Mkuu wa chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Joseph Sinde Warioba amezindua rasmi mashine ya kisasa ya kuchakata mazao ya misitu ijulikanayo kama Slidetec Sawmill 2020 yenye thamani ya shs 200 milioni.

Aidha uzinduzi huo umefanyika leo katika kampasi ya msitu wa mafunzo Olmotonyi ,Arusha ambapo mashine hiyo itaongeza uwezo wa uzalishaji sambamba na kuongeza tija katika mafunzo kwa wanafunzi kwa vitendo.

Hata hivyo uzinduzi wa mashine hiyo umeenda sambamba na ufunguzi wa mafunzo ya wajumbe wa Baraza la chuo na washiriki wa mafunzo kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja juu ya majukumu ya Bodi za Wakurugenzi au Mabaraza kwa kuzingatia miundo na mipango ya Taasisi wanazosimamia.

Aidha Warioba amewataka wajumbe wa baraza la chuo hicho kuhakikisha tafiti za masuala ya misitu,kilimo na uvuvi zinaendana na mabadiliko ya tabia nchi katika kutatua changamoto zinazohusiana na hali hiyo.

Amesema kuwa ,semina elekezi zinazotolewa kwa kila taasisi zina lengo la kuhakikisha ufanisi wenye tija ikiwemo weledi, uzalendo sanjari na matumizi sahihi ya fedha katika kuleta maendeleo chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA) ,Prof.Raphael Chibunda amesema kuwa , uwepo wa mashine hiyo mpya ina uwezo wa kuzalisha mbao mita za ujazo 10 hadi 15 kwa masaa 8 ambapo umeme ukikatika ina uwezo mkubwa wa kutumia trekta.

“Kwa mashine za zamani zilikuwa na uwezo wa kuzalisha mbao mita za ujazo 5 hadi 7 kwa masaa 11 ikilinganishwa na hii mashine ya kisasa ambayo ina uwezo mkubwa sana wa kuzalisha mbao nyingi na kwa wakati na uwepo wa mashine hii mpya utaongeza ufanisi mkubwa sana wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wetu ili wanapohitimu wakaweze kufundisha na wengine wasiokuwa na utalaamu wa kutosha juu ya mashine hizo za kisasa.”amesema .

Kwa upande wake ,Kaimu Rasi Ndaki ya misitu Wanyamapori na utalii,Agnes Sirima amesema kuwa,lengo la uwepo wa mashine hiyo ni kuongeza uzalishaji katika kufundisha wanafunzi wa shahada ya misitu na kuongeza uzalishaji kwani hapo awali kulikuwa na mashine mbili tu ambazo zilikuwa zinatumika kwa ajili ya mafunzo na uzalishaji ,hivyo uwepo wa mashine hiyo mpya utaongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa sana.

Sirima amesema kuwa, uwepo wa mashine hiyo utaongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa katika kufundisha wanafunzi kisasa zaidi ikilinganishwa na hapo awali ambapo zilikuwa na changamoto kutokana na kutumika muda mrefu.