Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeingilia kati mgogoro wa uongozi unaoendelea kufukuta ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kuanza kuzisikiliza pande zinazosigana.

Mgogoro huo umeibuka hivi karibuni baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kutaka kurejea kwenye nafasi hiyo baada ya kujiuzulu wadhifa huo mwaka jana kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM Alhamisi iliyopita, Profesa Lipumba alisema Katibu Mkuu wa CUF anataka kuiua CUF Tanzania Bara.

“Mimi nipo CUF bado, na ni mwenyekiti halali kwa mujibu wa Katiba na sina mpango wa kuhamia chama kingine,” anasema Lipumba. 

“Katibu Mkuu wetu anataka chama hiki upande wa bara kife kabisa na ibaki Chadema pekee yake, ndiyo maana anafukuza wabunge,” anasema Prof Lipumba.

Katika barua yake ya Septemba 2, mwaka huu, aliyomwandikia Katibu Mkuu wa CUF, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, anakiri kupokea malalamiko huku akiwataka kuwa watulivu.  

Barua hiyo ambayo JAMHURI imeiona inasema; “Ni dhahiri chama chenu kinakabiliwa na sintofahamu kubwa kutokana na malalamiko na maelezo yaliyowasilishwa kwangu kuhusu mkutano mkuu wa tarehe 21 Agosti, 2014 na Mkutano  wa Baraza Kuu wa tarehe 28 Agosti, 2016,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, msajili amewashukuru CUF kwa kuitumia ofisi yake kutatua mgogoro unaoendelea na kwamba ofisi yake imeahidi kutatua mgogoro huo kwa weledi unaostahili.

“Aidha, ninawaahidi kuwa nitatoa msimamo wangu mapema iwezekanavyo baada ya kupitia nyaraka zote zinazohusu suala hili na kutoa fursa ya kusikiliza pande zote mbili,” inasema sehemu ya barua hiyo iliyotiwa saini na Jaji Mutungi.

Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya mpito wa CUF, Julius Mtatiro, anasema baada ya Prof. Lipumba kukabidhi barua yake, mwezi huo huo chama kiliitisha mkutano wa baraza kuu na kuteua kamati ya uongozi ili kuweza kuendesha shughuli za chama, kamati hiyo iliongozwa na Twaha Taslima.

“Iliteuliwa kamati ya uongozi baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu, Twaha ndiye aliyekuwa akiiongoza na ilipewa miezi sita, baada ya miezi sita kwisha ikaongezewa muda mpaka pale tulipoitisha mkutano mkuu kwa ajili ya kufanya uchaguzi ambao yeye aliibuka,” anasema Mtatiro.

Anasema kuwa CUF imekuwa ikifuata sheria na taratibu, hakuna mtu aliyekiuka Katiba zaidi ya yeye na wafuasi wake wanaolazimisha kumrudisha katika wadhifa aliojiondoa mwenyewe.

Alipoulizwa kuhusiana na kupasuka kwa CUF, amesema kwamba Profesa Lipumba hawezi kukipasua chama hicho kwani siyo mali ya mtu binafsi, na kwamba katika Baraza Kuu lenye wajumbe 30 Bara ni wajumbe 8 tu wanaomuunga mkono na katika Mkutano Mkuu wenye wajumbe 400 kutoka Bara ni wajumbe 100 tu ndiyo wanaomuunga mkono, hivyo nguvu hiyo hana.

“Hiki ni chama cha siasa hakiwezi kupasuliwa na mtu mmoja, hilo haliwezi kutokea,” anasema Mtatiro.

Akijibu kuhusu kikao kilichofanywa na viongozi wa CUF pamoja na Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Mutungi, amekiri viongozi hao kukutana na Msajili, lakini hakuwa tayari kubainisha nini kilichojadiliwa kwa madai ya kuwa bado majadiliano yanaendelea na kwamba siyo busara kuyaanika hadharani kutokana na unyeti wake.