Mashaka Mgeta

Alikuwa gwiji wa haki za binadamu, mwelekezi wa misingi ya utawala bora, mtetezi wa uhuru wa mihimili ya dola na mpigania haki za watu wanaoonewa; Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Robert Kisanga, amefariki dunia.

Januari 23, mwaka huu, mauti yalimkuta Jaji Mstaafu Kisanga akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa familia ya Jaji Kisanga, Dk Onesmo Kisanga, amesema chanzo cha kifo hicho ni ugonjwa wa saratani ya utumbo aliokuwa akiugua (Jaji Kisanga) kwa takribani miaka minne, kabla ya mauti kumkuta.

Kwa mujibu wa Dk Kisanga, jitihada kadhaa zilifanyika ili kuokoa maisha ya Jaji Mstaafu Kisanga, ikiwamo kupelekwa nchini India kwa matibabu ya kina zaidi. Ikampendeza Mungu hata akamchukua Januari 23, mwaka huu.

Jaji Mstaafu Kisanga ameshatangulia mbele za haki, mwanazuoni mbobezi wa sheria aliyelitumikia Taifa kwa kiwango cha juu cha uwazi na uadilifu, akijielekeza zaidi katika kuhakikisha nchi inakuwa na mifumo inayokidhi matakwa ya umma.

Wapo watu waliosoma na Jaji Mstaafu Kisanga, wapo waliofanya kazi pamoja, wapo walioishi naye na wapo waliowahi kukaa naye meza moja, wakila na kunywa.

Kwa upande mwingine, wapo waliofuatilia utendaji kazi wa Jaji Mstaafu Kisanga hasa kupitia vyombo vya habari, wapo waliomsikiliza akiwasilisha mada ama kutoa hotuba kwa hadhira na wapo wanaosoma maandiko yake.

Hivyo ni sawa na kusema Jaji Mstaafu Kisanga amewafikia maelfu ya Watanzania na watu wengine wenye mapenzi mema kwa njia mbalimbali. Unaposoma ama kusikiliza simulizi hasa baada ya kifo chake, ni rahisi kubaini karama alizojaliwa katika kuusimamia ukweli, kuuzungumza ukweli na kuutetea ukweli.

Jaji Mstaafu Kisanga hakuwa mwoga katika kuelezea jambo aliloliamini hasa likigusa maslahi mapana ya umma. Msimamo huo ulimfanya wakati mwingine kupata upinzani na kauli za kejeli ikiwamo kutoka kwa watu waliokuwa karibu naye, wakiwamo waliowahi kumkabidhi dhamana ya kutenda kwa maslahi ya nchi.

Ndiyo maana unapopitia simulizi mbalimbali za kuhusu maisha ya Jaji Mstaafu Kisanga, utaamini pasipo shaka kwamba si rahisi mambo mema aliyoyafanya yakaandikwa kwenye ukurasa huu, ama kwenye toleo moja la gazeti hili ikatosha. Yapo mambo mengi.

Miongoni mwa mambo ‘yaliyomfunua’ Jaji Mstaafu Kisanga, kwa utayari wake wa kuutumikia umma kwa maslahi mapana ya nchi, ni alipotangaza matokeo ya Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi “White Paper” juu ya maeneo mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi.

Jaji Mstaafu Kisanga alikuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo iliyoundwa mwaka 1998 na Rais wa Awamu wa Tatu, Benjamin Mkapa, ikawasilisha maoni ya wananchi katika maeneo tofauti, lakini lililogusa hisia za wananchi na waliokuwa katika utawala ni kuhusu muundo wa Serikali uliotakiwa kwa wakati huo.

Tume ya Jaji Kisanga ikawasilisha mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, kwa maana ya Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Rais wa wakati huo, Mkapa, ambaye alimteua Jaji Kisanga kuiongoza tume hiyo, akatupilia mbali maoni hayo na kumkosoa (Jaji Kisanga) kwamba hakutumwa kwa ajili ya hayo.

Jaji Kisanga ‘hakutikiswa’ na kauli ya Rais (mstaafu) Mkapa, hivyo alisimamia ukweli uliokuwapo kwamba hitaji la muundo wa Serikali halikutokana na fikra zake binafsi, bali maoni ya wananchi kwa Taifa lao.

Ripoti ya Tume ya Jaji Kisanga ilizua mjadala ukiwamo ulioripotiwa kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. Gazeti moja la kila siku nchini lilimhoji Jaji Kisanga kwa wakati huo, kuhusu msimamo wake baada ya Mkapa (akiwa Rais) kukataa na kukejeli mapendekezo ya tume hiyo.

Miongoni mwa majibu ya Jaji Kisanga kwa gazeti hilo linaloendelea kuchapishwa hadi sasa yalikuwa ‘…kama Rais (Mkapa) hataki kuyakubali mapendekezo ya tume yaliyotokana na maoni ya wananchi, basi ayachane.”

Jaji Kisanga alijiongezea heshima kwa jamii na jumuiya za kimataifa, si kwa sababu ya maoni kuhusu kuwapo muundo wa serikali tatu, bali kuusimamia ukweli uliotokana na maoni ya wananchi.

KESI YA NYAMUMA

Jaji Kisanga akajitokeza tena kwenye shauri lililofunguliwa na wananchi wa Kijiji cha Rwamchanga katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Shauri hilo likahusu malalamiko ya wanakijiji 135 kwa Tume ya Haki za Binadamu iliyokuwa inaongozwa na Jaji Kisanga, dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kwa wakati huo, Thomas ole Sabaya; Mkuu wa Kituo cha Polisi wa Serengeti, Alexender Lyimo; na uongozi wa Kijiji cha Bonchugu na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Wanakijiji hao wakaeleza kuwa kijiji hicho kilisajiliwa mwaka 1993 na mwaka mmoja baadaye (1994) sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji hicho ikachukuliwa na kufanywa Hifadhi ya Wanyama ya Ikorongo. Kijiji hicho kikabaki na eneo lililoitwa Nyamuma Iliyobaki.

Hatua hiyo ikadumu hadi Oktoba 8, 2001 pale wanakijiji hao walipotangaziwa kupitia kipaza sauti, kwamba walipaswa kuondoka kutoka eneo ‘lililomegwa’ ndani ya siku nne yaani Oktoba 12, 2001. Siku hiyo ilipofika, wakazi wa eneo hilo waliondolewa kwa nguvu huku mali zao hususani nyumba zikichomwa moto. Uhalifu huo ukafanyika chini ya usimamizi wa Ole Sabaya.

Zipo hoja na hatua nyingi zilizopitiwa kuhusu shauri hilo, hatimaye Tume ya Jaji Kisanga ikaamuru kupitia mapendekezo matatu ikiwamo wanakijiji hao kurejeshwa kwenye eneo lao na kulipwa fidia iliyofikia Sh milioni 800.

Hata hivyo, mapendekezo ya Tume ya Kisanga hayakupokewa kwa mtazamo chanya na mamlaka za utawala na kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa wakati huo, Andrew Chenge, Serikali ikatangaza kutoyatekeleza. Hiyo ilikuwa ni baada ya Tume ya Jaji Kisanga kusubiri majawabu hayo kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kutoa mapendekezo.

Pamoja na mambo mengine yaliyoendelea, kuanzia ombi la kuitaka Mahakama Kuu ikazie utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Kisanga, ikakataliwa, kisha shauri hilo kupelekwa Mahakama ya Rufani iliyoagiza shauri la wanakijiji cha Nyamuma Iliyobaki lirudi Mahakama Kuu ili lipangiwe Jaji mwingine na si wa awali, Projest Rugazia, ambaye awali alitupilia mbali shauri hilo.

SERIKALI KUSHTAKIWA

Mwaka 1992 Jaji Kisanga, akiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, akasimamia rufani ya madai ikiwahusisha Kukutia ole Pumbun kutoka jamii ya Wamaasai na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakati huo, hatua ya kuishtaki Serikali ilifikiwa baada ya kuiomba kibali Serikali yenyewe, ndipo baada ya kusikiliza pande zote akatoa uamuzi wa Serikali kushtakiwa kama inavyoshtaki.

Mashauri hayo ni miongoni mwa ukweli kuhusu namna Jaji Kisanga alivyokuwa mwadilifu, mkweli, jasiri na mwenye kuisimamia haki kwa watu wote, pamoja na kufikia uamuzi ulioweza kumuingiza katika mfarakano dhidi ya watawala wa wakati huo.

Mwenyezi Mungu ampumzishe katika usingizi wa amani-AMINA