Jaji Lawrence Mugambi amepeleka kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili kuunda jopo la majaji litakalosikiza na kuamua suala hilo.

Katika uamuzi wake wa Ijumaa asubuhi, Jaji Mugambi alisema ombi hilo linaibua masuala mazito ya kikatiba ambayo yanahitaji kuwepo kwa jopo kusikiliza suala hilo.

Huku hayo yakiarifiwa ratiba iliyotayarishwa na Karani wa Seneti, inaonyesha kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi, Oktoba 17, atakuwa na saa nne kutoka saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya sababu za kushtakiwa na kikao kingine alasiri kwa mahojiano.

Katika kipindi hicho, mawakili wa Gachagua pia watapata fursa ya kuwaita mashahidi kwenye jukwaa hilo, ambao anaamini watasaidia kuokoa kazi yake. Timu yake ya mawakili inasema wana mashahidi kadhaa lakini hawakufichua majina yao.

Baada ya uwasilishaji wake, Maseneta watapata nafasi ya kuhoji na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa Gachagua, kabla ya kuikaribisha timu yake kutoa mawasilisho yao ya mwisho kwa saa moja.

Timu ya Bunge pia itakuwa na kipindi kama hicho cha kutoa hotuba yao ya mwisho. Kikao cha kupiga kura kinatarajiwa kuanza mwendo wa saa moja unusu jioni.

Siku ya Jumatano, timu ya Bunge la Kitaifa ikiongozwa na mwasilishaji wa hoja hiyo, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, pia itakuwa na muda sawa na ule wa Gachagua kuwasilisha kesi yao ambapo mashahidi kadhaa wataitwa kwenye kikao hicho.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau na aliyekuwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA Andrew Mulwa wako kwenye foleni kutetea hoja ya kuondolewa madarakani kwa Naibu wa Rais.