili.
Mwaka 2015 TBA hao hao walitaka kumwondoa Jaji Warioba, ila walitumia sababu nyingine. Kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. GC:2/210/043/II/4 iliyoandikwa Novemba 11 mwaka 2015, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo ya Serikali, Mhandisi Elius Mwakalinga, alimwandikia Warioba notisi akisema wamebadili matumizi ya jengo hilo.
“Hii ni kukuarifu kwamba nyumba hii inatakiwa na serikali kwa matumizi mengine hivyo tunakujulisha kuwa baada ya upangaji wako kuisha mwezi Desemba 2015, hatutaendelea na upangishaji wa nyumba hiyo,” aliandika Mwakalinga.
Mgogoro kati ya Jaji Warioba na TBA ulianza mwaka 2007 na ndipo wakakubaliana utaratiu mpya wa kulipa kodi. Maelezo yanaonyesha kuwa Kampuni ya Warioba ilitumia Sh milioni 50 kwa ajili ya matengezo na upanuzi wa jengo hilo.
Katika kesi waliyofungua Warioba na wenzake wanaonyesha kuwa mwaka 2007, kodi katika nyumba hiyo ilipandishwa kutoka Sh 150,000 kwa mwezi waliyokuwa wanalipa tangu mwaka 2001 na kufikia Sh 700, 000 kwa mwezi, kabla ya kupandishwa na kuwa Sh 900,000 kwa mwezi, mwaka 2009.
Kilichoharibu uhusiano kati ya pande hizi mbili ilikuwa ni hatua ya TBA kupandisha kodi ya nyumba hiyo kutoka Sh 900,000 hadi Sh milioni 3.5 mwaka 2013. Ongezeko hilo ni takribani mara tatu ya kiwango kilichokuwa kinalipwa awali.
Hata hivyo, wakati TBA sasa wakiitaka Yono iiondoe kampuni ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates, kwa nguvu, kuna taarifa kuwa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, umesita kutoa askari wa kusimamia kazi hiyo baada ya kubaini upungufu wa kisheria.
Kutoka Polisi Oysterbay, JAMHURI limeambiwa kuwa wiki iliyopita Yono walifika kuomba askari kwenda kumwondoa Jaji Warioba kwenye ofisi hizo, lakini ilishindikana baada ya kampuni hiyo ya udalali kukosa Amri ya Mahakama ya kuhalalisha hatua hiyo.
“Walikuja kuomba askari, tukaambiwa tujiandae kwenda kumwondoa Jaji Warioba, lakini baadaye tukaambiwa hilo haliwezekani kwa sababu hawana Amri ya Mahakama,” amesema mmoja wa polisi aliyekuwa atumike kwenye operesheni hiyo.
Jaji Warioba amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwapo msuguano huo, lakini hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo kwa kile alichoeleza kuwa suala hilo lipo kwenye vyombo vya kisheria.
“Ninyi Waswahili haya mambo mmeyapata wapi? Ni kweli hili shauri lipo, hata wiki ijayo tutakuwa mahakamani, kama ni habari basi msubiri ya kutoka mahakamani,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne, amezungumza na JAMHURI kuhusu sakata hili na kusema hakumbuki kuwapo kwa tukio la kuondolewa Jaji Warioba katika nyumba aliyopanga, lakini akasema hiyo haina maana halipo.
“Tunapokea matukio mengi ya aina hiyo, lakini ukweli ni kuwa tunasimamia sheria, hatuwezi kumwondoa mtu hivi hivi bila maelekezo ya mamlaka za kisheria. Inawezekana hilo jambo lililetwa ofisini na likaishia kwa askari wanasheria kwa sababu nimehakikisha tunafuata sheria.
“Waulize hao Yono walikuja na barua ya Mahakama? Kama hawakuja nayo, basi ujue hilo shauri linaweza likawa limeishia kwa askari wanasheria kwa sababu hatutaki kumwonea mtu au kufanya kazi kwa shinikizo.
“Unajua mtu anaweza kuja kuomba askari ili wasimamie kumwondoa mtu fulani mahali fulani, sasa kwa kawaida ya kazi zetu lazima tufuate sheria. Kitu tunachokifanya cha kwanza ni ku- cross-check (kuhakikisha) na Mahakama kama kweli kuna amri hiyo. Kama haipo hatuwezi kupeleka askari,” amesema na kuongeza:
“Polisi ni wasimamizi wa sheria, hilo naomba ulijue-tunapokea maelekezo ya kisheria kwa documents [nyaraka] za kimahakama-huwezi kuamka tu na uamuzi wako. Nikiletewa nitauliza amri imetolewa na chombo gani cha kisheria-na katika hili ni Mahakama.
“Atakuwa polisi wa ajabu kutekeleza jambo ambalo halipo kwenye miongozo ya kisheria. Yono wakuonyeshe order ya Mahakama kama wanayo uje nayo maana isionekane tumekataa maelekezo ambayo ni halali kisheria.
“Tunafuata mfumo wa kisheria ili kutenda haki kwa pande zote kwa mujibu wa sheria. Mimi sina kumbukumbu na hili unalonieleza, na kama walikuja bila order yawezekana waliishia kwa wanasheria wetu.”
JAMHURI limezungumza na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart, Stanley Kevela, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Scholastika Kevela, na wote wamekiri kupokea barua ya TBA ya kumwondoa Jaji Warioba kwenye nyumba husika.
Kevela amesema, “Polisi hawajakataa kutupatia ulinzi wa kumwondoa, lakini naomba hili suala tuliache kwa sababu tumepanga tukutane sisi [Yono], Jaji Warioba na TBA. Kwa sasa naweza kusema ni suala ambalo halijafanyiwa kazi. Naomba uwafuate TBA uwaulize-sisi tukitaka kumtoa hatushindwi.”
JAMHURI limemuuliza kama ni halali kisheria kumwondoa mteja ambaye kuna hukumu ya Mahakama inayozuia asiondolewe. Kevela amesema hajaiona hukumu, lakini akaongeza kwa kusema, “Chukua hukumu usome uone kama imezuia. Alipewa miezi sita ambayo imeisha kwa hiyo ni haki kumwondoa.
“Lakini TBA ni Serikali, kwa hiyo mpaka uone Serikali imechukua uamuzi huo ujue iko sahihi. Inayotolewa kwenye nyumba ni kampuni na siyo Jaji Warioba, Serikali mpaka imefikia hatua hiyo imejiamini kuwa iko sahihi. Nakushauri umfuate Mwakalinga [Mtendaji Mkuu TBA] atakueleza. Najua yako maongezi yanaendelea… tunaongea naye [Jaji Warioba]. Yeye hajatupa hiyo hukumu.”
Kuhusu kupewa polisi wa kuiondoa kampuni ya Jaji Warioba, Stanley anasema, “Tulipeleka maombi Polisi Oysterbay ya kupewa askari, lakini hatujapewa majibu, na hii kazi hatuifanyi bila polisi-sharti tupate ulinzi. Sisi ni wakusanyaji wa kodi za Serikali, nadhani CEO wa TBA atawafafanulia zaidi.”
Kwa upande wake, Scholastika, anasema, “ Tumepanga kukutana na Jaji Warioba na TBA Jumatatu (jana) au Jumanne (leo).”
Kuhusu zuio la Mahakama, anasema, “Hizi ni nyumba za Serikali, wengi wanaodaiwa wanatolewa. Hii ni Serikali na inaweza kumtoa mteja ambaye halipi kodi.”
Kuhusu kama wamepata Amri ya Mahakama inayokinzana na hukumu ya Jaji Korosso, Scholastika anasema, “Siyo lazima kibali cha Mahakama-siyo lazima TBA wanapotaka kumwondoa mteja wapite mahakamani kupata kibali. TBA ni mamlaka kabisa. Watu walizoea kufanya nyumba za Serikali shamba la bibi, hawalipi madeni.
“Kama anayo hukumu alete kwenye kikao tulichopanga, lakini najua kuna hukumu zina-expire [zinaisha muda]. Order kama ni ya miezi sita basi hiyo imeshaisha muda wake. Kama ana zuio aende TBA ambako kuna mawakili wa Serikali. Sisi kwa barua tuliyopewa na TBA ya kumwondoa huyo mpangaji (Jaji Warioba) iko sahihi kabisa.”
Mtendaji Mkuu wa TBA, Mwakalinga, ametafutwa kwa siku mbili bila mafanikio. Awali, ofisi kwake Dar es Salaam walisema amesafiri Dodoma. Hata hivyo, baadaye alijibu kwa ujumbe wa maandishi akisema: “Naomba. Ufike ofisini TBA Makao Makuu utapewa taarifa zote kama utakavyo uliza. Mimi kwa sasa niko Dodoma Kikazi, siwezi kukumbuka kila kitu. Ili uweze kupata taarifa za uhakika na sahihi, naomba uonane na niliyemwachia ofisi wakati huu sipo ofisini. Nakushukuru kwa taarifa. ”
JAJI WARIOBA NI NANI?
Jaji Joseph Sinde Warioba alizaliwa September 3, 1940 Bunda mkoani Mara. Amekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kuanzia mwaka 1985 hadi 1990. Amekuwa Jaji katika Mahakama ya Afrika Mashariki na pia Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
Amesoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966. Kuanzia mwaka 1966 hadi 1968 alikuwa Mwanasheria wa Serikali mkoani Dar es Salaam, na kuanzia mwaka 1968 hadi 1970 alikuwa Wakili wa Jiji la Dar es Salaam. Mwaka 1970 alihitimu Hague Academy of International Law. Kuanzia mwaka 1976 hadi 1983 alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kuanzia mwaka 1983 hadi alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mwaka 1985, alikuwa Waziri wa Sheria.
Amekuwa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Masuala ya Bahari, Hamburg, Ujerumani kuanzia mwaka 1996 hadi 1999. Mwaka 1996 Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mianya ya Rushwa-maarufu kama Tume ya Warioba.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuongoza waangalizi wa kimataifa kutoka nchi za Jumuiya Madola kwa ajili ya uchaguzi mkuu nchini Nigeria. Mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Novemba 2016 Rais John Magufuli alimteua kuwa Kansela wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.